WAKATI Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa(pichani) akisema Serikali haiwezi kukubali hoja za kupungua kwa mizigo bandarini na kudorora kwa uchumi wa Taifa zilizotolewa bungeni na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe jana, mpaka itakapopata taarifa sahihi kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na Hazina, wadau wameitaka iachane na utaratibu wa kusubiri takwimu badala kuchukua hatua stahiki.
Waziri Mkuu alitoa kauli hiyo jana bungeni katika kipindi
cha Maswali ya Papo kwa Papo kwa Waziri Mkuu, baada ya Mbowe kumhoji kuhusu
mkakati wa Serikali kukabiliana na mdororo wa uchumi na kupungua kwa mizigo
kwenye bandari za Tanga na Dar es Salaam, huku kampuni za usafirishaji na
hoteli zikifunga biashara.
Takribani wiki moja iliyopita, Kamati ya Bunge ya Viwanda,
Biashara na Mazingira ilitembelea bandari ya Dar es Salaam na kubaini kwamba
mizigo inayoingia imepungua kutoka kontena 40,000 Agosti, mwaka jana hadi 1,000
katika mwezi kama huo mwaka huu.
Rais wa Chama cha Mawakala wa Forodha Tanzania (Taffa),
Stephen Ngatunga na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara, Johnson Minja
jana waliieleza JAMBO LEO sababu za mizigo kupungua na kuitaka Serikali
kukubali hali halisi na kuitatua.
Katika swali la nyongeza, Mbowe alisema BoT ilitoa ripoti
yake ya tathmini ya uchumi kwa miezi mitatu inayoonesha kushuka kwa
usafirishaji na uingizaji wa mizigo nchini, kuporomoka kwa sekta ya ujenzi na
mzunguko wa fedha.
Katika majibu yake, Majaliwa alisema Serikali itakutana
na wadau kujadili jambo hilo huku akieleza sababu za kupungua kwa mizigo
bandarini na jinsi nchi zilivyothibitisha kuanza kutumia bandari za Tanzania
kupitisha mizigo yao.
“Mizigo katika bandari na mipaka yetu imepungua kwa zaidi
ya asilimia 60, asilimia 40 ya baadhi ya kampuni za usafirishaji zimefunga kazi
zao, hivi hali hii Serikali inaijua? Inachukua hatua gani za makusudi za
kurekebisha hasa ikizingatiwa uchumi ukipo-romoka mazao ya wakulima nao
yanauzwa kwa bei ndogo?” Alihoji Mbowe.
Majaliwa alijibu akisema ni lazima Serikali ipate takwimu
kutoka taasisi zake hasa BoT na kuzilinganisha za miaka ya nyuma, ili kubaini
kama kweli kauli ya kushuka kwa uchumi ina ukweli.
“Serikali hii jitihada zake ni kuhakikisha uchumi unakua
katika nyanja zote. Kupungua kwa mizigo bandarini kumekuwa kukizungumzwa na
watu wengi, hata Kamati ya Bunge, lakini wadau peke yao hawatoshi, lazima
tupate taarifa kutoka ndani ya Serikali na mwenendo wa uendeshaji wa bandari na
mipaka yetu,” alisema Majaliwa.
Alisema Serikali itaendelea kupokea ushauri wa wabunge na
wadau kuhusu hatima ya uchumi wa nchi, ili kama kuna udhaifu ufanyiwe kazi na
kusisitiza kuwa mara zitakapopatika takwimu sahihi za uchumi, Bunge litajulishwa.
Akijibu swali la nyongeza la Mbowe, Majaliwa alisema wafanyabiashara
maarufu wa meli duniani walimweleza kuwa usafirishaji mizigo umeshuka duniani
kote, kutokana na kuporomoka kwa bei ya gesi na mafuta.
“Tanzania tunategemea mizigo kutoka Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Rwanda, Burundi na Zambia. Wote mnajua DRC na
Zambia ni nchi zilizokuwa zinaelekea kwenye uchaguzi na kulikuwa na migogoro
mingi… wiki iliyopita Rwanda na Kongo
walithibitisha kwa barua kuanza kutumia bandari zetu kupitisha mizigo,”
alisema.
Hata hivyo, Waziri Mkuu alisema tayari wafanyabiashara wa
Rwanda na DRC wameihakikishia Serikali kwamba mizigo yao yote itakuwa inapitia
Dar es Salaam hasa kwa mkakati wa pamoja wa ujenzi wa reli ya kisasa inayoanzia
Dar es Salaam-Tabora - Isaka.
Wadau
Minja alisema: “Kontena na mizigo haviingii bandarini kwa
sababu kodi zinazotozwa hazina uhalisia na hazifanani na wenzetu wa Afrika
Mashariki, gharama zinaingia kwa bei kubwa na kuuzwa kwa bei juu, hivyo wafanyabiashara
wanapata hasara.”
Aliitaka Serikali kusikiliza ushauri wa wadau huku akibainisha
kuwa kodi hazieleweki kwa maelezo kuwa kontena moja linaweza kutozwa kodi ya Sh
milioni 40, lakini kontena hilo hilo likiingia nchini baada ya wiki moja,
litatozwa kodi ya Sh milioni 60.
Ngatunga alisema Taffa walilizungumza suala hilo kabla
halijatokea, wakati linakaribia kutokea na sasa linatokea, lakini ushauri wao
ulipuuzwa.
Alitaja sababu tatu za mizigo kupungua bandarini kuwa ni
Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), mfumo wa himaya moja ya ushuru wa forodha na
kukosekana ushirikiano kati ya wao na viongozi wa Mamlaka husika.
Katika hatua nyingine, Majaliwa alisema Serikali ya Awamu
ya Tano iko macho, haijalala na haijashindwa kuongoza nchi bali imeji-panga
kuliongoza Taifa kwa mafanikio makubwa.
“Serikali haijashindwa kuongoza nchi. Nataka niwahakikishie
wabunge na wananchi wote,” alisema.
0 comments:
Post a Comment