William Shao
KUKIWA na majonzi yaliyosababishwa na tetemeko la ardhi
mkoani Kagera na kusababisha vifo na uharibifu wa mali, kitabu cha The WorldBook Encyclopedia kinasema “matetemeko ya ardhi ni mojawapo ya matukio
yanayosababisha uharibifu mkubwa zaidi duniani.”
Utafiti mwingine unadai kuwa nishati ya tetemeko kubwa la
ardhi inaweza kuwa mara 10,000 zaidi ya bomu la kwanza la nyuklia.
Jambo hilo linaogopesha zaidi kwa kuwa tetemeko linaweza
kutokea katika tabia yoyote ya nchi, msimu wowote, na saa yoyote na mahali
popote. Ingawa wanasayansi wanaweza kufahamu kwa kiasi fulani mahali ambapo
tetemeko lenye nguvu litatokea, hawawezi kutabiri litatokea lini.
Ijumaa ya Machi 11, 2011, nchi ya Japan iliathiriwa na
tetemeko kubwa la ardhi lenye ukubwa wa 9.0 kwenye kipimo cha Richter.
Tetemeko hilo lilisababisha Tsunami (mawimbi makakubwa ya
baharini yaliyosababishwa na tetemeko) yaliyosababisha madhara makubwa. Ni
bahati tu kuwa tetemeko kubwa la mfano huo ni nadra kutokea. Utabiri wa kutokea
kwa tetemeko la ardhi kwa usahihi ungeweza kuokoa maisha ya watu wengi.
Hata hivyo, uwezekano wa kujua kutokea kwa tetemeko la
ardhi baadaye kunaweza kutabiriwa kwa kutumia takwimu za kisayansi.
Ni jambo jema kujua kama matetemeko ya ardhi yanaweza
kutabiriwa ili wakazi wa maeneo yanayoathiriwa waweze kujiandaa. Ni jambo jema
zaidi ikiwa utabiri huo unaweza kutaja mahali na wakati. Watafiti katika Jumuia
ya Jiolojia nchini Marekani (USGS), wanaamini kwamba huenda ukafika wakati
wakaweza kutabiri matetemeko ya ardhi kwa asilimia 67.
Pamoja na kuwapo kwa jitihada nyingi za kisayansi za
kutafuta njia ya kutabiri kutokea kwa matetemeko hayo, bado wanasayansi hao
hawajaweza kugundua ishara ya kutokea kwa hali hiyo, na wanakiri kuwa hakuna
ishara ya wazi inayoweza kuonesha kuwa kuna tetemeko litakalotokea karibuni.
Mtikisiko unaweza kugunduliwa muda mfupi kabla ya tetemeko kutokea, lakini hiyo
haitoi muda wa kutosha wa watu kujiandaa.
Matetemeko ya ardhi hutokea kwa sababu ya kusonga kwa
miamba mikubwa ambayo iko chini ya uso wa dunia. Miamba hiyo husonga daima.
Mara nyingi, mawimbi ya tetemeko la ardhi ambayo hutokea
huwa dhaifu kiasi kwamba hayawezi kutambuliwa waziwazi kwenye uso wa dunia,
lakini yanaweza kutambuliwa na kurekodiwa na kipima tetemeko. Nyakati nyingine,
miamba mingi huvunjika na kusongasonga kiasi cha kutetemesha ardhi.
Wanasayansi wa USGS na mashirika mengine ya utafiti wako
katika jitihada kubwa ya kuendeleza mbinu zitakazowasaidia kutabiri tetemeko la
ardhi. Ingawa hadi sasa utabiri huo umekuwa mgumu, watafiti hao wana matumaini
kuwa hatimaye watagundua ili kuokoa maisha ya watu wanaouawa kutokana na
tetemeko.
Kwanini kipimo cha Richter? Tetemeko la ardhi linaweza
kupimwa kulingana na ukubwa au kiwango chake. Katika miaka ya 1930, Charles
Richter alibuni kipimo cha kuonesha ukubwa wa tetemeko la ardhi.
Wakati vituo vya kupima tetemeko la ardhi vilipoongezeka,
vipimo vipya vilibuniwa kwa kutumia uvumbuzi wa Richter. Mfano, kipimo cha
nguvu za tetemeko la ardhi huonesha kiasi cha nishati kilichosababishwa na
chanzo cha tetemeko la ardhi. Vyovyote iwavyo, bado watafiti hawajagundua mbinu
ya kutabiri tetemeko la ardhi kabla halijatokea.
0 comments:
Post a Comment