Fidelis Butahe
MWENYEKITI wa chama cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia (pichani) amemtaka Rais
John Magufuli kuwachukulia hatua waliotajwa katika kashfa ya Akaunti ya Tegeta
Escrow na IPTL akieleza kwamba wakati sakata hilo lilipoibuka bungeni, kiongozi
mkuu huyo wa nchi alikuwa waziri hivyo anawajua wote waliohusika.
Mbatia ambaye pia ni mbunge wa Vunjo amehoji; iweje Rais Magufuli alitengua
uteuzi wa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga kwa sababu ya
kujibu swali bungeni akiwa amelewa na sasa anashindwa nini kuwatumbua waliotajwa
kupata mgawo wa fedha hizo?
“Bunge lilitoa maazimio manane kuhusu Escrow, mpaka sasa utekelezaji
wake unasuasua. Tunashuhudia utumbuaji majipu tu kwa watendaji mbalimbali,
lakini hatuoni chochote kuhusu wahusika Escrow na IPTL, kwa hili vipi Rais Magufuli?”
alisema.
Mbatia alitoa kauli hiyo baada ya kuulizwa kuhusu hukumu ya Baraza
la Usuluhishi la Benki ya Dunia kulitaka Shirika la Ugavi wa Umeme (Tanesco)
kuilipa Benki ya Standard Chartered Hong Kong (SCB-HK) zaidi ya Sh bilioni 320.
Uamuzi wa baraza hilo umekuja takribani miaka miwili tangu Serikali
iliporuhusu kiutatanishi kufanyika kwa malipo ya zaidi ya sh bilioni 350 kutoka
katika akaunti hiyo iliyokuwa imefunguliwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kwenda
Kampuni ya Harbinder Singh Seth ya Pan African Power Solutions Tanzania Limited
(PAP).
Akaunti hiyo ilifunguliwa BoT kuhifadhi fedha za malipo ya umeme
kusubiri kumalizika kwa mzozo wa kimkataba baina ya Kampuni ya IPTL na Tanesco.
Malipo hayo tata yalisababisha Bunge kutoa maazimio manane, ikiwa
baada ya ripoti yake na ile ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali
(CAG) kuwasilisha bungeni na wahusika kuonekana kuhusika moja kwa moja au kwa
kushindwa kutekeleza majukumu yao.
“Hatuna viongozi wa kweli na mfumo ni uleule uliotekwa na dhana ya
kujadili watu. Katika Escrow Rais Magufuli alikuwa sehemu ya maazimio ya Bunge
akiwa waziri wa ujenzi,” alisema Mbatia na kuongeza:
“… Alikuwa katika Baraza la Mawaziri na anajua uamuzi wa Kikwete
(Jakaya-Rais mstaafu) kuwaondoa akina Tibaijuka (Profesa Anna) na Muhongo
(Profesa Sospeter) na anajua kuwa maazimio ya Bunge lazima yaheshimiwe.”
Alisema Rais Magufuli tangu alipoingia madarakani ametumbua majipu
mengi lakini ameshindwa kuwatumbua waliohusika katika sakata la Escrow na IPTL.
“Nawatahadharisha watawala, wajue leo wapo, lakini kesho hawapo. Tungezingatia
maazimio ya Bunge, haya yasingetokea. Hii ni kwa sababu ya kubebana na
kulindana,” alisema.
0 comments:
Post a Comment