Mawazo Lusonzo |
Ukiuzungumzia
muziki wa dansi katika nchi za kusini mwa Jangwa la Sahara, una rekodi na
kumbukumbu kubwa za aina ya bendi ambazo zilikuwamo katika orodha, lakini
zikafutika katika ramani ya dunia.
Tunapouzungumzia
muziki wa dansi leo, hatuwezi kukamilisha historia na kumbukumbu sahihi bila kuzitaja
baadhi ya bendi zilizoingia katika orodha ya bendi kongwe zilizokuwa sehemu ya
uasisi wa miondoko mbalimbali ndani na nje ya bara la Afrika.
Jamhuri
ya Watu wa Congo, DRC (Zaire ya zamani) inatajwa kama ndiyo chimbuko la bendi
nyingi zilizoutangaza muziki wa aina ya rhumba na dansi la mirindimo ya kasi ya
rhumba na hatimaye ‘Kavasha’ na Soukous, ambalo ndilo dansi lenyewe.
Ujio wa
muziki wa dansi lililochangamka ulianzia mwanzoni mwa miaka ya 50 hadi 70 baada
ya kuingia kwa teknolojia ya magitaa ya moto na ala za upepo, ambapo bendi
chache zilizoanzishwa katika nchi za kusini mwa Jangwa la Sahara zililitangaza
bara la Afrika hadi ndani ya mabara mengi duniani.
Ni
katika miaka hiyo, bendi kubwa zilianzishwa, lakini zilizoteka nyoyo na
ushabiki mkubwa nyingi ni zile za kutoka DRC, ambazo nyingi zilianzishwa
mwishoni na mwaka 1950 na ndani ya miaka ya ilianzia 1960 na kuendelea.
TP OK
Jazz iliyoasisiwa mwaka 1956 ilipata mafanikio makubwa na kuutalawa muziki wa
rhumba la ndani na nje ya DRC hadi miaka ya 80 na ndiyo inayotajwa kama chimbuko
la bendi nyingi zilizopiga muziki wa dansi la kizazi cha dansi la hivi sasa.
Lakini,
jambo linaloweza kuwa ndiyo msingi wa hoja ya leo ni kwamba, pamoja na TP OK
Jazz kuwa mwasisi wa bendi nyingi za kizazi cha baadae, lakini ilikosa jambo
moja la msingi, nalo ni hili la kutoweka duniani kwa kifo cha kimya kimya hadi
sasa.
Kutoweka
kwa bendi hiyo iliyokuwa chini ya Luambo Lwanzo Makiadi, maarufu kama Franco ilizimika
rasmi mwaka 1993 kulikochangiwa na kifo cha mwasisi huyo (Franco) na hadi sasa
hakuna bendi inayoitwa kwa jina hilo, zaidi ya wanamuziki waliowahi kuitumikia kuendelea
na muziki kivyaovyao.
Zaiko
Langa langa iliyoasisiwa mwaka 1969 ndiyo bendi pekee ya kizazi cha miaka ya 60
ambayo bado ipo hai ikiendeleza muziki wa wa dansi la kizazi hiki, huku ikiwa inaendeleza
mirindimo ya kisasa na ile ya kizamani.
Zaiko
iliyoanzishwa ikiwa na jina la ‘Bel Guide National’ iliasisiwa na wanamuziki
wengi vijana ambao wengi wao walikuwa ni wanafunzi wa shule za masomo ya juu ya
jiji la Kinshasa, ambayo ndiyo Langa Langa ya sasa.
Ikiwa chini
ya uongozi wa mwanamuziki mkongwe, Nyoka Longo, Zaiko inaingia katika rekodi
ambayo wengi hawaifahamu. Nayo ni hii ya kuwa ni bendi iliyoanzishwa miaka ya
60 lakini bado ipo hai hadi leo hii.
Bendi
ya muziki ya Msondo Ngoma ya sasa ya nchini Tanzania ndiyo inayoingia katika
rekodi hii ya kihistoria inayofanana na Zaiko Langa Langa. Zinafanana katika
matukio yanayozifanya ziwe hai, japo zimepitia katika majina tofauti!
Kwa faida
ya wadau wa muziki wa dansi wa kizazi hiki wanapaswa kuitambua Msondo Ngoma
kama ndiyo iliyokuwa ikiitwa NUTA Jazz, ambayo pamoja na kubadilika badilika,
lakini historia inabakia kuwa ndiyo bendi kongwe zaidi nchini, ambayo hadi sasa
bado ipo hai!
Ikiwa
na jina la NUTA Jazz, bendi hiyo ilianzishwa mwaka 1964 ikiwa chini ya Chama cha
Wafanyakazi wa iliyokuwa Tanganyika ambapo, katika vipindi tofauti imekuwa ikibadilisha
jina kadri chama hicho cha wafanyakazi kilivyokuwa kikibadilika!
Hadi
ilipokuja kuitwa ‘Msondo Ngoma’, bendi hiyo iliwahi kuitwa JUWATA na OTTU Jazz,
hadi pale mfumo wa uendeshaji ulipobadilika kwa wanamuziki wenyewe kukabidhiwa umiliki
huu wa sasa.
Nimewahi
kuzungumza na baadhi ya wadau wa bendi hiyo nikiwa na swali kama wanatambua
historia na rekodi hii muhimu iliyopo nyuma ya pazia? Jibu limenipa faraja iliyonifanya
niandike makala haya.
Shaaban
Dede, ambaye kwa sasa ndiye kiongozi wa bendi ya Msondo Ngoma alizungumzia
suala la kuitambua historia ya rekodi hii na kusema, ni hatua inayofanya
wajipongeze kwani ndiyo bendi kongwe iliyoanzishwa mwaka 1964 na kubakia kuwa
hai hadi sasa.
Abdulfareed
Hussein, huyu ni mmoja wa kundi la ‘Maseneta’ wa bendi hiyo ambaye alikiri
kuitambua kwa kuienzi rekodi hii kwa kuasisi siku maalum katika kila mwezi
inayojulikana kama ‘Msondo Ngoma Family Day’, ambayo itafanyika Septemba 30
katika ukumbi wa Mango Garden, Kinondoni, jijini Dar es Salaam.
Kwa
namna yoyote, hoja hapa ni historia iliyo nyuma ya pazia ya bendi ya Msondo
Ngoma na uhai wa bendi hiyo iliyoasisiwa mwaka 1964 lakini bado ipo hai kama
ilivyo kwa Zaiko Langa Langa ya DRC. Kazi kwao wana familia ya Msondo Ngoma kuienzi
historia hii na kuiendeleza hadi vizazi vijavyo.
Maoni:
0782 151 409
0 comments:
Post a Comment