WIZARA ya Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu imetaka wananchi kuepuka kampuni za uwakala wa ajira nchini ambazo hutangaza nafasi za ajira huku zikiwataka waombaji kulipia ili kusailiwa.
Akizungumza
na JAMBO LEO jana Dar es Salaam Msemaji wa Wizara hiyo, Ridhiwan Wema alisema
kampuni za namna hiyo hawazitambui na hivyo hazina usajili wa kufanya shughuli
hiyo nchini.
“Hizi
kampuni sisi hatuzitambui, mtafuta kazi hatakiwi kutozwa fedha isipokuwa
kampuni inaingia makubaliano na mwajiri ambaye amempa kazi ya kumtafutia
wafanyakazi,” alisema Wema.
Alitaka
wananchi wawe makini na wasikurupuke kutuma maombi kabla ya kujiridhisha kama
kampuni zimesajiliwa na ili kupata taarifa sahihi, mwombaji anaweza kufika
Wizara ya Kazi na kuuliza, kwa kuwa wao ndio wasajili pia wakibaini uwepo wa kampuni
hizo watoe taarifa wizarani na Polisi ili hatua za kisheria zichukuliwe.
Aidha,
aliwasihi wananchi hususan vijana, wasiwe wepesi kulipia gharama, kwa sababu
huduma ya ajira haipaswi kutozwa fedha kwa kuwa si haki kutoa kazi kwa masharti
ya kulipwa, hali ambayo inaashiria vitendo vya rushwa.
Wema
alibainisha kuwa kampuni zinazofanya shughuli za uwakala wa ajira nchini
zimesajiliwa na Wizara ambapo moja ya masharti yanayotakiwa kuzingatiwa ni pamoja
na kutowatoza waombaji wa nafasi za ajira zinazotangazwa.
Alisema
kuna vigezo vingine pia vinavyozingatiwa, ili kukidhi usajili ambapo huainishwa
kwa majina na taarifa za mahali pa kudumu zilipo ofisi za kampuni na kufahamu
kama zimesajiliwa kwenye mamlaka husika, mfano Brela, hayo yote ni kwa ajili ya
kufanya urahisi wa kizifuatilia pindi kunapozuka utata.
Aliongeza
kwamba vigezo vingine ni kujiridhisha kama ina wataalamu wa kutosha kwenye
masuala ya ajira, ambapo baada ya kujiridhisha husajiliwa na kuzitangaza kwenye
vyombo vya habari.
Wema
alitaka wananchi watambue kuwa kampuni zinazotangaza nafasi za ajira huku
zikitaka waombaji walipie fedha kwa ajili ya usaili si salama kwao, hivyo
wanatakiwa kuepukana nazo na kutoa taarifa.
Nuh Yusuf
ambaye ni Ofisa wa kampuni ya Zoom ambayo ni wakala wa ajira nchini, alisema
sababu kubwa ya kuendelea kwa utapeli wa mtandao ni kukosekana kwa ushikiano wa
karibu na vyombo vya sheria hususan Jeshi la Polisi katika kudhibiti suala hilo.
“Tumejaribu
kufuatilia suala hilo TCRA kitengo cha TZ-CERT, tukashauriwa twende Polisi na
mmoja ambaye alipatwa na hilo tatizo, tulipofika kituo cha Polisi cha Oysterbay
hawakuonesha ushirikiano wowote,” alisema Yusuf.
0 comments:
Post a Comment