Mashaka Mgeta
JUZI, Ikulu ya jijini Dar es Salaam ilitoa taarifa mbili, moja ikielezea ziara ya Rais John Magufuli nchini Zambia, baadaye ikaelezea kuahirishwa kwake.
JUZI, Ikulu ya jijini Dar es Salaam ilitoa taarifa mbili, moja ikielezea ziara ya Rais John Magufuli nchini Zambia, baadaye ikaelezea kuahirishwa kwake.
Ziara hiyo iliyopangwa ‘kuchukua’ siku tatu, huku ratiba ikihusisha
kushiriki kuapishwa kwa Rais Edgar Lungu, ilifutwa ili Rais Magufuli
ashughulikie kadhia ya kuibuka kwa tetemeko la ardhi lililotokea na kugharimu
maisha ya Watanzania zaidi ya 16.
Ninamuomba Mwenyezi Mungu awapumzishe katika usingizi wa Amani wote
waliotutoka, na kuwaondolewa maumivu majeruhi wa janga hilo.
Lakini tukio la Rais Magufuli kuahirisha ziara yake nchini Zambia kutokana
na kadhia ya tetemeko ni jambo jema, lile ambalo linaashiria na kuchagiza ari
kwa Watanzania na dunia kujali utu wa mtu.
Ingawa Rais Magufuli amewakilishwa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu
Hassan, ile kuwapo kwake nchini wakati huu taifa likiomboleza vifo, majeraha,
upotevu wa mali na kadhia nyinginezo zinazotokana na tetemeko hilo, inatia faraja.
Ni faraja ambayo haipaswi kutokana na asili ya tukio, kwamba ni
tetemeko ambalo halikutarajiwa, ni faraja ambayo haipaswi kuwa katika msingi wa
namna watu walivyoangukiwa na kuta, wakapoteza maisha ama kujeruhiwa.
Ni faraja ambayo haipaswi kutokana na kutafuta na ‘kuziteka’ hisia
za watu. La hasha. Rais Magufuli, kwa hatua hiyo anauleta utu wa mwanadamu katikati
ya mioyo ya watu.
Utu wa mtu unapojengwa kwa raia wa taifa kama Tanzania, inakuwa
kichocheo chema cha ‘kusimika’ umoja wa kitaifa, ushirikiano, utulivu na amani
ya kweli.
Kwa hiyo wakati Rais Magufuli akiwasilisha kielelezo hicho kwa
kujali tatizo lililoikabili nchi badala ya kwenda kugongesha glasi za shangwe kwenye
jiji la Lusaka kusherehekea kuapishwa kwa Rais Lungu, inabidi tafakari iliyopo
ivuke mipaka kutoka Bukoba mkoani Kagera.
Kwamba wapendwa wetu kadhaa wamepoteza maisha kutokana na tetemeko la
ardhi. Janga hilo ni la asili ambalo ni vigumu kuzuilika hata kwa mataifa yenye
nguvu kubwa za kijeshi na uchumi ulioimarika.
Lakini ukweli unabaki kuwa janga limeyachukua maisha ya watu wetu
kama wanavyopoteza maisha ndugu wengine ama itakavyokuwa kwetu kupitia magonjwa
kama malaria, vifo vya watoto na wajawazito, japo kutaja kwa uchache.
Kwa hiyo tunaweza kujiweka kando na uwezekano wa kudhibiti janga la
asili kama tetemeko lililotokea Bukoba. Lakini kama taifa inabidi utashi wa
kisiasa na dhamira ya mtu mmoja mmoja vielekezwe katika kulifanya taifa
lisiingie katika simanzi kama iliyopo sasa, kwa kudhibiti vifo vinavyoweza kuzuilika.
Kuvizuia vifo visivyotokana na majanga ya asili ni pamoja na kuwapo
kwa sera, sheria, kanuni na taratibu bora, zikichangiwa na ushiriki wa kila
kada ya kijamii badala ya kuwaachawatawala ili mwisho wa siku
wasutwe ama kunyooshewa vidole.
Tetemeko la Bukoba linapomuibua Rais Magufuli kuahirisha ziara yake
huko Zambia, linakuwa fundisho kuwa Tanzania ni moja na Watanzania ni wamoja.
Kwamba tunapozungumzia tetemeko hilo, waathirika wake si wakristu
tu, waislamu tu, watu wa kabila fulani ama au chama cha siasa.
Ni Watanzania kwa asili yao, tumeathirika, tumepoteza ndugu, mali
na miundombinu kuharibika. Kumbe sasa kupitia maisha ya ndugu waliolala katika
usingizi wa milele, ama wale wanaoumia katika majeraha makali wengine
wakipoteza viungo vyao, Watanzania wana wajibu wa kuiona nchi ni zaidi ya
maslahi ya tofauti zilizopo.
Kwamba kama ilivyo kwa tetemeko, taifa ‘likitikiswa’ kwa namna
nyingine yoyote, waathirika wake ni Watanzania na si vinginevyo.
Mathalani, kama uchumi ukiyumba kiasi cha raia kushindwa kumudu
gharama za maisha, ni Watanzania wote watakaoathirika. Kama ni kupotea kwa
amani na utulivu uliopo, waathirika ni raia wote katika upande wowote wa nchi.
Ama kama ambavyo taifa limeletwa pamoja kupitia shida zinazotokana na
tetemeko la ardhi, Watanzania wanahitaji kuwa pamoja katika maisha ya kawaida,
kuanzia ngazi za familia hadi taifa.
Haiwezekani Watanzania wakalilia kutokuwapo hali ya kuridhisha nchini,
pasipo kujitafakari katika hali ilivyo katika ngazi tofauti za kijamii. Kwa mfano,
Rais Magufuli anapoahirisha ziara nje ya nchi, inatoa tafisri gani kwa baba ama
mama anayekabiliwa na shida kwenye familia yake, lakini akaendelea ‘kutumbua maisha’
kwenye maeneo ya starehe ama vilezi?
Rais Magufuli ameonyesha njia, kwamba haifai. Ninaamini kwamba kwa
tukio la tetemeko hilo, nchi italetwa pamoja, ili tofauti za Watanzania ziwe
katika hoja na si mapigano.
Kwa maana mapigano yanaleta mauti yasiyotofautiana na
yanayoshuhudiwa kwa ndugu waliokufa kutokana na tetemeko la ardhi, kasha nchi
kuingiwa na simanzi. Tanzania haihitaji simanzi hasa zinazotokana na tofauti za
kijamii kama siasa, imani nakadhalika. Tanzania haihitaji kutojali utu wa mwanadamu,
hivyo kusudio jema lipate kujengwa kuanzia ngazi ya familia hadi taifa.
Mwenyezi Mungu awapumzishe ndugu zetu waliokufa katika tetemeko la
ardhi huko Bukoba-
AMINA.
0754691540
0 comments:
Post a Comment