MTU aliyekuwa akihubiri Neno la Mungu kwenye mabasi ya abiria aliyejulikana kwa jina la Makoye Shigela (56) amefariki dunia baada ya kuanguka ndani ya basi alimokuwa akihubiri.
Tukio hilo lililoshitua abiria
lilitokea mwishoni mwa wiki, baada ya mtumishi huyo wa Mungu anayetajwa kutoka
Kanisa la Mashahidi wa Yehova, kupanda basi la Kampuni ya Nyehunge linalofanya
safari zake kati ya mikoa ya Mwanza na Morogoro.
Alianguka na kufariki dunia wakati
akikusanya sadaka kutoka kwa abiria waliokuwa wakisafiri kwa basi hilo, huku mwandishi
wa habari hii akishuhudia tukio hilo.
Marehemu alipanda basi hilo maeneo
ya Buhungumalwa akielekea mkoani Shinyanga na alipomaliza kutoa Neno la Mungu
na kuhubiri, alianza kuomba sadaka kwa abiria na kuzikusanya. Ghafla alianguka
na kupoteza fahamu.
Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo
alieleza kuwa marehemu alikuwa akijihusisha na kazi hiyo kwa muda mrefu
akihubiri katika mabasi ya mikoani yanayotumia Barabara ya Mwanza Dar es Saalam.
Baada ya Shigela kuanguka, abiria
waliopatwa na mshangao walimshauri dereva wa basi hilo, Emanuel Deus kumpeleka
hospitali ya karibu ili apatiwe huduma, lakini kabla ya kufika eneo hilo la
kutolea huduma, ilibainika amefariki dunia.
Kifo cha mhubiri huyo kilifanya
dereva alipeleke basi hilo katika kituo cha polisi ambako alitoa taarifa na
polisi kuuchukua mwili huyo na kuupeleka hospitali.
Kwa nyakati tofauti abiria
walieleza kusikitishwa na tukio hilo na kusema ni muhimu kwa binadamu kupima
afya zao kila mara kuliko badala ya kusubiri hadi wanapougua ili kuepuka vifo
vya ghafla.
Mmoja wa abiria hao, Robert Tomas
alisema: “ Watanzania wanatakiwa kujenga mazoea ya kupima afya zao ili kubaini
matatizo yalioyo ndani ya miili yao. Dunia ya sasa ina magonjwa mengi yanayoua watu
kila siku.”
0 comments:
Post a Comment