Magendela Hamisi |
Baada ya kubainika idadi kubwa ya watoto wanaoishi katika
mazingira hayo, katika mikoa mbalimbali hapa nchini hususan maeneo ya mijini
kumekuwa na mikakati mbalimbali ya kulitafutia ufumbuzi suala hilo.
Dar es Salaam ni moja ya majiji hapa nchini ambalo
limekuwa likiweka mikakati mara kadhaa ya kuwaondoa watoto hao. Hata hivyo
hakuna matunda ya mikakati hiyo baada ya watoto hao kuendelea kuongozeka badala
ya kupungua.
Hakuna sababu za moja kwa moja zinazobainishwa kuwa zinachangia
ugumu wa kudhibiti watoto hao kwenda mijini na kubaki huko, licha ya kuwa wengi
wanasema hakuna mipango madhubuti ya kukomesha tatizo hilo.
Zipo baadhi ya sababu zinazojulikana kuwa ndizo chanzo
cha baadhi ya watoto kukimbia katika familia zao na kwenda kuishi katika
mazingira hatarishi ambazo ni pamoja na ugomvi baina ya baba na mama ambapo
mwisho wa siku wanalazimika kutengana na hivyo watoto hao kukosa uangalizi.
Hata hivyo, baadhi yao watoto wamekuwa wakijiingiza
katika vitendo vya uhalifu inayosababisha Serikali kutumia nguvu kubwa kudhibiti
uhalifu unaojitokeza kwenye maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam na mikoa
mingine.
Mfano siku chache zilizopita mmoja wa viongozi wa Jeshi
la Polisi nchini alinukuliwa na vyombo vya habari akibainisha kuwa moja ya
sababu za kuwepo vitendo vya uhalifu hususan ‘panya road’ ni baadhi ya watoto
wa mitaani ambao wamekuwa wakijiingiza katika makundi hayo.
Hivyo, kutokana na jitihada nyingi kukwama za kuwaondoa
au kuwasaidia watoto wanaoishi katika mazingira magumu, jana Waziri wa Afya,
Ummy Mwalimu, alinukuliwa na vyombo vya habari akisema kuwa kwa sasa serikali
inajipanga kuhakikisha wanafanya mchakato wa kuanza kuwachukua ili kuwapeleka
katika mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT).
Binafsi napongeza mchakato huo kwa maana utasaidia
kupunguza watoto wanaoishi mazingira hayo magumu kuzagaa mitaani ambao wengine
wanaishia kutumbukia katika kujiunga na makundi ya uhalifu jambo ambalo
linakuwa na hasara kwa familia na Serikali kwa ujumla. Pia utasaidia
kuhakikisha vijana hao wanaweza kujiajiri kutokana na mafunzo watakayopata
hususan ya ujasiriamali watakayopata wakiwa katika mafunzo ya JKT ikiwemo
kilimo, ufugaji kuku na ufundi wa aina mbalimbali utakaosaidia kuwaweka kando
na vitendo viovu.
Wakati mwingine hata kama watashindwa kujiajiri wenyewe
wanaweza kuajiriwa katika kampuni mbalimbali za ulinzi jambo ambalo litasaidia
wao kuishi vizuri pamoja na kutunza ndugu zao.
Kutokana na kuwepo kwa mkakati huo wa kuwaingiza JKT,
watoto wanaoishi katika mazingira magumu kuanzia wenye umri wa miaka 18 ni vema
ukafanywa kwa umakini ili kuhakikisha kuwa wanaopata nafasi hiyo ni wale wenye
sifa kwa maana upo uwezekano wa baadhi ya wahusika wa kusaili watoto hao
kutumia nafasi hiyo kuwaingiza wasio wahusika.
Natoa tahadhari hiyo kwa kuwa vijana wengi wanahitaji
nafasi za kujiunga na JKT kwa kuwa wanaamini ni moja ya sehemu ya njia sahihi
ya kujiunga na majeshi mengine ya ulinzi na usalama jambo litakalosaidia
kuwahakikishia ajira Serikalini.
0 comments:
Post a Comment