TAHARIRI
KAMA kuna jambo linaweza kuwashitua na kuwasikitisha Watanzania katika kipindi hiki kigumu cha wenzao kuendelea kuugulia maumivu ya tetemeko la ardhi mkoani Kagera, huku Serikali ikifanya kila njia kuwasaidia, wanatokea watu kuwaibia misaada.
Jana vyombo
karibu vyote vya habari nchini, viliripoti taarifa za vigogo watatu mkoani
humo, kufungua akaunti inayofanana na iliyofunguliwa na Serikali kwa ajili ya
kuchangisha fedha za kusaidia waathirika wa tetemeko hilo na wao kukusanya
fedha na kuzitumia binafsi.
Taarifa hiyo
ambayo iliikariri Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu, iliwataja Katibu
Tawala wa Mkoa wa Kagera, Amantius Msole, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa
ya Bukoba, Steven Makonda na Mhasibu Mkuu wa Mkoa, Simbaufoo Swai.
Watatu hao
wanadaiwa kufungua akaunti zingine mbali na ile rasmi ya Serikali na kutumia
jina hilo hilo la ‘Kamati Maafa Kagera’ kwa lengo la kujipatia fedha. Kwa kuwa kwa
mujibu wa Rais John Magufuli jana walifikishwa mahakamani hatutaingia kwa
undani kuhusu suala hilo.
Kama kweli
hilo limetokea, ndilo ambalo Rais Magufuli mara nyingi amekuwa akilikemea na
kuliita ni upigaji dili, lakini hili linauma zaidi, kwa sababu dili hizo
zinapigwa kwenye migongo ya waathirika ambao hivi sasa hawana nyuma wala mbele.
Matukio
kama haya ya kutumia fursa potofu kama hizi, yamekuwa yakiripotiwa sehemu
nyingi na hayana tofauti na wale ambao hukimbilia sehemu za ajali na badala ya
kuokoa watu, huwapora mizigo na fedha mifukoni bila soni wala huruma.
Mengine ni
kama yanayojitokeza misibani kwa baadhi ya watu kujifanya wana majonzi, lakini
wakitumia fursa za misiba kujinufaisha kwa kukodi magari kwa gharama hewa na
wengine kulipia majeneza kwa gharama hewa pia.
Wote hawa
kama alivyopata kusema Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere (marehemu) ni
‘mazi ga nyanza’, kwamba ni wale wale walio na fikra zinzofanana za kutumia maafa
kujinufaisha kimaisha. Watanzania tunapaswa kuwa na huruma, tunapaswa
kusaidiana, lakini pia kushukuru wanaotusaidia kupunguza machungu yanayotupata.
Inakuwa si
sawa watu kujinyima wakiamini wanachangia walengwa, lakini kumbe michango yao
inaingia mifuko haramu. Kama kweli kitendo kama hiki kitakuwa kimefanyika, basi
kitakuwa kimetokana na nguvu za shetani, ambacho hata Mungu atakiadhibu na tunaomba
ikithibitika kuwa dili hilo lilifanyika basi sheria ifuate mkondo wake, ili
liwe onyo na funzo kwa wengine wenye nia ovu kama hiyo.
0 comments:
Post a Comment