JPM abana sekta zilizong’ara kwa JK


GAVANA wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Benno Ndulu (pichani) ametoa tathmini ya hali ya uchumi anayoeleza kuwa ukuaji unaridhisha, ingawa takwimu zinathibitisha kuwa sekta zilizoongoza kwa ukuaji wakati wa uongozi wa Rais mstaafu Jakaya Kikwete, zimeporomoka.

Mbali na sekta hizo za enzi za Kikwete kuporomoka, takwimu za BoT zilizotolewa kwenye mkutano wa jana wa Profesa Ndulu na waandishi wa habari, pia zilithibitisha kuwa ukuaji wa uchumi katika robo ya kwanza ya mwaka huu, ni wa chini kuwahi kutokea katika robo za kwanza za mwaka tangu mwaka 2011.

Ukuaji
Kwa mujibu wa takwimu hizo, ukuaji wa kiwango cha juu wa uchumi katika robo ya kwanza ya mwaka tangu mwaka 2011, ulifikia kilele cha asilimia 8.2 mwaka juzi.

Kwa mujibu wa takwimu hizo, mwaka wa pili ambao robo ya kwanza ilikuwa na ukuaji mzuri wa uchumi ni mwaka 2011, ambapo ukuaji ulifikia kiwango cha asilimia 7.9 na kufuatiwa na mwaka 2012 (7.1%); 2013 (6.6%); mwaka jana ukuaji ulikuwa asilimia 5.7.

Mwaka huu katika robo ya kwanza, takwimu hizo zilithibitisha kuwa ukuaji ulifikia kiwango cha chini kabisa cha asilimia 5.5 ikilinganishwa na robo zote za kwanza za mwaka tangu 2011.

Sekta zilizoporomoka
Miongoni mwa sekta zilizoporomoka katika robo ya kwanza ya mwaka huu, ikilinganishwa na robo ya kwanza ya mwaka jana, ni sekta ya ujenzi ambayo mwaka jana ilikua kwa asilimia 23.2 lakini mwaka huu, ukuaji wake umeporomoka na kufikia asilimia 4.3.

Sekta ya usafiri, usafirishaji na uhifadhi wa bidhaa, nayo pia iliporomoka kutoka ukuaji wa asilimia 14.5 katika robo ya kwanza ya mwaka jana, mpaka ukuaji wa asilimia 7.4 mwaka huu.

Ingawa ilielezwa kuwa uzalishaji umeme katika nusu ya kwanza ya mwaka huu umeongezeka kwa asilimia 14.5 kwa uzalishaji kufikia kilowati bilioni 3.45 kutoka kilowati bilioni 3.01, lakini takwimu hizo hizo zilibainisha kuwa katika ukuaji wa shughuli za uchumi, sekta ya nishati pia imeporomoka.

Kwa mujibu wa takwimu hizo, katika robo ya kwanza ya mwaka jana ukuaji wa sekta ya nishati ya umeme ulikua kwa asilimia 10.2, katika robo ya kwanza ya mwaka huu, ukuaji wa sekta hiyo muhimu katika ujenzi wa viwanda, umepungua hadi asilimia 6.

Hata katika sekta ya uzalishaji viwandani, takwimu hizo zilionesha kuwa ukuaji uliporomoka kutoka asilimia 9.9 katika robo ya kwanza ya mwaka jana, hadi asilimia 7.4 katika robo ya kwanza mwaka huu.

Katika sekta ya uuzaji bidhaa wa jumla na rejareja, hali iko hivyo hivyo kwani takwimu hizo zilionesha kuwa iliporomoka kutoka ukuaji wa asilimia 7.3 robo ya kwanza ya mwaka jana hadi asilimia 5.8.

Katika huduma za kitaalamu za ushauri ambazo mara kwa mara hutolewa na wasomi, hali si nzuri pia, kwani ziliporomoka kutoka ukuaji wa asilimia 4.9 hadi asilimia 0.1.

Sekta zilizoneemeka
Pamoja na kuporomoka kwa sekta hizo, baadhi ya sekta ambazo katika utawala wa Kikwete ukuaji wao ulikuwa wa kusuasua, katika robo ya kwanza ya mwaka huu chini ya utawala wa Rais John Magufuli, zilikuwa kwa ghafla, zikiongozwa na sekta ya kilimo iliyoajiri zaidi ya asilimia 70 ya Watanzania.

Takwimu hizo za BoT, zilithibitisha kuwa sekta ya kilimo, ukuaji wake uliongezeka kutoka chini ya asilimia sifuri, yaani asilimia -1.9 robo ya kwanza ya mwaka jana hadi asilimia 2.7.

Aidha, katika mchango wa kisekta kwenye uchumi, sekta ya kilimo ilitoka kuwa na mchango wa chini ya asilimia sifuri, yaani asilimia -8.9 katika robo ya kwanza ya mwaka jana, kwenda kwenye ukuaji wa uchumi kwa asilimia 11 katika robo ya kwanza ya mwaka huu.

Sekta ya huduma za umma nayo ukuaji wake uliongezeka kutoka ukuaji wa asilimia chini ya sifuri, yaani asilimia -1 katika robo ya kwanza ya mwaka jana, hadi asilimia 10.2 katika robo ya kwanza mwaka huu.

Katika sekta ya mawasiliano, ukuaji pia uliongezeka kutoka asilimia 12.8 katika robo ya kwanza ya mwaka jana hadi asilimia 13.4 katika robo ya kwanza mwaka huu.

Sekta ya elimu, ambayo Serikali ya Awamu ya Tano ilipoingia madarakani iliazimia itolewe bure hadi kidato cha nne, ukuaji uliongezeka kutoka asilimia 7.4 katika robo ya kwanza mwaka jana hadi asilimia 8.0 katika robo ya kwanza mwaka huu.

Hata kodi, ambazo ukusanyaji ukiimarishwa husababisha kupungua kwa fedha kwenye mzunguko, tawimu za BoT zilionesha kuwa ukusanyaji kodi za bidhaa nao uliongezeka kutoka asilimia 2 katika robo ya kwanza ya mwaka jana hadi asilimia 6 katika robo ya kwanza mwaka huu.


Miradi ya ukuaji
Akizungumza na waandishi wa habari Gavana Ndulu alisema Tanzania ni nchi ya 10 kwa ubora kati ya nchi zinazokua kiuchumi Afrika na katika Afrika Mashariki, inashika nafasi ya kwanza.

“Kwa kuzingatia mwenendo wa viashiria vya shughuli za uchumi, ni dhahiri kwamba hali ya uchumi wa Tanzania ni nzuri na inatoa matumaini makubwa kwamba lengo la Pato la Taifa kwa mwaka huu la kufikia asilimia 7.2, litafanikiwa.

“Hii inachangiwa pia na Serikali ya Awamu ya Tano kujipanga kuimarisha uchumi endelevu usio na mianya ya rushwa, usimamizi thabiti wa rasilimali za umma na ujenzi wa miundombinu bora, kwa lengo la kujenga uchumi wa viwanda chini ya mpango wa maendeleo wa miaka mitano,” alisema.

Alitaja miradi mikubwa ya viwanda na miundombinu inayoendelea na inayotarajiwa kuanza hivi karibuni na kuchangia katika ukuaji uchumi, ni pamoja na ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa.

Mingine ni ujenzi wa bomba la mafuta la Uganda ambalo litahusu upanuzi wa bandari ya Tanga na ujenzi wa Ukanda Maalumu wa Bidhaa za Nje Kurasini, utakaokuwa mhimili wa biashara kati ya China na ukanda wa Afrika.

Mingine ni mradi wa nishati ya umeme wa kuzalisha megawati 240 wa Kinyerezi II, miradi ya kupanua viwanja vya ndege na ujenzi wa maghala ya Taifa ya kuhifadhi chakula yenye uwezo wa kuhifadhi tani 350 za nafaka.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo