Mary Mtuka
TAMKO la
Septemba 23, mwaka huu lililotolewa na Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis
Mutungi, limekitibua Chama cha Wananchi (CUF) baada ya kuhalalisha uenyekiti wa
Profesa Ibrahim Lipumba aliyesimamishwa uanachama.
Jaji
Mutungi ametoa msimamo na mwongozo wake kuwa wanachama wengine waliosimamishwa
pia ni halali na viongozi walioathirika kutokana na uamuzi wa kikao cha Baraza la
Uongozi la CUF, Agosti 28, mwaka huu, ni viongozi halali.
Ingawa
tamko hilo halali kwa mujibu wa sheria, limetokana na utekelezaji wa majukumu
ya Ofisi ya Msajili, lakini mapokeo yaliyoakisi fununu za kuwapo upendeleo kwa
Profesa Lipumba, ‘yamekoleza moto’ wa mzozo wa kisiasa kwa chama hicho.
Jaji
Mutungi akatumia vifungu vya Sheria ya Vyama vya Siasa, vikiwamo 10(f) sura ya
258, 8A(1) na kanuni ya 5(1) ya Kanuni za Usajili wa vyama hivyo, toleo namba
111 la 1992, kufanya upembuzi wa hoja zilizofikishwa ofisini kwake.
Hoja hizo
zilikuwa za upande wa Profesa Ibrahim Lipumba na wenzake wanaopinga kufukuzwa
na kusimamishwa uanachama, na majibu ya uongozi wa CUF kuhusu uamuzi unaolalamikiwa.
Hatimaye, Jaji Mutungi akaandika, “hivyo baada ya upembuzi kama nilivyobainisha
hapo juu, msimamo na mwongozo wangu ni kwamba, Profesa Ibrahim Lipumba bado ni
Mwenyekiti halali wa Taifa wa CUF…”
Kwa tamko
hilo, Profesa Lipumba akarejea Makao Makuu ya CUF Jumamosi iliyopita,
akisindikizwa na wafuasi wake na askari polisi waliokuwa kwenye magari matatu.
CUF
imeitisha kikao cha Kamati ya Utendaji itakayojadili msimamo na mwongozo wa
Jaji Mutungi kuhusu Profesa Lipumba kurejea katika nafasi yake ya awali, huku
kukiwa hakuna dalili za kukubalina na mlezi huyo wa vyama vya siasa.
Wakati
Kamati ya Utendaji ikikutana leo, moja ya shughuli zake zikielezwa ni kumhoji
Profesa Lipumba kwa ‘uhalifu’ alioufanya ofisi za chama hicho, Buguruni jijini
Dar es Salaam, Jumamosi, hali iliyopo sasa ni kama kusema ‘CUF imetibuka’.
Shughuli
zinazofanyika sasa, kauli za viongozi na malumbano ya baada ya tamko la Jaji
Mutungi, havikielekezi chama hicho kwenye mwelekeo bora wa siasa.
Ndio maana
Mwenyekiti wa chama cha ACT-Wazalendo, Anna Mghwira, anasema kinachoendelea
ndani ya CUF ni sawa na ‘biashara haramu’ inayoweza kukiua chama hicho.
Anaasa kuwa
ni wakati muafaka kwa wanaoifanya biashara hiyo wakajulikana na kwamba ni aibu
kuvumilia kasoro hizo ziendelee ndani ya chama hicho.
Lakini
aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila, anaielezea hali ya kisiasa
iliyopo hivi sasa ndani ya CUF, inahitaji ushiriki wa mahakama ili kupata
suluhu na si Msajili anayedai kutokuwa na mamlaka ya kuchukua hatua
alizozitangaza. Kwa mujibu wa Kafulila, Msajili anapaswa kushauri kwa mujibu wa
sheria na si kuchukua hatua kama alivyofanya Ijumaa iliyopita.
Mtazamo huo
unafanana na ule wa Mbunge wa Tandahimba (CUF), Katani Katani na Mhadhiri wa
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Onesmo Kyauke wanaomkosoa Jaji Mutungi kwa
uamuzi wake. Katani anasema tukio la Profesa Lipumba kurejea CUF akisindikizwa
na polisi, muda mfupi baada ya kutambuliwa na Jaji Mutungi, ni sawa na
‘kutumika’ kukiharibu chama hicho.
Anaeleza
kushangazwa kwake na hatua ya polisi kulinda kile alichokiita kuwa maandamano
ya Profesa Lipumba kurejea CUF, licha ya kuwapo katazo la kufanyika kwake
(maandamano). Kwa upande wake, Dk Kyauke anamkosoa Jaji Mutungi kwa uamuzi wa
kumtambua Profesa Lipumba, kisha anakishauri chama hicho ‘kukimbilia’
mahakamani.
Agosti 5,
mwaka jana Profesa Lipumba alitangaza kujiuzulu uenyekiti wa CUF kwa madai ya
kukerwa na hatua ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kumkaribisha Waziri
Mkuu mstaafu, Edward Lowassa.
CUF pamoja
na vyama vingine vya Chadema, NCCR-Mageuzi na NLD viliunda Ukawa ukiasisiwa
kutoka kwenye Bunge Maalum la Katiba. “Nafsi yangu inanisuta hivi sasa
kuendelea na uongozi huku waliokuwa wanaipinga rasimu ya Katiba ya Jaji Joseph
Warioba (Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba) wakikaribishwa kuwania
uongozi wa nchi kupitia Ukawa,” akasema.
Hata hivyo,
Profesa Lipumba alitengua kujiuzulu huko, lakini CUF iliendelea na mchakato wa
uchaguzi wa kuziba nafasi yake, hali iliyozua vurugu ambazo hazijatulia hadi
sasa.
Pamoja na
Profesa Lipumba, wanachama wengine waliosimamishwa ni wabunge Magdalena Sakaya
(Kaliua) na Maftaha Nachuna (Mtwara Mjini). Pia wamo Naibu Mkurugenzi wa Habari
Taifa, Abdul Kambaya, na wajumbe wa Baraza Kuu la Uongozi la Taifa (BKUT) la
CUF, Masudi Mhina, Thomas Malima, Ashura Mustafa, Kapasha Kapasha na wanachama
Musa Kombe, Habibu Mnyaa na Haroub Shamis.
Suala la
msingi ni uamuzi utakaofikiwa na Kamati ya Utendaji ya CUF ili kuwasilishwa
kwenye vikao vya juu ikiwa ni sehemu ya kufikia uamuzi unaoweza kukoleza
mgogoro uliopo sasa, ama kuufikisha tamati na chama hicho kuendelea na shughuli
za kawaida.
0 comments:
Post a Comment