Grace Gurisha
MAHAKAMA Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam, imetupilia mbali
maombi ya Wakili wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Kharimu Rashidi ya kutaka
waandishi wa habari wasiandike kesi inayomtaka Gavana, Profesa Benno Ndulu
kwenda mahakamani kueleza ni jinsi gani watakavyotekeleza amri kulipa sh.
bilioni 92.
Amri hiyo ilitolewa na Msajili wa Mahakama hiyo, Project Kahyoza ya
kuitaka BoT iilipe Coast Textiles Ltd fedha hizo na kama watashindwa kufanya
hivyo, watafungwa jela kama wafungwa wa kesi ya madai.
Ombi hilo liliwasilishwa jana mbele ya Jaji Ama Munisi wa mahakama
hiyo, ambapo Wakili Rashid alidai kuwa anaona watu wanaandika wakati katika
utambulisho wao hawakujitambulisha na pia hilo linasikilizwa chemba, kwa hiyo
hapaswi mtu mwingine kusikiliza.
Hata hivyo, Jaji Munisi alitofautiana na wakili huyo na kutupilia mbali
hoja yake, kwa kusema kuwa kesi hiyo kweli inasikilizwa chemba, lakini ni suala
ambalo liko wazi. “Hatusikilizi suala hili kwa faragha, ndiyo tunasikiliza
kwenye chumba kidogo, lakini ni suala ambalo liko wazi kwa hiyo kama watu
wanaandika waache waandike,”alisema Jaji Munisi.
Kesi hiyo ilikuja jana kwa ajili ya kusikiliza pingamizi la Coast Textiles
Ltd, ambapo waliomba mahakama hiyo kutupilia mbali maombi ya Gavana na Mafuru
ya kutaka kuzuia utekelezaji wa amri kutakiwa kulipa sh.bilioni 92, lakini
ilishindikana kwa sababu benki hiyo iliwasilisha maombi.
0 comments:
Post a Comment