Bosi Polisi ahukumiwa kunyongwa hadi kufa


ALIYEKUWA Mkuu wa Upelelezi wa Jeshi la Polisi wa Wilaya ya Kinondoni, Christopher Bageni (pichani) amehukumiwa kunyongwa hadi kufa, baada ya kupatikana na hatia ya mauaji ya wafanyabiashara watatu wa madini na dereva teksi.

Katika kesi hiyo, aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi wa Mkoa wa Dar es Salaam (RCO), AbdallahZombe na wenzake wawili, wamenusurika baada ya upande wa mashitaka kushindwa kuthibitisha makosa dhidi yao.

Hukumu hiyo ilitolewa jana Dar es Salaam na jopo la majaji watatu; Bernard Luanda, Sauda Mjasiri na Semistocles Kaijage na kusomwa na Msajili wa Mahakama ya Rufaa, John Kahyoza.

Mauaji
Akisoma hukumu hiyo, Kahyoza alisema baada ya kupitia hoja kwenye hukumu ya Mahakama Kuu iliyowaachia huru washitakiwa hao, majaji hao walimwona Bageni kuwa alihusika kwenye mauaji ya watu wanne, hivyo Mahakama ya Rufaa ikatengua uamuzi wa kuachiwa huru kwa bosi huyo.

Jopo hilo lilieleza kuwa baada ya kupitia kwa makini ushahidi uliotolewa na utetezi wa Bageni, ilionesha wazi kuwa alitoa kibalicha wafanyabiashara hao kupelekwa kwenye msitu wa Pande, Mbezi, Dar es Salaam.

Pia jopo hilo lilieleza kuwa mazingira ya ushahidi na utetezi wa Bageni, yanaonesha kuwa alishuhudia mauaji hayo, baada ya Mahakama hiyo kujiuliza swali, la kwa nini aliamuru wafanyabiashara hao wapelekwe sehemu ambayo haina nyumba, kama hakukuwa na lengo la kutekeleza mauaji hayo.

Akiendelea kusoma hukumu hiyo, Kahyoza alisema Bageni pia aliidanganya Mahakama kuwa tukio hilo lilitokea Sinza, wakati wakirushiana risasi na wafanyabiashara hao, kwa madai kuwa ni majambazi na ramani ya tukio hilo ikachorwa.

Hata hivyo, alisema walibaini kwamba kulikuwa na jambo ambalo Bageni alilificha kwa sababu yeye na mashahidi wake wengine wawili, waliidanganya Mahakama kuwa tukio hilo lilitokea Sinza.

“Mahakama imetengua kuachiwa huru kwa Bageni, baada ya kupatikana na hatia katika makosa manne, ambapo katika kosa la kwanza la mauaji ya watu wanne, adhabu yake ni kunyongwa hadi kufa,” alisema Kahyoza.

Baada ya kusema hayo, askari wanne walimzunguka Bageni na kumkamata kwa kumweka chini ya ulinzi ndani ya chumba hicho na baada ya muda kidogo alipelekwa mahabusu.

Zombe
Kwa upande wa Zombe, Ahmed Makelle na Koplo Rajabu, jopo hilo lilisema wakatiwa rufaa
hao hawakupatikana na hati  ya kulinda wauaji kwa sababu upande wa mashitaka, ulishindwa kuthibitisha hilo. 

Pia walieleza kuwa hawawezi kuwatia hatiani wakatiwa rufaa hao, kwa sababu aliyeua hajahukumiwa, kwa sababu mtu anayetajwa kuwa muuaji, hakupata kukamatwa wala kushitakiwa na kati ya wakatiwa rufaa waliokuwa mbele yao, muuaji hakuwapo.

“Hakuna ushahidi wa moja kwa moja, kuonesha kuwa Zombe alishiriki mauaji, kwa hiyo Mahakama inatupilia mbali rufaa hiyo na kuwaacha huru,” alisema Kahyoza kwa niaba ya jopo.
Hata hivyo, jopo hilo lilieleza kuwa Zombe ana kitu kichwani mwake ambacho anakijua. Hukumu hiyo ilianza kusomwa saa 3:49 asubuhi hadi saa 5:14, na ilipofika saa 4, Kahyoza alimwita msaidizi wake na kumnong’oneza kisha mtu huyo kutoka nje.

Baada ya muda kidogo, waliingia askari wawili jambo lililoshangaza watu mahakamani humo, huku ndugu na jamaa wakishusha pumzi na kusababisha minong’ono ya chini kwa chini kutokana na kutojua nini kinaendelea.

Awali, DPP alifanya mabadiliko katika rufaa yake na kumwondolea Zombe kosa la mauaji na kutaka ahukumiwe kwa kuhifadhi wahalifu.

Mkurugenzi huyo alifikia uamuzi huo, baada ya kujiridhisha kuwa hakuna ushahidi wa kumtia hatiani Zombe kwa mauaji.

Katika rufaa hiyo, DPP alidai kuwa Jaji Salum Massati alikosea kuwaacha huru washitakiwa hao, kwa sababu kulikuwa na ushahidi wa kutosha kuwatia hatiani wote.

Katika kesi ya msingi, ilidaiwa kuwa Januari 14, 2006, katika msitu wa Pande, Mbezi Luis, Zombe na wenzake waliwaua kwa makusudi wafanyabiashara watatu wa madini kutoka Morogoro, Mathias Lunkombe, Sabinus Chigumbi na ndugu yake Ephrahim Chigumbi na dereva teksi, Juma Ndugu.

Nje ya Mahakama
Baada ya hukumu kutolewa vilio vilitawala kwenye viunga vya Mahakama hiyo huku aliyedaiwa kuwa mke wake, akilia huku akimlaumu mumewe kwa kufika mahakamani.

Zombe alionekana kupongezwa na ndugu na jamaa kwa kumkumbatia na kumpa pole tangu apate matatizo hayo ya kesi hadi jana, alipoachwa kwa rufaa iliyokatwa na Jamhuri.

Pia kulitokea tukio lingine la kusikitisha ambapo mwanamke aliyedaiwa ndugu wa Bageni alionekana akikimbia hovyo kama mtu aliyerukwa na akili. Hata hivyo haikufahamika mara moja kiini cha hali ile.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo