Suleiman Msuya na Celina Mathew
Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad
na Mwenyekiti, Profesa Ibrahim Lipumba aliyetangazwa kuvuliwa uanachama,
wanatarajiwa kukutana uso kwa uso leo hali inayotarajiwa kutoa sura mpya ya
mgogoro wa chama hicho.
Wawili hao wanatarajiwa kukutana kwenye ofisi za makao makuu ya
chama hicho, Buguruni, Dar es Salaam wakati Maalim Seif atakapofika hapo, siku
nne tangu Baraza Kuu la Taifa la CUF lilipotangaza kumvua uanachama Profesa
Lipumba.
Kukutana kwa viongozi hao kutatokea huku Maalim Seif akitafuta
kuonana na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Ernest Manguili kuwasilisha
malalamiko yake dhidi ya Jeshi hilo, ambapo jana alisotea kuonana na kiongozi huyo
bila mafanikio.
Taarifa zilieleza kuwa kabla ya kuingia ofisini, Maalim Seif
atataka kupata ufafanuzi wa mambo mbalimbali wanayoamini Jeshi hilo lina uwezo
nayo, ikiwamo barua ya Msajili wa Vyama vya Siasa nchini ya kumtambua Lipumba
ambayo nakala yake imepelekwa kwa IGP.
“Tangu asubuhi tunawasiliana na Jeshi la Polisi kupitia Msaidizi wa
IGP, hadi ninavyoongea nawe saa tisa hii (alasiri), hakuna msaada tuliopata,”
alisema Mjumbe wa Kamati ya Uongozi ya Chama hicho ambaye pia ni Mbunge wa
Tandahimba, Katani Katani.
Alisema maombi ya upande wa Maalim Seif kukutana na IGP yamejikita katika
kupata ufafanuzi wa barua ya Msajili na mambo mengine ambayo wanaamini kuwa Jeshi
hilo linahusika, hivyo kupaswa kutolea ufafanuzi. Alisema waliandika barua kwa
IGP kuomba kuonana naye lakini walijibiwa na Msaidizi kuwa IGP ana majukumu mengine
hivyo hawataonana naye.
Alisema kuna hali inayowatia shaka katika mchakato wa kurejeshwa
Profesa Lipumba madarakani na kwamba pamoja na wao kumfukuza, bado kuna mambo
wanahitaji ufafanuzi.
Hata hivyo, JAMBO LEO lilipomtafuta IGP Mangu kuzungumzia suala
hilo alisema: “Sina taarifa za watu hao, hata hivyo niko kwenye kikao nadhani
ungewasiliana nao ili wakueleze vizuri wamefikia wapi.”
Hata hivyo, Msaidizi wa IGP aliyetajwa kwa jina moja la Makuri
aliyeelezwa alikuwa akiwasiliana na CUF, alisema: “Ni kweli tumewasiliana nao,
ila mimi si Msemaji wa Jeshi la Polisi, mpigieni Advera (Bulimba) atakuelezeni
kila kitu kwani anajua, nielewe hivyo.”
Lipumba
Akizungumzia ujio wa Maalim Seif, Profesa Lipumba alisema
anamkaribisha na kwamba yuko tayari kufanya naye kazi kwa sababu ofisi yake
ipo.
“Kama Katibu Mkuu (Maalim Seif) anakuja aje, ofisi yake ipo jambo
la msingi akifika aripoti kwangu ili niweze kumpa mwongozo wa kazi za kufanya
tujenge CUF,” alisema Lipumba.
Huku akieleza kwamba hana taarifa ya ujio wa wabunge na mameya wa
CUF kutoka Zanzibar katika makao makuu ya chama hicho, Profesa Lipumba alisema:
“Sijaitisha kikao cha wabunge, kama wamejipanga kuja kufanya vurugu
nawasihi watumie busara zao, ili kumaliza mgogoro ndani ya chama, unaoendelezwa
na wenzetu wa Zanzibar.”
Alisema kwa sasa wapo kwenye utaratibu wa kuhakikisha wakurugenzi
wa idara za CUF wanabadilishwa na kuongeza Makamu Mwenyekiti ambaye alihama
chama na nafasi yake kuwa wazi akisema viongozi hao watathibitishwa kwenye
kikao cha Baraza Kuu.
“Nina mamlaka ya kuteua na kutengua wakurugenzi, na ili waweze kuwa
kamili lazima wathibitishwe, lakini katika kipindi cha mpito wanaweza kuendelea
kufanya kazi kama kawaida,” alisema.
Aliongeza kuwa sakata hilo linazidi kuibua mwamko mpya kwa
wanachama na anapokea simu nyingi huku akisema atazunguka mikoa mbalimbali
nchini, ili kujenga chama, na hawako tayari kuona CUF inakufa Bara.
Alisema wakati mapambano hayo yakiendelea wapo wanachama wenye ari
ya kuhakikisha CUF inajengwa na kwa sasa wana kazi kubwa ya kukuza chama na
mgogoro unamalizika.
Katika hatua nyingine, Profesa Lipumba alisema hana mpango wa
kwenda mahakamani kupinga kutimuliwa kwake kwa sababu anaamini uamuzi wa
Msajili ni wa msingi na Maalim Seif na wenzake sasa wanaubeza, ingawa awali
waliusifu.
0 comments:
Post a Comment