VIONGOZI wa vyama vya siasa nchini wametakiwa kuiga kwa vitendo uzalendo na moyo wa kujitoa aliokuwa nao Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere enzi za uhai wake ili kuliwezesha Taifa kupiga hatua kimaendeleo.
Mkurugenzi
wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Kailima Ramadhani (pichani) alitoa kauli hiyo jana
baada kutembelea kaburi na Makumbusho ya Baba wa Taifa eneo la Mwitongo
wilayani Butiama.
Alisema
kumbukumbu za Baba wa Taifa zilizohifadhiwa vizuri katika makumbusho hiyo zina
mambo mengi ya kujifunza ambayo wanasiasa wanatakiwa kuyafanya kwa vitendo hasa
uzalendo kwa nchi, uvumilivu, upendo na moyo wa kujitoa kwa dhati kuwatumikia
wananchi.
“Kupitia
kumbukumbu hizi sisi watumishi wa NEC tumejifunza ukomavu wa demokrasia
aliokuwa nao Mwalimu Nyerere akiwa ndani na nje ya Bara la Afrika, wengi
wanadhani demokrasia ni wakati wa uchaguzi tu, kumbe demokrasia ni pamoja na
kuheshimu watu wengine,” alisema Kailima.
Alieleza
kwamba maisha aliyoishi Baba wa Taifa ni mfano wa kuigwa na viongozi na
watanzania wote hasa pale alipojitofautisha na viongozi wengi wa Bara la Afrika
alipoepuka tamaa ya madaraka na mali kwa manufaa ya taifa.
“Sote ni
mashahidi kupitia kumbukumbu zake tumeona mahali alipokuwa anaishi mwalimu
kabla hajajengewa nyumba na Jeshi kama Rais mstaafu wengi walitegemea asingeishi
katika eneo lile, kumbukumbu hii nzuri aliyoiacha inatufundisha watanzania kuwa
mwalimu aliitanguliza Tanzania mbele kuliko maslahi yake binafsi,” alisisitiza.
Kailima alibainisha
kuwa NEC itaendelea kumuenzi Nyerere kwa aliyoyafanya na kuyasimamia kwa manufaa
ya taifa huku akitoa wito kwa viongozi wa vyama vya siasa wawe na kiasi na waridhike
na vile walivyonavyo.
“Suala la
kuridhika na kuwa na kiasi linapaswa kuzingatiwa, wanasiasa wanapaswa
kuwaheshimu wananchi wanaowachagua kupitia chaguzi mbalimbali, matokeo
yanapotoka kama ni sahihi basi wanasiasa wakubaliane na maamuzi yao,” alisema
Kailima.
Kwa upande
wake Mhifadhi wa Makumbusho ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere
Bw. Jacob Thomas alisema kuwa watanzania wanayo mengi ya kujifunza kupitia vitu
alivyoviacha Baba wa Taifa ambavyo vimehifadhiwa katika Makumbusho hiyo.
Alisema
kuwa maisha ya uadilifu aliyoishi enzi za uhai wake na mchango wake katika
kuiletea maendeleo Tanzania na Bara la Afrika vinapaswa kuenziwa kwa nguvu zote
na viongozi wa Tanzania.
“Ninyi
mliopata nafasi ya kuitembelea Makumbusho hii mmejifunza vitu vingi kumhusu
Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwamba alikuwa ni mtu wa namna gani kwa
viwango vya Afrika na dunia kutokana na kumbukumbu ya uadilifu aliyoiacha ndani
na nje ya mipaka ya Tanzania,” alisema.
0 comments:
Post a Comment