Seif aitisha kikao kujadili barua ya Jaji Mutungi


Suleiman Msuya


KAMATI ya Utendaji ya CUF inayoongozwa na Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad (pichani) imeitisha kikao cha Baraza Kuu la Uongozi kesho kujadili Ushauri wa Msajili wa vyama vya siasa na kumwita Profesa Ibrahim Lipumba akajieleze Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Nassor Mazrui alisema hayo jijini Dar es Salaam jana baada ya kamati hiyo kukutana kwa dharura.

Aidha alisema Kamati ya Utendaji ya CUF, imekataa maoni na ushauri uliotolewa na Msajili wa Vyama vya Siasa nchini Jaji Francis Mutungi kutaka Profesa Lipumba arejee katika nafasi hiyo.

“Tumeitisha kikao hicho kwa mujibu wa ibara ya 85(5) na ibara ya 108 ya Katiba ya CUF ya mwaka 1992 toleo la mwaka 2014 na kwamba ajenda kuu itakuwa kumjadili Profesa Lipumba, atapewa nafasi aseme kwa nini baraza lisimchukulie hatua za kinidhamu kwa matendo yake aliyoyafanya juzi,” alisema Mazrui.

Alisema kwa mujibu wa Katiba ya CUF ya mwaka 1992 Profesa Lipumba atafika mbele ya Baraza Kuu la Uongozi Taifa akitakiwa kujieleza na kujitetea ambapo chama kitatafakari na kuamua.

Kwa mujibu wa Mazrui Katiba ya CUF inazungumzia jukumu la mwanachama kulinda heshima ya chama kwa kuwa na tabia njema, kutekeleza masharti ya katiba, kutii kanuni, kutii sheria na sheria ndogondogo za serikali iliyoundwa kihalali.

“Kuwa mwaminifu kwa chama na Serikali zilizoundwa kihalali na kwa ridhaa ya wananchi na kuwa tayari kuwatumikia watu kwa juhudi, maarifa na vipaji vyake vyote,” Ibara 12(7)

“Kukilinda kutokana na maadui wa ndani au wa nje wanaokusudia kukihujumu, kukiua, kukigawa au kukidhoofisha.” Ibara 12(16) Kuhusu kukataa maoni ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Mazrui alisema kamati ya utendaji ilikutana katika kikao cha dharura kilichofanyika Ofisi za CUF Makao Makuu ya Zanzibar na kujadili taarifa hiyo ya msajili pamoja na kitendo cha Lipumba kuvamia ofisi kuu ya chama Dar es Salaam.

“Kamati ya utendaji Taifa imejadili taarifa kuhusiana kundi lake la wahuni na kusababisha uharibifu wa mali za chama kutokana na matukio hayo kamati ya utendaji ya Taifa imefikia maamuzi makuu mawili,” alisema.

Mazrui alisema kamati ya utendaji ya Taifa inakataa na kupinga kwa hoja thabiti ushauri na maoni yaliyopendekezwa na Msajili na badala yake inaendelea kusimamia uamuzi wa Mkutano Mkuu Maalum wa Taifa wa Agosti 21 mwaka huu uliokubali kujiuzulu kwa Lipumba kama mwenyekiti.

Aidha alisema kamati hiyo inaendelea na msimamo wake wa kikao cha Baraza Kuu la Uongozi Taifa yaliyofikiwa katika kikao chake cha Agosti 28 mwaka huu juu ya kuwasimamisha uanachama Lipumba, Magdalena Sakaya, Maftaha Nachuma, Abdul Kambaya, Masoudi Mhina, Thomas Malima, Ashura Mustafa, Kapasha H. Kapasha, Musa Haji Kombo, Habibu Mnyaa, Haroub Shamis na kumfukuza uanachama Shashu Lugeye.

Naibu Katibu alisema Katiba ya chama haina kifungu chochote kinachompa mamlaka Msajili wa Vyama vya Siasa kupokea rufaa kuhusiana na uamuzi wa vikao vya chama na kubatilisha maamuzi ya vikao hivyo.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo