Viongozi wa EAC |
Uamuzi huo ulifikiwa jana Ikulu Dar es Salaam na viongozi
wa Jumuiya hiyo baada ya kikao cha 17 kilichodumu kwa takribani saa sita.
Akizungumza baada ya kikao hicho, Mwenyekiti wa EAC, Rais
John Magufuli alisema kikao hicho kilikuwa na ajenda nne, ila ya EPA ilikuwa
ngumu kulingana na uzito wake.
Alitaja ajenda hizo kuwa ni ripoti ya mgogoro wa Burundi,
kuingizwa rasmi kwa Sudan Kusini kweney Jumuiya, kupitishwa kwa Naibu Katibu
Mkuu wa EAC na EPA.
Rais Magufuli alisema viongozi wote kwa pamoja walikubaliana
kupewa muda wa miezi mitatu ili Sekretarieti ya EAC iangalie na kupitia
masharti ya EPA kabla ya kusaini ili kila mmoja afaidike.
Hata hivyo nchi ambazo zilishasaini makubaliano hayo
kutoka Jumuiya hiyo ni Rwanda na Kenya.
Alisema katika kikao hicho, walibaini mambo 10 ambayo
yanapaswa kuangaliwa kabla ya kufikia uamuzi kwa maslahi ya nchi na wananchi.
Mwenyekiti alitaja mambo ya kuangaliwa kuwa ni kwa namna
gani nchi za EAC zitafaidika, njia gani itatumika kuzuia bidhaa za kilimo na
kulinda wakulima.
Maeneo mengine ni usawa, makusanyo yatokanayo na bidhaa
zitakazoingizwa, Burundi itasainije huku ikiwa imewekewa vikwazo na EU, kujitoa
kwa Uingereza EU na athari zake, kukosekana kipengele cha kuruhusu nchi zingine
kujihusisha na nchi za EAC kibiashara, kukosekana ushuru wa forodha na
kipengele cha nchi kujitoa pale inapoona haijaridhika na mkataba.
Rais Magufuli alisema mkataba huo ukisainiwa kwa wakati
huu, nchi wanachama zinaweza kuingia kwenye mtego mbaya.
“Tumejadiliana kwa muda mrefu ila mjadala mkubwa ulikuwa
suala la EPA ambapo tumekubaliana tupewe miezi mitatu ili tukutane Januari na
kutoa uamuzi wa pamoja,” alisema Magufuli.
Alisema Tanzania iko kwenye mkakati wa kujenga viwanda,
hivyo ni lazima iwe makini katika kusaini mkataba huo.
Aidha, aliiomba EU kutoiadhibu Kenya kutokana na uamuzi
huo kwani nia yao ni nzuri hivyo wapewe nafasi.
Mwenyekiti huyo alisema viongozi wote walikubaliana
kuiidhinisha Sudani Kusini kuwa mwanachama wa EAC na Christopher Bazivamo
kutoka Rwanda kuwa Naibu Katibu Mkuu Mpya na mapendekezo ya kutatua mgogoro wa
Burundi.
0 comments:
Post a Comment