JICHO LA TATU:
UMRI ni chuo. Unavyoishi unaona
mengi na unaelemika katika vitu vingi. Kadiri binadamu wanavyoishi, ndivyo
wanavyofanya makosa mengi. Wingi wa makosa huongeza uzoefu na mzoefu ni
mwanazuoni.
Uanazuoni pia unatofautiana viwango.
Kama ilivyo chuo kikuu kulivyo na shahada, uzamili na uzamivu, ndivyo na uzoefu
ulivyo. Kama utafanikiwa kufumaniwa mara nyingi ndivyo na uanazuoni wako
unavyokua, kutahamaki unafikisha PhD ya kufumaniwa.Yaani wewe ni daktari wa
falsafa za kufumaniwa.
Unaweza kuwa na PhD lakini ukaishia
tu kuitwa daktari (dokta), lakini ukivuka viwango zaidi, unaitwa profesa.Na
profesa yeyote ni mwalimu wa kiwango cha juu katika taaluma yake chuo kikuu.
Umri ni elimu; Tendo moja la kipuuzi
likifanywa na watu wa aina tatu tofauti, tafsiri pia hutofautiana. Akifanya
mtoto hupuuzwa kwa maneno “ni utoto, akikua ataacha”, ikiwa ni kijana husemwa
“damu inachemka, ujana maji ya moto,” kwa mzee mwenye fainali yake kama
isemwavyo fainali uzeeni, yeye husikitikiwa “mzee anazeeka vibaya.”
Maisha kila hatua kuna mitihani.
Anayeishi miaka mingi kwa yakini anakuwa amekuwa amejaza majibu mengi. Kila
hatua ina mafundisho, mitihani, majibu na ufaulu wake. Ukimuona mzee anafanya
vituko, anafumaniwa au anajihusisha sana na mapenzi na vitoto, hapo kuna
mawili, ama kuna mitihani aliruka au alikuwa anaibia majibu. Inawezekana pia
alighushi matokeo.
Kawaida, mtu ambaye anaishi
maisha yake umri huwa haudanganyi. Atajidanganya kwa utoto wake, atakosea kwa
ujana wake lakini akishazeeka anakuwa mzoefu wa kujidanganya na utoto wake,
vilevile anakuwa na majibu ya makosa aliyofanya katika ujana wake, kwa hiyo
hawezi kurudia makosa, maana ni mwanazuoni tayari.
Miss Tanzania 2006, Wema Isaac
Sepetu ni mwanazuoni sasa wa mapenzi. Jinsi anavyolia leo kukumbuka penzi la
aliyekuwa boyfriend wake, marehemu Steven Kanumba, inatosha kuonesha kuwa
amepitia mengi ya kumfunza.
Mapenzi yana tabia ya kuwafanya
watu wajute. Huwalazimisha watenda makosa wajutie makosa yao wakati ambao muda
umeshapita. Wenye kustahili kujuta, hujuta katika nyakati ambazo haiwezekani
kurudisha wakati nyuma. Wahenga walimaliza waliposema, majuto mjukuu!
Mfano leo hii Wema anamlilia
Kanumba, atampata wapi? Mungu alishamchukua miaka minne iliyopita. Na hata
wakati Kanumba anafikwa na mauti, hakuwa na Wema kimapenzi.
Kanumba na Wema wana visa vingi
vya mapenzi. Nakumbuka kisanga cha Kanumba kuharibiwa gari na Wema. Siwezi
kusahau pia kuwa Kanumba alimshtaki Wema polisi na kumsababishia alale
mahabusu.
Kanumba alifariki dunia Aprili 7,
2012, ilipofika Septemba 15, mwaka huu, Wema alichukua picha yake ya zamani
aliyopiga na Kanumba, kweli ya zamani na muonekano wao wakiwa wadogo, Wema
akaandika: “Penzi langu la kweli la kwanza. Wanasema unapata penzi la kweli
mara moja katika maisha.
“Kama ndivyo, vizuri siwezi
kupingana na ukweli kuwa anayo nafasi muhimu kwenye moyo wangu. Baada ya Mungu
kumchukua, nina chumba kingine kwa ajili ya mpenzi mwingine wa kweli. RIP Steve
wangu.”
Maneno hayo ya Wema ndiyo
yamenifanya niamini kuwa sasa amekua. Amepata uzoefu wa mapenzi. Kama mapenzi
ni taaluma basi amekuwa mwanazuoni aliyekomaa. Ni kipindi ambacho anayajua
mapenzi ya kweli na udanganyifu wake. Na ndiyo sababu sasa anamkumbuka
Kanumba.
Siwezi kusema kweli Kanumba alimpenda sana Wema, maana Bongo Movie
na mapenzi yao wanajuana wenyewe. Ila naweza kukiri kuwa Kanumba alihangaika
mno kwa ajili ya Wema.
Alikuwepo muigizaji wa kike anaitwa Asha Jumbe.
Asha naye ana kaka yake anayeitwa Jumbe Yusuf. Mbele ya macho ya
Kanumba, Wema akamtolea udenda Jumbe. Penzi lenye nguvu likachipua na kuchukua
nafasi kubwa kati ya Wema na Jumbe.
Mama Wema, Mariam Sepetu, akaona mwanaye anapotea. Akalipiga vita
penzi la Wema na Jumbe usiku na mchana.
Wema akajichimbia Tabata na Jumbe wake. Kanumba akawa anahangaika
huku, mama Wema anarusha maneno kule. Wema haambiwi hasikii kwa Jumbe.
Nakumbuka ilikuwa mwaka 2008, nikiwa mhariri wa gazeti moja la
kila wiki, Wema alinipigia simu baada ya kuona kile ambacho mama Wema alikuwa
amekisema na kuandikwa gazetini. Akasema naye anataka kufunguka.
Nilimwambia Wema nipo tayari kumsikiliza, akanielekeza Tabata
alipokuwa anaishi, nami nikaondoka na timu yangu tukamfuata. Tulimkuta Wema
na Jumbe, alikuwepo pia Asha.
Wema alieleza jinsi alivyoanza uhusiano na Jumbe, akasema alipomuona
tu alijikuta anavutiwa naye. Akasema yeye hampendi Kanumba. Zikafuata tambo za
Jumbe kuwa Kanumba hamuwezi na kwamba alishampiga walipokutana.
Maneno hayo ya Wema na Jumbe ndiyo yaliyoamsha hasira za Kanumba,
akaenda polisi kushinikiza Wema akamatwe kwa sababu aliharibu gari lake.
Zilikuwa nyakati mbaya mno kwa watu waliopendana kufikia tamati ya aina hiyo.
Haina haja kugusia baada Wema kuachana na Jumbe alienda kwa nani
na nani, ila nina stori ya mwaka 2011 Dodoma. Timu ya Bongo Movie ikiwa Dom,
mimi pia nilikuwa kwenye shughuli zangu za uandishi. Kilikuwa kipindi cha vikao
vya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kipindi hicho Nasibu Abdul Juma ‘Diamond Platnumz’ ametoka kutwaa
tuzo tatu za Kili (KTMA), na wimbo unaotamba ni Mbagala, Wema tayari mpenzi wa
Diamond kwa wakati huo.
Nayakumbuka mazungumzo jinsi ambavyo Wema alikuwa akijaribu
kuzungumza na Kanumba japo kawaida, Kanumba akawa anamjibu kuwa anaogopa
kufanya mazungumzo na mke wa mtu kwa sababu hakuna asiyejua uhusiano uliopo
kati ya Wema na Diamond.
Kanumba akaniuliza: “Eti Luqman, nani asiyejua kama sasa hivi Wema
ni mke wa Diamaond? Wengine tuna damu mbaya, naweza kukaa pembeni na Wema,
halafu ikasemwa mimi na Wema tumerudiana, mimi sitaki kabisa.”
Mimi hata sikuchangia neno, nilibaki najichekelesha tu! Maana
ningeweza kumuunga mkono Kanumba, kumbe alisema vile kwa sababu aliniona nipo
karibu. Na ningemshauri Kanumba akubali kuzungumza na Wema pembeni, Diamond
angesikia si angekwenda kunikalia kikao Tandale? Sikutia neno kabisa.
Hata hivyo, baada ya kuona maneno hayo, na nikikumbuka sura ya
Wema siku ile akimbembeleza Kanumba wazungumze, napata picha ni kwa kiasi gani
mrembo huyo alimpenda godfather huyo wa Bongo Movie ambaye alikatika kama
utani.
Kama Kanumba angekuwa hai, ningempigia simu na kumshauri akae
chini na Wema wazungumze, lakini haiwezekani. Siku zimepita na haziwezi kurudi
nyuma. Nayaona maumivu ya Wema anapomkumbuka Kanumba wake.
Maneno ya Wema leo, yanaonesha jinsi ambavyo anatamani siku zirudi
nyuma asimsaliti Kanumba kwa tamaa za kijana mwenye rasta Jumbe. Hata hivyo
hayo hayawezekani tena. Hiki ndicho kipindi hasa ambacho Wema anaona makosa
aliyofanya. Maana miaka imepita hamkumbuki Jumbe, anamkumbuka Kanumba.
Wema katoka na wangapi wenye kujulikana? Ni wengi tu lakini kwa
nini anamuwaza Kanumba kama mtu aliyekuwa na penzi la kweli kwake? Ni kwamba
baada ya mitihani mingi, ameweza kuelimika kwa kiwango cha kutosha.
Mitihani mingi ya kimapenzi, kutoka Kanumba kisha katikati kupita
akina Jumbe, Charlz Baba, Diamond, Hartmann Mbilinyi, Idris Sultan na wengine
ambao hajataka kuwaweka wazi, kwa hiyo sasa amekuwa mwanazuoni.
Maneno ya Wema kukiri kuwa Kanumba ndiye penzi lake la kweli la
kwanza na kusema mtu huwa anapenda mara moja maishani, yanaonesha Wema tayari
anamiliki shahada ya uzamivu (PhD) ya mizungu ya mapenzi.
Ni PhD ambayo inaweza sasa kumuongoza kuishi vizuri kimapenzi,
maana amevuka mitihani mengi, kwa hiyo anayo majibu mengi kuhusu changamoto za
mapenzi.
Wema anaweza kuwa mshauri kwa wengine, kwamba wakikutana na
changamoto kama alizopitia wafanye nini ili kuvuka salama. Binafsi nimeanza
kumwamini Wema kwa uanazuoni wake.
Ni shule pia kwa watu wengine wote kuwa wanapokuwa na wapenzi
wanaowapenda, watulie nao, dunia ina vishawishi vingi hii. Uaminifu ni
kujizuia.
Ndimi Luqman Maloto
0 comments:
Post a Comment