Waziri wa Sheria na Katiba, Harrison Mwakyembe |
WIZARA ya Katiba na Sheria imesema atakayetoa taarifa za mashahidi wa uhalifu au taarifa za uongo atafungwa kifungo kisichopungua mwaka mmoja au faini isiyopungua Sh milioni tatu au vyote pamoja.
Hatua hiyo imefika ikiwa ni utekelezaji wa sheria ya kulinda watoa taarifa za uhalifu na mashahidi iliyoidhinishwa Julai mosi na Waziri Harrison Mwakyembe kwa mujibu wa kifungu cha 17 cha sheria hiyo.
Mkurugenzi Msaidizi Utekelezaji wa Wizara hiyo, Kamana Stanley alisema jana kuwa kuwapo kwa sheria hiyo kutaimarisha utawala bora na mapambano dhidi ya uhalifu nchini.
“Kuanzishwa kwa sheria hii na utekelezaji wake, kutasaidia kuwapa ulinzi wa kisheria wanaotoa taarifa za uhalifu wa makosa wanayoshuhudia yakitendeka,” alisema.
Alisema sheria hiyo inaelekeza anayefanikisha kuokoa mali za umma, kupatikana kwa wahalifu, kulinda mazingira na maisha ya binadamu kutokana na uhalifu uliopangwa na Mamlaka husika kuifanikiwa kuzuia, kuna utaratibu wa kutoa motisha.
“Mbali na motisha inayotolewa, sheria hiyo itaweka utaratibu wa kufidia waathirika kutokana na taarifa walizotoa,” alisema.
Mkurugenzi huyo alisema utekelezaji wa sheria hiyo, utaisaidia Serikali kuleta matokeo chanya katika kupambana na uhalifu na kukuza ari ya wananchi kusimamia juhudi za kuleta maendeleo zinazofanywa na Serikali.
Alisema sheria hiyo imeweka utaratibu wa kutoa fidia kama mtoa taarifa atapata madhara ya kisasi na mirathi kwa ndugu wa shahidi atakayepoteza maisha.
“Masuala ya usimamizi wa utawala wa sheria yataimarika kutokana na utayari wa wananchi kushiriki mapambano dhidi ya uhalifu kwa kufika katika vyombo vya sheria kutoa ushahidi,” alisema.
Alisema mbali na kuongeza usimamizi wa sheria, lakini sheria hiyo itasaidia kukuza uchumi, kutokana na wananchi wengi kushiriki kufichua maovu pamoja na yanayosababisha hasara kwa Taifa.
Alitaka wananchi kujitokeza bila woga kutoa taarifa za uhalifu ili kusaidia Serikali na kujenga jamii na Taifa linalopinga uhalifu.
0 comments:
Post a Comment