UCHAMBUZI HURU
Mashaka Mgeta |
MWISHONI
mwa wiki iliyopita, wananchi kutoka maeneo tofauti za nchi walishiriki upimaji
afya ulioratibiwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, ukafanyika
kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja, Dar es Salaam.
Idadi ya
wahitaji wa vipimo vya afya ikazidi matarajio, kwamba kutoka watu 3,000
waliotarajiwa ikafika 15,000.
Kwa tafsiri
rahisi, afya ni ukamilifu wa binadamu kimwili, kiakili na kijamii na kutokuwepo
kwa maradhi. Akizungumza kwenye hafla ya mazishi ya aliyekuwa Mwandamizi
Mwandamizi wa Habari, marehemu Simon Kivamwo, Makonda akasema kutokana na
ongezeko hilo, alilazimika kuomba madaktari 90 kutoka Jeshi la Wananchi
Tanzania (JWTZ) ili ‘kuongeza nguvu’.
Inafaa
kumpongeza Makonda kwa ubunifu huo, licha ya changamoto nyingi zilizojitokeza
katika utekelezaji wa mpango wa kupima afya za watu.
Mpango wa
upimaji afya huo unaweza kutafsiriwa kwa namna nyingi tofauti, ingawa katika
ujumla wake, tafsiri hizo hazipaswi kubezwa, bali kumpongeza Makonda na watoa
huduma walioshiriki katika upimaji na tiba kwa waliopaswa.
Pasipo kuzijadili
changamoto ama namna utekelezaji wa mpango ulivyofanyika, ongezeko la wahitaji wa
upimaji afya limeibua taswira ya namna Taifa linavyokabiliwa na changamoto
zinazohusiana na afya za watu.
Ni wazi
kwamba kuna tatizo. Watu wengi kwenye maeneo tofauti ya nchi wanaathirika kwa
kuugua maradhi wasiyoyabaini, hususan kwa kukosa tiba inayostahili. Kwa sababu
hospitali za rufaa katika mikoa tofauti, ama zile za wilaya, vituo vya afya na
zahanati, zinapokosa madaktari ama watoa huduma wenye sifa zinazotambulika kwa
mujibu wa sera ya afya, haipaswi kujiaminisha kwamba taifa ‘lipo salama’.
Kumiminika
kwa wahitaji kutoka maeneo ya mijini na vijijini kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja
hakupaswi kuchukuliwa kama mafanikio ya utekelezaji wa mpango husika, basi kuwa
kielelezo cha kuwapo utashi wa kisiasa, utakaowezesha kutambuliwa zaidi kwa
umuhimu wa sekta ya afya kwa maisha ya watu.
Kama ilivyo
kwa mataifa mengi hususani barani Afrika, sekta ya afya haipewi kipaumbele sana
hata katika ahadi zinazotolewa nyakati za kampeni za Uchaguzi Mkuu. Inaelezwa
‘kijuu-juu’ kuhusu azma ya kuiboresha sekta hiyo, lakini ahadi nyingi
hazijikita katika mkakati usiotiliwa shaka, kwamba unajenga mazingira bora ya
kuiboresha sekta ya afya.
Mathalani,
sera ya afya ya mwaka 1990 iliyopitiwa mwaka 2007, imeweka bayana dira na makusudio
ya kuwa na zahanati kwa kila kijiji na kituo cha afya kwa kila kata. Je, tangu
kupitishwa kwa sera hiyo na marekebisho yake kadha wa kadha, ni hatua gani
Taifa limepiga katika kuhakikisha kuwa kila kijiji kina zanahati na kata kuwa
na kituo cha afya?
Ni ukweli
ulio dhahiri kwamba vipo vijiji vyenye zanahati na kata zenye vituo vya afya.
Lakini tathmini inayohusisha muda, rasilimali, vipaumbele na nguvu kazi, vinawiana
na idadi ya zahanati na vituo
vya afya
vilivyopo?
Hata pale
ambapo kuna zahanati, vituo vya afya na hospitali katika ngazi za wilaya, mkoa
na taifa, kuna idadi inayotosheleza ya wataalamu na vifaa tiba?
Je, mfumo
wa tiba unaotumika nchini ni rafiki kwa mwananchi hasa mlipa kodi masikini,
akiwamo anayeisikia sauti ya Makonda ikihamasisha mpango wa vipimo bila malipo,
yu radhi hata kutembea umbali mrefu kwa saa kadhaa, afike Mnazi Mmoja? Haifai kukosoa mfumo ama hali ya huduma za
afya nchini, lakini haipaswi kujiliwaza na kutembea kifua mbele kwamba taifa
‘lipo salama’ katika upatikanaji wa huduma hizo.
Mpango wa
upimaji afya jijini Dar es Salaam ni wa muda mfupi, ambao pamoja na kuwa wenye
tija, lakini hauwezi kukidhi vigezo vya kuwa endelevu na kuwafikia wahitaji wanaostahili.
Ni kwa
mtazamo huo, Serikali, wadau wa maendeleo, watunga sera, wawakilishi wa umma na
wadau wengine, wanapaswa kuunganisha nguvu za pamoja na kuiwezesha sekta ya
afya iwe yenye manufaa kwa mujibu wa haki inayomstahili kila raia.
Kuwapo
majengo ya zahanati, vituo vya afya na hospitali hakutakuwa na manufaa kama
taifa halitawekeza katika kuwaandaa wataalamu na kuwaandalia mazingira bora ya
kufanya kazi nchini badala ya kukimbilia nje.
Wataalamu
wanapaswa kujulikana kwa idadi inayohitajika, hata kama ni kuwalipia kwa
vipindi maalum ili ufike wakati nchi iwe na uwiano unaotakiwa kikanda na
kimataifa, kwa daktari mmoja kutibu wagonjwa. Kwa upande mwingine, taifa
linapaswa kuwekeza katika tiba na vifaa tiba katika ngazi za zahanati, kituo cha
afya na hospitali.
Mambo ya
msingi yatakaposhindwa kufikiwa na badala yake nchi ikajiridhisha kwa mipango
ya muda mfupi, hata kama ina tija kama ya upimaji afya ulioratibiwa na Makonda,
bado hatutakuwa katika njia nzuri ya kuboresha huduma hizo na kuzifanya kuwa
rafiki wa raia wengi. Hongera. Paul Makonda.
0754691540
0 comments:
Post a Comment