CUF yampongeza Jaji Mkuu kuwatimua mahakimu


CHAMA cha Wananchi (CUF), kimempongeza Jaji Mkuu wa Tanzania, Mohammed Chande, kwa kuwachukulia hatua mahakimu 11 na maofisa 23 kutokana na makosa ya nidhamu, sheria na mzaha wa sheria.

Pongeze hizo zilitolewa na Mkurugenzi wa Haki za Binadamu na Sheria wa chama hicho, Kulthumu Mchuchuli hivi karibuni jijini Dar es Salaam.

Mchuchuli alisema uamuzi huo ni wa kupongezwa kwani una lengo la kurekebisha mfumo wa mahakama nchini.

Alisema tume ya utumishi wa mahakama imefanya kazi nzuri ambayo inapaswa kuwa endelevu ili kuujengea heshima mhimili huo muhimu wa kusimamia na kutoa haki kwa wananchi wote.

“Tunapongeza mahakama kuwachukulia hatua mahakimu wakazi, wafawidhi na mahakimu wa mahakama za mwanzo ni vema kuendelea na utaratibu huo ili kurejesha heshima ya nchi,” alisema.

Mchuchuli alisema wananchi wamekuwa wakilalamikia mahakama kuchelewa kutoa maamuzi ya mashauri mbalimbali kwa wakati, na baadhi ya watendaji na mahakimu hujihusisha na vitendo vya rushwa au kutumika kuyaamua mambo kwa misingi ya kisiasa.

Alisema CUF inawapongeza watendaji na mahakimu wanaozingatia maadili, weledi, na juhudi za kuifanya kazi yao kwa umakini na uadilifu mkubwa.

Mchuchuli alisema kitendo cha idara ya mahakama kushughulikia haraka kesi mbalimbali zinazofunguliwa mahakamani zikiwemo zinazohusiana na masuala ya uchaguzi mkuu wa mwaka jana 2015, bila kujali upande upi umeshinda kesi hizo ni cha kupongezwa.

Alisema serikali inapaswa kutatua changamoto ya majaji wa mahakama ya rufaa kufanyiwa kazi mapema na mamlaka husika ili haki ziweze kupatikana kwa haraka kwa wahusika.

“Tunaunga mkono hatua za kukamilisha taratibu za uanzishwaji wa mahakama ya kushughulikia mafisadi kwa maana ya wahujumu uchumi wa taifa na wabadhilifu wa mali za umma,” alisema.

Alisema uanzishwaji wa mahakama hiyo unatokana na msukumo wa kisiasa zaidi bila kuzingatia rasilimali watu (uhaba wa majaji), na watendaji wengine katika idara ya mahakama, haja, hitajio na wakati.

Alisema CUF inaamini kuwa, “utawala wa sheria na mahakama huru ndiyo ngao kubwa ya demokrasia ya nchi yetu” (katiba ya CUF ibara 6(5) katika ibara ya 7(5) inayozungumzia lengo na madhumuni ya chama inaeleza wazi kuwa, “kuondoa mambo yote yanayoruhusu rushwa, ufisadi, ubadhilifu, uonevu, ukandamizaji na ubaguzi wa aina yeyote,” alisema.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo