Halima Mdee |
Msimamo wa wabunge hao uliibua mvutano kati yao na Waziri
wa Katiba na Sheria, Dk Harrison Mwakyembe, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG),
George Masaju na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Dk Abdallah Possi.
Muswada huo wenye vifungu 24, ulifanyiwa marekebisho katika
vifungu zaidi ya 15 yakiwamo marekebisho ya Serikali huku Mwenyekiti wa Bunge,
Andrew Chenge akitengua kanuni za chombo hicho cha kutunga sharia, kilipokaa
kama kamati juzi jioni, ili kikao kiendelee na hadi Muswada huo utakapopitishwa
kifungu kwa kifungu.
Wabunge waliokuwa wakizungumza kwa kupokezana kusimama
bungeni mithili ya watu waliokuwa wamepanga jambo hilo tangu awali, ni Profesa
Anna Tibaijuka (Muleba Kusini), Halima Mdee (Kawe) na Mbunge wa Viti Maalumu,
Susan Lyimo (Chadema).
Kabla ya kupitishwa kwa Muswada huo, Dk Mwakyembe alijibu
hoja za wabunge walizotoa wakati wa mjadala na kubainisha kuwa haukusudii
kudhibiti vyombo vya habari, bali kuviongeza wigo wa upatikanaji wa taarifa,
huku akiwashukia wabunge wa upinzani na kuwapiga kijembe kwa uamuzi wa Chadema
kumpokea Edward Lowassa na kumpitisha kuwa mgombea urais katika uchaguzi
uliopita.
Licha ya juhudi za wabunge hao kutaka mabadiliko ya
vifungu hivyo, baadhi ya mapendekezo yao yalipanguliwa na Masaju na mawaziri hao
na kuwezesha vifungu hivyo kupita kama vilivyo.
Katika kifungu cha pili, Profesa Tibaijuka alitaka
kibadilishwe ili kulinda watu kutumia mamlaka vibaya, kusumbua taasisi binafsi
kudai taarifa kwa madai ya kuwa na maslahi ya umma.
Licha ya Mbunge huyo kutaka hoja hiyo ijadiliwe na
wabunge wengine, Mwenyekiti Chenge ambaye alikuwa akiingilia kati pale
malumbano kati ya wabunge na mawaziri hao yalipokuwa makali, alipangua hoja
hiyo.
Tibaijuka aliibuka tena wakati wa kupitisha kifungu cha
tatu, lakini aliondoa hoja yake kwa kuwa ya kifungu cha pili ilikataliwa, huku
Lyimo akiibuka katika kifungu cha tatu akitaka utolewe ufafanuzi wa neno mtu wa
tatu jambo ambalo lilipingwa na Masaju na Possi.
Mdee pia alitaka marekebisho katika kifungu hicho kwa maelezo
kuwa lazima sheria imtaje mtu wa tatu ni nani, jambo ambalo Dk Mwakyembe
alilijibu na kufafanua kuwa suala hilo likiibua ukakasi, litabadilishwa.
Vifungu vingine vilivyopingwa na wabunge hao wakitaka
marekebisho ni kifungu cha nne, sita, tisa, 12,13, 15,18, 20, 22 na 23.
Kwa upande wa Serikali ilifanya marekebisho yakiwamo ya
kuondoa makosa katika Sheria ya Usalama wa Taifa ya mwaka 1970 ambayo
yaliingizwa kwenye Muswada huo.
Awali ilipendekezwa adhabu ya kifungo jela kati ya miaka
15 hadi 20 kwa mtu atakayebainika kutenda makosa kuhusu na kukiuka maslahi ya
Taifa.
0 comments:
Post a Comment