MKUU wa Polisi wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, Mohamed Mpinga amesema wanafikiria kutoa namba ya simu itakayomwezesha abiria kupiga bure, ikiwa ni njia itakayorahisisha utoaji wa taarifa za madereva wanaovunja sheria za barabarani.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Kamanda Mpinga alisema
baadhi ya abiria hushindwa kutoa taarifa za madereva wanaokiuka sheria za
usalama barabarani kwa kisingizio cha kukosa fedha za kupiga simu.
Kamanda Mpinga alisema kuwa, kutokana na madai hayo ya wananchi,
wameamua kuweka namba hizo za kupiga bure ili ziweze kusaidia kupunguza ajali.
“Katika utoaji wa taarifa kumekuwa na changamoto ya baadhi ya
abiria kushindwa kupiga simu na kutoa taarifa za madereva wanaovunja sheria
kwa kisingizio kuwa, hawana fedha kwenye simu zao,” alisema Mpinga.
Alisema tangu kuanza kutoa elimu kwa abiria ya kuona umuhimu wa
usalama barabarani na kubandika namba za simu kwa ajili ya kutoa taarifa za
madereva wanaoendesha magari kwa mwendo wa kasi kumekuwa na mwitikio mkubwa wa
kupiga simu na kuripoti matukio hayo.
Aliongeza kuwa hata madereva wa mabasi na malori pia wamehamasika
katika kujali sheria za barabarani na wameanza kulindana wenyewe kwa wenyewe, ambapo
huelezana na hata kuripoti sehemu husika ili wachukuliwe hatua za kisheria.
Mpinga alisema baadhi ya abiria hawajui umuhimu wa kuripoti
matukio hayo, ambapo wamekuwa wakichangia kukwamisha kazi hiyo, hivyo wamekuwa
wakiwasakama abiria wanaotoa taarifa na kuwavunja moyo wa kufanya hivyo.
“Wakati mwingine kuna abiria ambao hushabikia mwendo kasi,
wanapoona wenzao wakitoa taarifa huwasakama na kuwaambia washuke,”alisema.
0 comments:
Post a Comment