WAKATI vijana wengi nchini wakilalamikia Serikali kwa
kukosa ajira, baadhi ya watu wameibuka na kampuni hewa zinazotangaza nafasi za
kazi na kutapeli fedha na mali kwa wanaoomba kazi.
Mbali na kutapeliwa fedha, baadhi ya wanawake hujikuta wakilazimishwa
kutoa rushwa ya ngono kwa ahadi ya kupewa kazi na mishahara minono bila
mafanikio. Watu walioingia kwenye mtego huo wamejikuta wakitapeliwa kati ya Sh
10,000 na Sh 30,000.
Uchunguzi wa JAMBO LEO umebaini kuibuka na kuzagaa kwa kampuni
hizo mijini ambazo hubandika au kugawa matangazo barabarani na kwenye vituo vya
mabasi, mitaa inayopitwa na watu wengi, pia kusambaza vipeperushi kwa wapita na
sehemu zenye mikusanyiko mikubwa ya watu.
Uchunguzi umebaini kuwa baadhi yao hudiriki kutumia
vyombo vya habari na kulipia matangazo na nyingine mitandao ya kijamii. Kampuni
hizo huwataka wahusika kuwasiliana nao kwa kupiga namba za simu za mikononi na husisitiza
wanao ‘beep’ au kutuma ujumbe mfupi wa maneno hawajibiwi.
Kampuni ambazo zimetiliwa shaka na watu walioomba kazi na
kulazimika kutoa taarifa kwa vyombo vya habari ni Rifa Consultants Co. Ltd,
Human Capital, GHM Company Ltd.
Mmoja wa waomba kazi katika kampuni ya Rifa Consultants
Co. Ltd, Halima Mchau alisema baada ya kuomba kazi kama ilivyo kawaida,
alisubiri majibu na baada ya kujibiwa pamoja na mashariti mengine, alikutana na
ya kulipa Sh 16,500.
Mwomba kazi huyo alisema kutokana na masharti hayo,
aliingiwa wasiwasi kwani hajapata kukutana na mazingira hayo ya kuomba kazi na kutakiwa
kutoa fedha za usaili. Abraham Ntambara alisema aliomba kazi katika kampuni ya
Human Capital na kukutana na masharti ya kulipa Sh 12,000.
Katika barua za majibu kwenda kwa waomba kazi, kampuni
hizo zilijulisha waombaji kwamba wamechaguliwa kusailiwa na kuelekeza kuwa
wanapaswa kulipa fedha hizo siku mbili kabla ya usaili.
Baadhi ya kampuni hizo, zinaelezewa kutoa masharti nafuu kama
vile mwajiriwa kujua kusoma na kuandika Kiswahili, huku zikitolewa ahadi za
mshahara wa kati ya Sh 200,000 hadi Sh 600,000 kwa mwezi.
Mmoja wa watu waliowahi kushiriki mfumo huo wa utapeli,
alidai kuwa walikuwa wanakusanya hadi Sh milioni tatu kwa siku kutoka kwa
watafuta ajira.
Alibainisha kwamba walikuwa wakitumia namba za simu
zilizosajiliwa kwa majina ya bandia, ambazo huharibiwa baada ya kufanikisha
utapeli, ili kuepuka kukamatwa.
Alisema kinachofanyika ni kusambaza matangazo ya ajira na
kuweka namba hizo ili wahitaji waombe na kuingizwa kwenye utapeli bila kujua.
Miongoni mwa kazi zinazotangazwa wa wingi ni usimamizi wa
ofisi, usambazaji bidhaa, usafi, utunzaji stoo, usambazaji barua na uwekaji
kumbukumbu za majalada.
Wengine walioingizwa kwenye utapeli huo walidai kuwa
baadhi ya kampuni hujinadi kuwa za kimataifa, hivyo kuhitaji wanaojua
Kiingereza.
“Ninayo furaha kukutaarifu kuwa timu ya usaili imepokea,
kupitia na kujadili ombi lako na kufanya uamuzi wa kukuita kwenye usahili wa
ana kwa ana,” inasema sehemu ya barua
ya majibu.
Barua hiyo ilibainisha kuwa taasisi hiyo ni ya kimataifa
hivyo lugha ya mawasiliano ni Kiingereza na pia ndiyo lugha itakayotumika
kwenye mazingira ya kazi.
Pia barua iliendelea kusema, kuwa watu wote ambao
wamechaguliwa wanashauriwa kuandaa kila kitu kwa Kiingereza na si lugha
nyingine yoyote.
“Hatutakubaliana na jambo lolote ambalo litakuwa kwa Kiswahili
kabla ya usaili, uzingatie agizo la mteja wako,” alisema.
Aidha, katika kuhakikisha kuwa kampuni hizo zinaonesha
uhalali wao, zimekuwa zikitaja kuwa na matawi katika miji mbalimbali. Kampuni
ya Rifa ilieleza kuwa ofisi zake ziko Dar es Salaam, mtaa wa Ohio, karibu na benki
ya Barclays.
Pia ilisema ipo katika eneo la Afrika Mashariki ambako
wanafanya shughuli mbalimbali. Taarifa hizo zilionesha fedha hizo ambazo
wanatakiwa kutoa kuwa zitasaidia waomba kazi kupewa chai, ada ya mahojiano na
malipo ya wahoji wanaotoka nje ya mkoa husika.
Hali kadhalika wasailiwa walipaswa kulipa fedha hizo
kupitia mtandao wa simu namba +255 783749091 kabla ya jana saa moja usiku kwa
kampuni ya Rifa.
Maeneo ambayo yametajwa kwa ajili ya usaili ni Karena
Hotel ya Shinyanga ambako unafanyika leo na wahusika walitakiwa kuwasiliana kwa
namba +255 686479958 kwa maelezo zaidi.
Dar es Salaam usahili utakuwa kesho na mawasiliano
yafanywe kwa namba +255 686479958 kwa maelezo zaidi, Morogoro namba +255
686479958, Meatu Hotel Singida namba +255 686479958, Tanga namba +255 686479958
na Arusha namba +255 686479958.
Maeneo mengine ni Mbeya namba +255 686479958, Mwanza
Ngasamo Hotel namba +255 686479958, Pwani namba +255 686479958 na Mtwara namba
+255 686479958. Barua hiyo imeandikwa na Abubakari Gondwe ambaye
anajitambulisha kama Mkuu wa Idara ya Ajira wa kampuni hiyo.
0 comments:
Post a Comment