RAIS John Magufuli ameibua mambo matatu makubwa, likiwamo la kuagiza mazungumzo ya kurekebisha mkataba wa Kampuni ya Kimataifa ya Kuhudumia Shehena ya Kontena Bandarini (TICTS), ili uwe na tija kwa Taifa.
Hatua hiyo
ya Rais imekuja miezi mitano baada ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali(CAG),
Profesa Juma Assad, kubaini Aprili kwamba kampuni hiyo imevunja mkataba na
Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA).
Kampuni
hiyo inadaiwa kubadili umiliki wa asilimia 51 za hisa kutoka kampuni ya Ictis zilizoko
Titcs kwenda Hutchison International Port Limited (HPH) na kuikosesha mapato
TPA.
Titcs
iliingia mkataba na TPA mwaka 2000 wa upangishwaji eneo la kontena la TPA
Kurasini Dar es Salaam, lakini ripoti ya CAG ilibainisha kuwa siku 20 baada ya mkataba
huo wa miaka 10 kusainiwa, hisa hizo zilihamishiwa HPH.
Katika
ziara ya Rais Magufuli bandarini Dar es Salaam jana, ambayo waandishi wa habari
walizuiwa bila maelezo ya kina, tofauti na kuambiwa ni mkutano wa ndani kati
yake na wafanyakazi wa TPA, Rais alikutana na wafanyakazi hao huku wafanyakazi
wasiokuwa na vitambulisho licha ya kuvaa vizibao vya TPA wakikataliwa kuingia ndani
na kurudi ofisini kuendelea na majukumu yao.
Mbali na
kuuzungumzia mkataba wa Ticts, pia aliiagiza TPA kununua mashine nne za
kukagulia mizigo bandarini hapo na mita za kupimia mafuta.
Kuhusu
kampuni hiyo, Rais alisema TPA inapaswa kushirikiana na Wizara ya Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano ili kurekebisha mkataba huo. Magufuli alisema mkataba wa
Ticts na Serikali ulilenga kunufaisha pande zote, hivyo ni vema ukaangaliwa
upya ili kutoa manufaa stahiki.
Ticts
inafanya kazi ya kupakua mizigo kwenye magati namba nane hadi 11 ambapo kwa
muda mrefu mkataba wake umekuwa ukilalamikiwa bila ufumbuzi.
Kuhusu
mashine, Rais aliipa TPA miezi miwili kununua nne ambazo zitasaidia kudhibiti
uhakika wa mizigo ambapo kwa sasa kuna udanganyifu.
Pia alitoa
agizo hilo baada ya kubaini kuwa kati ya mashine nne za ukaguzi wa mizigo
zilizopo, ni mbili tu ndizo zinafanya kazi na hazina uwezo wa kukagua mizigo yote
inayotoka na kuingia nchini kupitia Bandari hiyo.
“Kwa hiyo
nawaagiza TPA, na Waziri (Profesa Makame Mbarawa) na TRA (Mamlaka ya Mapato
Tanzania) mpo hapa hakikisheni mnanunua mashine nne za kukagulia mizigo ndani
ya miezi miwili, na ikifika miezi mitano muwe mmenunua sita, ni lazima mizigo
yote ikaguliwe kwa mashine,” aliagiza Rais Magufuli.
Aidha, Rais
Magufuli aliiagiza TPA kuhakikisha kuwa inanunua mita za kupimia mafuta
yanayopakuliwa kwenye meli, hiyo ikiwa ni baada ya kubaini kuwa mita zilizopo hazifanyi
kazi.
“Naagiza
tena TPA kuharakisha mchakato wa kununua mita mpya na kuzifunga eneo hilo ili
kudhibiti ukusanyaji wa mapato ya kodi ya mafuta,” alisema.
Dk Magufuli
aliitaka TPA kujipanga kujenga bandari kavu (ICD) Ruvu, Pwani na kuachana na
bandari kavu zilizoanzishwa na watu binafsi Dar es Salaam ambazo zimekuwa
zikitumika kukwepa kodi.
Akizungumza
na wafanyakazi baada ya kumaliza kutembelea bandari, Rais aliwatoa shaka na
wafanyakazi wengine serikalini, kuwa uhakiki wa vyeti unaoendelea nchi nzima
hauna lengo la kuwafukuza kazi.
Alisema
unafanyika ili kukabiliana na tatizo la wafanyakazi hewa ambao sasa wamefikia
17,500 na pia kuondoa wafanyakazi wanaotumia vyeti bandia.
Wakati
huo huo, Rais Magufuli
amemwapisha Dk Zainab Chaula kuwa Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Tawala za
Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi). Dk Chaula amejaza nafasi iliyoachwa wazi
na Dk Deodatus Mtesiwa ambaye amestaafu. Kabla ya kuteuliwa Dk. Chaula alikuwa
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, Dodoma.
0 comments:
Post a Comment