Profesa Ibrahim Lipumba |
Profesa Lipumba ambaye pia ni mchumi, aliitoa kauli hiyo
jana wakati akizungumza kwenye kipindi cha Joto la Asubuhi kupitia kituo cha
Clouds FM ambapo pia alisema mapendekezo ya awali yalikuwa ni kila chama kitoe
mgombea urais lakini Maalim Seif Sharif Hamad alikiuka na kutaka Chadema pekee
ndiyo itoe mgombea.
Swali: Ni kitu gani kilikuaminisha kuwa mtu anayefaa
kugombea ndani ya Ukawa ni Jaji Warioba?
Lipumba: Nilipata fikra kuwa kwa sababu wanahitaji
kutekeleza mambo ambayo Jaji Warioba amekuwa akiyasimamia na kuyaweka ndani ya
Rasimu ya Katiba, ikiwamo ripoti ya kupambana na ufisadi ya mwaka 1996 wakati
wa awamu ya Rais Benjamin Mkapa, na kwa kuwa ni mwadilifu, angeweza.
Baada ya kuona kuwa Jaji Warioba anafaa nilimfuata na kumwomba
asimame kwa upande wa Ukawa kama mgombea urais, lakini alinigomea na kunieleza
kuwa ameshastaafu siasa tangu mwaka 2002 hivyo hawezi kugombea.
Nilipoona mtu niliyekuwa namtarajia ambaye ni Jaji Warioba
alinijibu kuwa amestaafu siasa na bado mwana CCM, aliniambia anakubali mambo
ambayo tumefanya pamoja hasa kwenye uandaji wa Rasimu ya Katiba mpya, lakini
suala la kujiunga na Ukawa kwake halikuwapo.
Baada ya kunijibu hivyo nilimweleza kuwa kutokana na
kukataa kwake kunanifanya niamini kuwa yeye ndiye mtu sahihi zaidi, maana
hakuwa tayari kukubali kirahisi lakini msimamo wake ukabaki kuwa haitawezekana.
Nilikuwa nafikiri kuwa ikiwa tunakwenda kutafuta mtu nje
ya Ukawa na anayeweza kuwa na msimamo mzuri kwa misingi ya kuanzishwa Ukawa ya
kuunga mkono Katiba ya Wananchi basi alikuwa Jaji Warioba.
Kama kuna watu ambao ndani ya CCM wangeweza kuchukuliwa
kuwa wagombea wa urais kwenye Ukawa kwa misingi ya kuanzishwa kwake, mtu
aliyekuwa anawekwa kwenye fikra hizo ni yeye.
Swali: Ulitumwa na Ukawa kumfuata Jaji Warioba?
Jibu: Hakuna aliyenituma ila mimi binafsi niliamini Jaji
Warioba ndiye mtu sahihi kama tunataka mgombea kutoka nje ya Ukawa.
Swali: Uliposikia wanafanya mpango wa kumkaribisha
Lowassa ndani ya Ukawa. Je, ulitumia nafasi yako kabla ya kuandika barua?
Lipumba: Nilikutana na Lowassa peke yangu, maana nilielezwa
kuwa anataka kukutana nami. Akanieleza kuwa alifanya mazungumzo na wenzengu na
kuhoji kama nina habari.
Nilimjibu sina taarifa nasikia tu ambapo nilishauri ni
vema tuwe na kamati ya vyama vyote ili kujadili suala hilo kabla ya kulipatia
ufumbuzi.
Nilikutana na Lowassa na kuzungumza naye kuhusu suala
hilo kabla ya kwenda kukutana na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na
Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia.
Baada ya hapo niliwapa taarifa Mbowe na Mbatia kuwa
inabidi wakutane na Lowassa ili kujadili anayepaswa kugombea urais.
Ingawa Lowassa alikuwa na nafasi kubwa ya kupata uongozi
ndani ya Serikali, lakini sidhani kama angeweza kutimiza matakwa ya wananchi.
Swali: Kama uliona Lowasa hawezi kutimiza matakwa ya
wananchi, uliwashauri nini Ukawa?
Lipumba: Niliwashauri walipo wangeweza kutazama mtu
anayeweza kuendana na mahitaji yao na mimi nikiwa ndani ya Ukawa kabla ya
kupata mgombea urais.
Tungeweza kupata ushindi kupitia kwa Lowassa lakini hata
ukipatikana ushindi tungekwenda kusimamia mambo gani na katika eneo lipi?
Suala lililopo katika siasa ni kuwa ukishachaguliwa
unatakiwa uunde Serikali ili usimamie misingi fulani ambayo itakidhi mahitaji
ya wananchi .
0 comments:
Post a Comment