MAMLAKA ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) imesema itaanza kutoa vitambulisho vipya vya Taifa vyenye saini kwa wananchi waliokamilisha taratibu za usajili na utambuzi na kuchukuliwa alama za kibiolojia.
Kwa mujibu wa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa NIDA, Andrew
Massawe (pichani) uchukuaji wa vitambulisho hivyo utaanza kesho kwenye ofisi
zote za Mamlaka hiyo zikiwamo za wilaya zilizoanza usajili Zanzibar na mikoa ya
Dar es Salaam, Pwani, Lindi, Mtwara, Morogoro, Tanga, Arusha, Kilimanjaro na
Ruvuma na wabunge Dodoma.
Alisema waombaji wote ambao vitambulisho vyao viko tayari
watatumiwa ujumbe mfupi wa maandishi kupitia simu zao kufahamishwa kufika
kwenye vituo vya usajili kuvichukua.
“Mamlaka inakusudia kubadilisha vitambulisho vyote vya
zamani visivyo na saini, ila kwa sasa vya zamani vitaendelea kutumika pamoja na
vipya wakati taratibu za kuvibadilisha zikiendelea,” alisema.
Alisema kutokana na uwepo wa njia nyingi na salama za
kusoma taarifa za mwombaji ndani ya kifaa maalumu kilichofichwa kwenye kadi ya
mtumiaji, ndiyo sababu vitambulisho vya zamani vitaendelea kutumika kwa huduma
mbalimbali zinazohitaji kutambua mtumiaji kabla ya kupata huduma.
Akizungumzia wananchi ambao hawakusajiliwa, Massawe
alisema kwa mikoa ambayo tayari kuna ofisi za usajili, waliwata kuendelea kujitokeza
kusajiliwa kwani ni kazi endelevu.
Alikumbusha wananchi kutunza vizuri vitambulisho vyao ili
kuepuka gharama kwani kitambulisho cha Taifa kwa mara ya kwanza kitatolewa bure
na kikipotea, ili kupata kingine lazima mtumiaji alipie.
Alisema kwa sasa vitambulisho vya Taifa vimeanza kutumika
katika baadhi ya huduma nchini hususani kwenye benki kufungua akaunti na
kuthibitisha taarifa za mtu kabla ya kupewa huduma, pia taratibu za kupanua
wigo wa matumizi ya vitambulisho kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali
zinaendelea.
0 comments:
Post a Comment