Fidelis Butahe
MWENYEKITI
wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, anayetajwa kurejeshwa madarakani na Msajili wa
Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi ametangaza kujitenga na Umoja wa Katiba
ya Wananchi (Ukawa), akisema kwa sasa hana nafasi, bali ana kazi ya kukijenga upya
chama chake.
Kauli hiyo
ya Lipumba imekuja siku moja baada ya gazeti hili kuripoti kuwapo hatari ya
Ukawa kufa, ambapo msomi huyo wa Uchumi amesema kazi ya kwanza atakayofanya ni
kuiimarisha CUF na si kukumbatia vyama vya Ukawa.
Lipumba
alitoa kauli hiyo jana asubuhi katika mahojiano maalumu na JAMBO LEO, siku
mbili baada ya kurejea madarakani kwa kauli ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini,
kumtambua kuwa Mwenyekiti halali wa CUF kisheria.
“Ushirikiano
utakuwa wa kimkakati… lengo langu kubwa ni kujenga chama na kuleta maridhiano
ya kisiasa Zanzibar maana tumepata majeraha makubwa. Ukawa ni Katiba ya
Wananchi na tutashirikiana nao (Ukawa) litakapokuja suala la kusimamia maoni ya
Katiba ya Jaji Warioba (Joseph). Ukawa si chama rasmi kinachotambuliwa,” alisema
Profesa Lipumba katika mahojiano hayo.
Hatua hiyo
ya Lipumba inaweza kupunguza nguvu za Ukawa inayojipanga kuwania umeya katika manispaa
nne za Jiji la Dar es Salaam za Kinondoni, Ubungo, Temeke na Kigamboni.
Uchaguzi
huo unakuja baada ya kugawanywa kwa manispaa za Kinondoni iliyozaa Ubungo na
Temeke iliyozaa Kigamboni, huku mvutano ukitarajiwa kuwa mkali iwapo kutaibuka
madiwani watakaomwunga mkono Lipumba ndani ya CUF.
Kauli hiyo
ya Profesa aliyerejea kwenye wadhifa wake baada ya kujiuzulu kutokana na alichoeleza
kuwa ni kutofautiana na uongozi wa chama hicho, pia imekuja siku moja baada ya
wenyeviti wa vyama vinavyounda Ukawa, kutaja mambo manne yanayokwamisha malengo
yao.
Viongozi
hao, Freeman Mbowe (Chadema), James Mbatia (NCCR- Mageuzi) na Mwenyekiti wa Kamati
ya Uongozi wa CUF, Julius Mtatiro walitaja changamoto hizo kuwa ni Dola
kutumika kugawanya vyama hivyo, kuzuiwa kwa mikutano ya hadhara, kupuuzwa kwa
maoni ya Rasimu ya Katiba ya iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba na migogoro
ya ndani inayovikumba vyama hivyo.
Ukawa
iliundwa na vyama hivyo pamoja na NLD mwaka 2013 wakati wa Bunge Maalumu la
Katiba baada ya kususa kushiriki vikao vya Bunge hilo, kwa maelezo kuwa maoni
ya wananchi yaliyokuwa kwenye Rasimu ya Katiba ya iliyokuwa Tume yaliondolewa
na CCM kuweka maoni yake.
Mwaka mmoja
baadaye, vyama hivyo vilisaini makubaliano ya ushirikiano, ukiwamo wa Uchaguzi
Mkuu wa mwaka jana namasuala mengine, huku msingi mkuu ukiwa ni kutaka Katiba
ya wananchi.
Katika
maelezo yake, Profesa Lipumba alisema baada ya kujiuzulu wadhifa wake, CUF
ilidorora huku taswira ya chama hicho ikitoweka machoni mwa watu.
“Kazi
inayonikabili hivi sasa ni kurejesha wanachama wetu pamoja ili kujenga chama na
kutibu majeraha. Baada ya mimi kung’atuka chama kimedorora na taswira yetu haisikiki.
Chama hakifanyi uenezi na kuna wilaya nyingi hazina uongozi. Sitafukuza mtu CUF
zaidi ya kutaka kurekebisha mambo,” alisema.
Alipoulizwa
atafanyaje kazi na wanachama wasiomwunga mkono alisema, “msisome watu
wanachoandika kwenye mitandao ya kijamii. Wanachama wengi wananiunga mkono wala
sina wasiwasi katika hilo hasa Bara, ila Zanzibar kuna ‘sumu’ imemwagwa ila
tutapeana taarifa ili kujenga chama.”
Alibainisha
kuwa kama angekuwa haungwi mkono angekosa nguvu ya kutaka kurejea kwenye chama
hicho, na kusisitiza kuwa lengo lake lilikuwa kustaafu, lakini wanachama wengi
walimfuata nyumbani kumtaka arejee kwenye uongozi.
Akizungumzia
viongozi wa CUF wanaompinga, akiwamo Naibu Katibu Mkuu, Zanzibar, Nassor Ahmed
Mazrui na Mtatiro, alisema ni vijana wadogo kwenye siasa wasiomsumbua na
kubainisha kuwa kama hawana tamaa basi wanatumika.
“Huyu
(Mazrui) wakati sisi tunafanya maandamano Zanzibar kudai mambo ya msingi yeye
alikuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyabiashara wa Zanzibar la Dk Salmin
(Amour- Rais mstaafu wa Zanzibar),” alisema.
“Hawa
vijana wadogo wadogo ambao hawajui michango yangu katika chama wamekuwa wakitoa
kauli zao tu… wapo akina Mtatiro ambao nilimteua kuwa Naibu Katibu Mkuu,
hajagombea nafasi yoyote ndani ya chama ila kwa kuteuliwa,” alisema.
0 comments:
Post a Comment