Mashaka Mgeta |
Dhana ya ‘kutumbua majipu’ ni isiyotofautiana
kiutekelezaji na kauli mbiu kama ‘kupiga vita wahujumu uchumi’ iliyoasisiwa
katika utawala wa Mwalimu Julius Nyerere, ama ‘ufagio wa chuma’ wakati Rais akiwa
Alhaj Ali Hassan Mwinyi.
Lakini kwa namna ya pekee, Rais Magufuli
akalitangazia taifa na dunia kwa ujumla, kwamba atahakikisha anaishinda vita
dhidi ya mafisadi wa aina tofauti wanaohujumu raslimali za umma, ili Tanzania
iwe mahali salama pa kuishi.
Akilihutubia taifa kutokea bungeni
mjini Dodoma, sura ya Rais Magufuli ilionyesha dalili za kudhamiria alichokuwa
akikitamka, kwamba hakikutoka akilini tu bali na moyoni pia.
Umma uliipokea hotuba yake kwa shangwe,
dunia iliitafsiri hotuba yake kama sehemu ya safari mpya kwa nchi za Afrika,
iliyofunguliwa na Rais Magufuli ili watawala wengine hasa katika mataifa
yaliyoghubikwa na ufisadi, wafuate nyayo zake.
Rais Magufuli akaiita dhamira yake hiyo
‘kutumbua majipu’. Mpaka sasa kutumbua majipu kumekuwa na maana halisi ya
kuwashughulikia mafisadi wa aina tofauti wa uhujumu wa mali na raslimali za
umma.
Ilikuwa mfano wa hadithi inayoanza huku
miongoni mwa wasikilizaji wakitarajia itaishia njiani pasipo kukidhi kiu ya
wao. Lakini ikawa jioni, ikawa asubuhi, Rais Magufuli bado `anatumbua majipu’ Anasafisha
uozo ndani ya sekta ya umma.
Walio wengi wanampongeza Rais Magufuli
kwa hatua iliyopo sasa na inayoendelea katika `kutumbua majipu’.
Wapo wanaomkosoa wakitumia kigezo kuwa
Rais Magufuli anatoa kauli zilizo mfano wa maagizo kwa mahakama, akiwakandamiza
watuhumiwa wanaokabiliwa na ‘kutumbuliwa majipu’.
Lakini wanaomtetea Rais Magufuli
wanaweka wazi kwamba hatua zinazofikiwa ni kujibu hitaji la kuchukua uamuzi
mgumu dhidi ya watumishi wa umma waliotumia mianya ya udhaifu wa sheria
zilizopo, ili kuliibia taifa na kujineemesha kulikopita ukomo, wakawa mfano wa
watu wanaoishi peponi!
Mbali na ‘kutumbua majipu’, Rais
Magufuli amefikia hatua ya kushusha kiwango cha kipato kwa watumishi wa umma,
waliokuwa wanalipwa mishahara minono, kwa wengine isiyolingana na majukumu ya
kazi zao.
Inapofikia hatua hiyo, Rais Magufuli anaistahili
pongezi. Anastahili kupigiwa makofi ikibidi kuimbiwa nyimbo za shangwe na
mapambio. Pamoja na mafanikio hayo, ipo haja kwa wasaidizi wake na jamii kwa
ujumla, kumsaidia. Tanzania haiwezi kujengwa na mtu mmoja ama kikundi cha watu
wachache waliopo Ikulu, kwenye baraza la mawaziri ama ndani ya Chama Cha Mapinduzi
(CCM).
Ujenzi wa taifa wenye tija unawahitaji
watu wa kada zote, Imani zote, itikadi za vyama vyote, wenye taaluma tofauti,
japo kutaja kwa uchache.
Kwa mfano haiwezekani kwa Watanzania
wote kushiriki mipango ya namna bora ya kukuza uchumi na kustawisha maisha ya
watu.
Ama wanasiasa wote, waandishi wa habari
wote, wabunge wote ama asasi zote za kiraia. Lakini kupitia kupazwa kwa sauti
ama kueneza maandiko yenye utashi mwema kwa nchi, serikali inaweza kuchukua
mambo ya msingi, ikayatumia kuboresha mipango ya wataalamu ili azma ya kuwa na
maendeleo endelevu ifikiwe.
Ni kwa hali hiyo, kada hizo hazipaswi
kufumba midomo yao kama ambavyo isivyostahili kufumbwa midomo yao. Wanapaswa
waachwe wakidhibitiwa kwa misingi ya Katiba na sheria zilizopo, kuteta ili
kutoa mchango wa kuchagiza kasi ya maendeleo ya nchi.
Kuachwa huru kwa kada nyingine zilizo nje
ya serikali, hakuna manufaa kwao binafsi bali kwa jamii pana wakiwamo waliomo
kwenye mifumo rasmi ya utawala wa nchi.
Ndivyo ilivyokuwa kwa taifa tangu
utawala wa Mwalimu Nyerere, ambaye baada ya kustaafu kwake alisema si kweli
katika miaka 24 ya utawala (viongozi wa serikali) hawakufanya mambo ya hovyo.
Ni kwa hali hiyo, kada zilizo nje ya utawala
zinapopewa fursa kutumia haki za kikatiba na sheria, kuikosoa, kuishauri na
kuielekaza serikali iliyopo madakarani, linakuwa jambo lenye tija na si udhaifu
kwa watawala. Kwa mfano, yapo mambo ya kufanywa baada ya ‘kutumbua majipu’, ili
kutoa jawabu la maisha bora kwa Mtanzania.
Kwa maana haitakuwa na maana sana ikiwa
ufanisi wa ‘utumbuaji majipu’ hautajibu hitaji la kuondokana na umasikini.
Ama kupunguza kipato cha ‘mabosi;
katika sekta ya umma hakutakuwa na tija ikiwa wenye kipato duni wataendelea
‘kusota’ wakishindwa kumudu gharama za maisha, wakajikuta wanaendelea kuambulia
mlo mmoja kwa siku.
Hongera Rais Magufuli kwa ‘utumbuaji majipu’.
Lakini umma unahitajika kumsaidia ili hatua hiyo ijibu hitaji la kuondokana na
umasikini.
0754691540
0 comments:
Post a Comment