Waagiza mafuta watoa milioni 400/- za tetemeko


Janeth Shekunde

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amepokea Sh milioni 400 na mifuko 1,000 ya saruji kutoka Chama cha Waagizaji Wakubwa wa Mafuta (TAOMAC) kwa ajili ya kusaidia waathirika wa tetemeko
la ardhi hivi karibuni Kagera.

Akizungumza juzi baada ya kupokea msaada huo, Waziri Mkuu Majaliwa pamoja na kushukuru watu binafsi, taasisi na mashirika yaliyojitolea kusaidia waathirika, pia aliwahakikishia kuwa misaada wanayotoa itawafikia walengwa, huku akibainisha kuwa Serikali imejipanga kuzuia kila aina ya wizi au ubadhirifu wa misaada hiyo.

“Tayari tumechukua hatua kwa wahusika wote waliojaribu kucheza na misaada hii. Niwahakikishie tu, kwamba Serikali iko makini kwenye misaada na michango inayoendelea kutolewa, kwa kuwa ni jukumu lake kufanya hivyo, kwa kuwa mnapotoa misaada hii maana yake kuna sehemu mmejinyima,’’ alisema.

Mkurugenzi Mtendaji wa TAOMAC, Salum Bisarara alisema mchango huo ni mwitikio wa ahadi waliyotoa kwenye mkutano wa Waziri Mkuu Ikulu Septemba 13 nakuhusisha wadau kwa ajili ya kuchangia waathirika wa tetemeko hilo.

“Katika kikao kile wanachama wa TAOMAC tuliahidi mambo mawili, kwanza wanachama wenzetu watatu ambao ni GBP, OILCOM na MOIL kuchangia kwa kujenga upya shule mbili za sekondari zilizoathirika ambazo ni Ihungo na Nyakato. Gharama za ujenzi huo tutajulishwa baada ya kukamilika tathmini.

“Pili, wanachama waliosalia tuliahidi kukutana na kuchangisha fedha ili zisaidie waathirika wa tetemeko kwa njia mbalimbali ikiwamo kutengeneza upya miundombinu iliyoharibika hasa zahanati, hospitali, barabara na madaraja, ahadi ambayo tunaikamilisha leo,’’ alisema.

Katika mchango huo jumla ya Sh milioni 244, zilikuwa zimeingizwa kwenye akauntimaalumu ya waathirika hao huku Sh milioni 160, zikiwa ni hundi halisi za kampuni wanachama ambazo zilikabidhiwa kwa Mhasibu Ofisi ya Waziri Mkuu.

Alizitaja kampuni zilichonga kuwa ni pamoja na Mogas Tanzania Ltd, National Oil (T) Ltd, Barrel Petrol Energy, ATN Petroleum Company Ltd, Petroafrica (T) Ltd, TSN Oil, Delta Petroleum, Engen Petroleum, Agusta Energy, Petrofuel, Genera Petroleum, Sahara, TIPER, Hass Petroleum, Lake Oil, Dalbit Petroleum, Camel Oil, Gapco, Oryx Oil Company na Puma Energy.

Aidha, wanachama wa chama hicho walimwahidi Waziri Mkuu kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali katika ujenzi wa Taifa letu huku wakiishukuru Serikali kwa kuwashirikisha kusaidia waathirika wa tetemeko hilo.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo