Suleiman Msuya na Elizabeth Mwaseba
BARAZA Kuu
la Uongozi la Taifa la CUF, limemfukuza uanachama aliyekuwa Mwenyekiti wake
Profesa Ibrahim Lipumba likieleza kujiridhisha kwamba amekiuka Katiba ya chama.
Baraza hilo
limetaja makosa mengine kuwa ni Lipumba kuvamia Ofisi Kuu ya CUF, kuongoza
makundi ya wahuni yaliyopiga walinzi wa chama, kuvunja ofisi za chama na
kufanya uharibifu wa mali za chama siku ya Septemba 24 mwaka huu.
Pamoja na
viongozi wakuu wa chama hicho kutopokea simu kuthibitisha taarifa hiyo, baadhi
ya wajumbe ambao hawakupenda majina yao yatajwe, walisema ni kweli Lipumba
amefukuzwa kama mwanachama na si kiongozi.
“Baraza
limejiridhisha kuwa kikao cha Kamati ya Utendaji kiliitishwa kwa kufuata
masharti ya Katiba na hakikuvunja masharti yoyote ya kuitisha Baraza Kuu na limejiridhisha
kuwa Profesa Lipumba alifikishiwa barua yenye tuhuma zake, lakini kwa makusudi alikiuka
kuitika mwito wa Baraza na hivyo kupoteza haki ya kusikilizwa,” ilisema taarifa
hiyo iliyotumwa na Ismail Jussa kwenye ukurasa wake wa Facebook jana jioni.
Taarifa
hiyo ilinukuliwa pia na Julius Mtatiro ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya
Uongozi wa CUF.
Aidha,
taarifa hiyo ilisema Baraza lilikataa ushauri na mwongozo wa Msajili wa Vyama
vya Siasa, Jaji Francis Mutungi kwa chama kwa sababu ulikiuka matakwa ya Sheria
ya Vyama Vya Siasa, hauna mantiki na mashiko ya kisheria na unakiuka matakwa ya
Katiba ya CUF.
Taarifa
hiyo ilieleza kuwa Baraza Kuu linasisitiza kuwa Kamati ya Uongozi iliyoundwa
ndiyo inayotambulika kikatiba hadi atakapochaguliwa Mwenyekiti mpya wa CUF.
Aidha,
mmoja wa wajumbe ambaye hakutaka jina lake litajwe, alisema katika mkutano huo
uliofanyika kwa takribani saa tatu akidi ilitosheleza, ambapo kati ya wajumbe
62 waliopaswa kuhudhuria, 45 walifika huku watatu wakitoa udhuru.
Alisema
wajumbe wawili ambao ni Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti, hawakuhudhuria kwa
sababu chama hicho hakina viongozi hao, baada ya Lipumba kujiuzulu na Makamu
Mwenyekiti Juma Duni Haji kuhama chama.
Mjumbe huyo
alisema wajumbe saba walisimamishwa kwenye kikao cha Baraza kilichofanyika
Agosti 28 na wajumbe watano hawakutoa taarifa ya kutohudhuria.
Alisema
katika kikao hicho, ajenda zilikuwa tatu; kufungua kikao, kumjadili Lipumba na
uharibifu wa mali za ofisi na barua ya Msajili ya kuelekeza CUF kumtambua
Lipumba kama Mwenyekiti.
Juzi Kamati
ya Uongozi ya CUF ilimwandikia bara Lipumba kumwita mbele ya Baraza Kuu ahojiwe,
lakini alisema hawezi kwenda kwa sababu Mwenyekiti wa Kikao ambaye ni Katibu
Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad hayupo.
Wakati
akitoa majibu hayo, Seif aliwasili Zanzibar juzi usiku na jana akashiriki kikao
hicho ambacho kilifanya uamuzi wa kumfukuza.
Wakati
uamuzi huo ukitolewa, Profesa Lipumba aliitisha mkutano wa wanachama Dar es
Salaam kuwaambia wananchi sababu za kurudi kwenye uongozi wa chama hicho
tofauti na awali kuwa alijiuzulu.
Profesa
Lipumba alieleza sababu zilizomfanya ajiuzulu kuwani chama hicho kumezwa na
Ukawa, huku Chadema ikichanua. “Lakini nilishangaa kuona wakati wa kampeni za
uchaguzi mwaka jana, Chadema ikipita kila jimbo na kusema Ukawa ni Chadema tu,
hivyo kuigawa Tanganyika na Zanzibar kimafungu,” alisema.
Alisema
sababu nyingine ni kuwa wakati wa kikao, Katibu Mkuu Maalim alipata kusema kuwa
Freeman Mbowe na Lipumba hawamhitaji Dk Wilibrod Slaa hivyo kumtaka yeye
agombee urais.
Wakati wa
kipindi cha uchaguzi aliuliza kama wamejiandaa kuweka wagombea wakati yeye ni
kiongozi wa chama. Alisema CCM ilishaambiwa kila kitu na Katibu wa chama chao,
hivyo wana CUF hawana mgombea wa chama na wanategemea makapi ya CCM.
Mwenyekiti
alisema yeye bado ni mwanachama wa CUF na ataendelea kuwa Mwenyekiti, hivyo
wanachama wasiwe na wasiwasi.
“Mimi sina
matatizo na Katibu Mkuu na tunamsubiri aje kuendelea na kazi yake. Akae akijua
atakaporejea atanikuta mimi Mwenyekiti na tutaendelea na kazi, kwani meza yake
na viti vipo, lakini ajue kabisa kuwa nina nafasi yangu ya uenyekiti wa chama,”
alisema Lipumba.
0 comments:
Post a Comment