WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amewasimamisha kazi maofisa misitu wanne na kusimamisha shughuli za uvunaji mazao ya misitu wilayani Rufiji kwa muda usiojulikana, baada ya kutoridhishwa na usimamizi wake.
Maofisa
waliosimamishwa kazi ni pamoja na Mkuu wa Idara ya Ardhi, Maliasili na
Mazingira, Dk Paul Ligonja, Ofisa Misitu wa Wilaya, Gaudens Tarimo, Ofisa
Misitu Yonas Nyambuya na Ofisa Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) wa Wilaya,
Seleman Bulenga.
Waziri Mkuu
alifikia uamuzi huo jana wakati akizungumza na watumishi wa wilaya kwenye
ukumbi wa halmashauri kabla ya kuzungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara
katika viwanja vya jumba la maendeleo.
Aidha,
Waziri Mkuu alimwagiza Mkuu wa Wilaya, Juma Njwayo kukusanya magogo yote
msituni na kuyapiga mnada na kuitaka Wizara ya Maliasili na Utalii, kwenda
Rufiji kuchunguza leseni za uvunaji walizotoa kwa wilaya hiyo.
Waziri Mkuu
alibainisha kwamba wilaya hiyo ni moja ya wilaya zinazoongoza kwa uvunaji mazao
ya misitu bila ya kufuata taratibu licha ya kuwa na maofisa misitu.
“Hakuna
mafanikio katika sekta ya misitu kwenye wilaya hii. Nasimamisha shughuli zote
za uvunaji mazao ya misitu na watendaji wake kwa sababu hatuwezi kuacha watu
wanakata magogo bila kufuata taratibu.
“Haiwezekani
Rufiji iwe ‘shamba la bibi’, nimesimamisha uvunaji wa magogo hata kwa wenye leseni,
hadi tuzichunguze zimetoka wapi. Hatuwezi kuruhusu maofisa wanashiriki vitendo
vya hujuma kwa kuvuna misitu Rufiji na kugonga mihuri ya Kilwa, kisha fedha
wanatia mifukoni,” alisema.
Wakati huo
huo, Waziri Mkuu amemwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya, Rashid Salum
kufuatilia maagizo aliyotoa kuhusu kizuizi cha Ikwiriri kwa Waziri wa Maliasili
na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe alipokutana na watumishi wa wizara hiyo.
Julai 18
Waziri Mkuu alikutana na watumishi wa wizara hiyo Dar es Salaam na kusisitiza,
kwamba hakuna sababu ya Serikali kuendelea kuwa na watumishi wasio na uaminifu,
uadilifu na uwajibikaji.
Waziri Mkuu
aliitaka wizara hiyo kupunguza vizuizi vya ukaguzi wa mazao ya misitu
barabarani, baada ya kukosa tija, alitolea mfano wa barabara ya mikoa ya Kusini
kuanzia Dar es Salaam yenye vizuizi visivyopungua sita na kila kizuizi
kikitumika kukagua mazao ya misitu na maliasili.
Awali,
Mbunge wa Rufiji, Mohammed Mchengelwa alilalamikia vitendo vya dharau
vinavyofanywa na watumishi katika wilaya hiyo, jambo linalosababisha wananchi
kukosa imani na Serikali yao.
0 comments:
Post a Comment