Paul Makonda |
Makonda alikuwa akitolea ufafanuzi taarifa anayodaiwa
kuitoa kwa wakuu wa wilaya kukamata wanaolala kwenye nyumba za wageni muda wa
kazi.
Alisema: “Kulala mchana si kosa, msako unaofanyika ni wa
kutafuta wahalifu ambao wengi hukaa kwenye nyumba za wageni ili kufanya uhalifu
usiku.”
Hata hivyo, baada ya ufafanuzi wa Makonda baadhi ya
wananchi walipinga msako huo wakidai ni vigumu kugundua wahalifu na wasio
wahalifu ndani ya nyumba hizo hivyo msako huo utaumiza wasio na hatia.
“Kauli za Makonda mara kadhaa zimekuwa zikileta
mkanganyiko katika jamii, anatoa ufafanuzi kwamba si wanaolala mchana, lakini
ni msako wa wahalifu katika nyumba za kulala wageni, hivi unawezaje kujua
kwamba huyu ni mhalifu na mwingine sio?’’ alisema Ludovick Materu wa Temeke.
Alisema polisi wanapofanya msako huchukua watu wote
walioko kwenye nyumba, hivyo kusababisha usumbufu kwa wananchi wasio na hatia
ambao wamepumzika.
Katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya
Dar es Salaam, limesema litaendelea na operesheni dhidi ya watuhumiwa
wanaofanya biashara ya nyumba za wageni kinyume cha sheria.
Hatua hiyo imefikiwa baada ya Jeshi hilo kubaini kuwa
baadhi ya nyumba zimekuwa zikitumika kuhifadhi wahalifu, dada poa na kaka poa,
hivyo Polisi inawajibika kufuatilia na kuwakamata.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotumwa jana kwa vyombo vya
habari, Kamanda wa Kanda hiyo, Simon Sirro alisema ni wajibu wa Polisi kufanya
ukaguzi wa mara kwa mara kwenye nyumba za wageni, hoteli, migahawa, vilabu vya
vileo, kumbi za starehe zinazokesha na zisizokesha.
“Kimsingi niwatoe hofu raia wema kuwa tunaendelea na
operesheni za kusaka watuhumiwa wakiwamo wanaofanya biashara ya nyumba za
wageni kinyume cha sheria, majambazi na wahalifu wengine,”alisema.
Aliwataka wenyeviti wa serikali za mitaa na wajumbe wa
nyumba kumi kuwajibika kutambua wageni wote wanaoingia kwenye himaya zao na
kuwachukulia hatua stahiki ili kuimarisha usalama.
*Imeandikwa na Sharifa Marira, Hussein Ndubikile na Salha
Mohamed
0 comments:
Post a Comment