Akizungumza Dar es Salaam jana, Mkuu wa Idara ya Jiolojia ya UDSM,
Dk Elisante Mshiu alisema kati ya matetemeko yaliyotokea mwaka huu, manne
yalitokea ndani ya miezi 10 iliyopita. Alitaja matetemeko hayo kuwa la kwanza
lilitokea Dodoma Julai 7 likiwa na ukubwa wa 5.1 kwa kipimo cha Richter, Mtwara
5.2, Manyara 4.8 na Kigoma 4.3 huku kubwa zaidi likiwa ni la Kagera la 5.9.
“Tetemeko hili la Kagera ambalo kiini chake kilikuwa ni kilometa 40
lilitokea karibu na mkondo wa Magharibi wa bonde la Ufa la Afrika Mashariki na
kutokana na uhalisia wa kijiolojia na kijiografia, matetemeko zaidi
yanatarajiwa kutokea,” alisema.
Hata hivyo, alifafanua kuwa matetemeko hayo ni ya kawaida na kwamba
kwa mwaka hutokea matetemeko 150 hadi 1,500 duniani yakiwa na ukubwa wa kati ya
Richter 4.5 hadi 5.2.
“Matetemeko ya ardhi hutokana na msuguano na mgandamizo wa miamba
ambayo ikifikia hatua ya kutohimili migandamizo husababisha tetemeko,” alisema.
Aidha, alifafanua kuwa kupitia tetemeko hili wataalamu watapata
fursa ya kujadili na kuangalia kama nchi inaweza kupata matetemeko mengine,
huku akisisitiza kuwa hakuna kifaa kinachoweza kutabiri matetemeko.
Alisisitiza kuwa maeneo yaliyo katika Bonde la Ufa Afrika Mashariki,
yamo hatarini kukumbwa na matetemeko.
Aliihadharisha Serikali ya mkoa wa Dodoma, kutumia wataalamu wakati
wa mchakato wa ujenzi wa majengo, ili kupata utaalamu wa majengo yatakayohimili
matetemeko hayo.
Akizungumzia harambee, Kaimu Makamu Mkuu wa UDSM, Dk Bashiru Ally
alisema itaendeshwa kwa mwezi mmoja na kutaka wachangiaji kutumia akaunti ya
University of Dar es Salaam Self Insurance namba 040103001175 kupitia benki ya NBC.
“Tunahamisha Watanzania wenzetu kujitokeza kuchangia kusaidia
waathirika,” alisema. Pamoja na harambee hiyo, chuo kinataendelea kutoa elimu
na taarifa sahihi kwa umma kuhusu tetemeko la ardhi, kwani ni moja ya nyenzo
muhimu za kukabiliana na majanga ya asili.
“Tutafanya hivi kwa kutoa mafunzo ya muda mfupi na mrefu, kufanya
utafiti na uhamasishaji Watanzania kuongeza mshikamano katika kipindi cha shida
na raha,” alisema.
0 comments:
Post a Comment