Fidelis Butahe
MWEZI mmoja baada ya Chadema kusitisha Operesheni Ukuta kupinga
inachokiita ukiukwaji wa haki za binadamu na ukandamizaji wa demokrasia, leo
inatarajia kutoa mwelekeo wa mkakati huo.
Operesheni hiyo ilipangwa kuzinduliwa Septemba mosi nchini kwa
maandamano na mikutano ya hadhara kama maazimio ya Kamati Kuu ya Chadema, baada
ya chama hicho kukumbwa na vikwazo kadhaa kuendesha shughuli zake, ikiwa ni
pamoja na kuzuiwa kufanya mikutano ya hadhara.
Siku moja kabla ya kufanyika kwa operesheni hiyo, Mwenyekiti wa
Chadema, Freeman Mbowe alitangaza kuisitisha kwa mwezi hadi kesho, ili kutoa
fursa kwa viongozi wa dini kusemezana na Rais John Magufuli na Serikali yake.
Akizungumza na JAMBO LEO jana, Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu
Lissu alisema: “Kuhusu Ukuta, kesho (leo) tutatoa msimamo wetu juu ya kitu
tutakachofanya.”
Alisema operesheni hiyo ilisitishwa kutokana na sababu za msingi
zilizoelezwa, hivyo kauli ya chama hicho leo itafafanua kwa kina kuhusu mambo
yote yaliyojitokeza katika kipindi hicho cha mwezi.
Wakati Lissu akieleza hayo, hadi jana hakukuwa na taarifa zozote za
kufanyika kwa kikao kati ya viongozi wa dini na Serikali.
Viongozi hao waliitaka Serikali na Chadema kufikiria amani ya nchi
na kutafuta njia mwafaka za kumaliza msuguano wa kisiasa hasa baada ya chama
hicho kushikilia msimamo wake wa kufanya mikutano na maandamano.
Wakati Chadema wakijipanga kutoa tamko lao, Mkuu wa Mkoa wa Dar es
Salaam, Paul Makonda jana alisisitiza kuwa Oktoba mosi ni Siku ya Kupanda Miti
jijini humo ambapo viongozi mbalimbali watahudhuria.
0 comments:
Post a Comment