WASOMI wa fani ya uchumi nchini, wametaja mambo yaliyochangia
fedha kupotea kwenye mzunguko, tofauti na kauli ya Rais John Magufuli, kuwa
huenda kuna watu wamezificha majumbani.
Huku wakitaka utafiti ufanyike kuhusu hali hiyo, wasomi hao
wamesema hali hiyo pia imechangiwa na hatua zilizochukuliwa na Serikali ya
Awamu ya Tano, kudhibiti matumizi mabaya ya fedha za umma.
Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu jana, Mhadhiri wa Chuo
cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Profesa Humphrey Moshi alisema kutokana na
hatua hizo, watu wako makini kwenye matumizi, kwa sababu fedha zinapatikana
kwa wanaofanya kazi tu na ndiyo maana hazionekani mitaani.
“Watu wamekuwa makini katika utoaji na utumiaji wa fedha zao, mtu
hawezi kutoa fedha tu wakati hazalishi, zamani kabla ya kuingia Rais John
Magufuli, fedha zilikuwa zinazagaa kwa kuwa kulikuwa na mianya mingi ya
kupiga ‘dili’,’’ alisema.
Alitaja mambo yanayosababisha kupotea kwa fedha mtaani, kuwa ni
pamoja na kusitishwa kwa safari za nje kwa watumishi wa umma, ambazo kwa
mujibu wa Profesa Moshi, safari hizo zilikuwa zikiwapa watu fedha za ziada.
Alitaja hatua ya Serikali kukabiliana na watumishi hewa waliogundulika,
kwamba kabla ya hapo tatizo hilo lilisababisha watu kupata fedha kwa njia
zisizo halali na kuzitumia hovyo mitaani.
“Pia kuna wafanyabiashara waliokuwa wakiingiza bidhaa bila kulipia
kodi, nao walikuwa wanatumia fedha vibaya ndiyo maana zilikuwa zinazagaa tu na
watu wanafanya starehe,’’ alisema.
Profesa Moshi alisema baada ya hatua hizo za Serikali ambazo zinaendelea,
kwa sasa ili mtu apate fedha, ni lazima afanye kazi na kinachotakiwa si
wananchi kulalamika, bali kujitahidi kutafuta njia za kujiingiza kipato.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Profesa Honest Ngowi alisema
hata kudorora wa shughuli za uchumi na kodi kubwa, vinaweza kupunguza fedha
mifukoni, hivyo ni vyema kufanyie utafiti utakaosaidia kutoa majibu mazuri.
Kwa mujibu wa Profesa Ngowi, hata riba kubwa ya kukopa benki
inaweza kupunguza fedha mitaani kwa kuwa zina tabia ya kukatisha tamaa wakopaji.
Alisema riba ya kuweka fedha benki nayo ikiwa kubwa, huvutia watu
kuweka fedha benki badala ya kuziacha kwenye mzunguko, lakini hata sera za
kifedha za kupunguza fedha kwenye mzunguko kwa sababu mbalimbali kama vile
kupunguza mfumuko wa bei, nazo huchangia kupunguza fedha.
0 comments:
Post a Comment