MADEREVA wanane wa Kitanzania waliotekwa nyara na waasi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), wamehifadhiwa kwenye kambi ya Jeshi hilo nchini humo, baada ya kuokolewa.
Watanzania hao walitekwa juzi wakati waasi wa kikundi cha Mai Mai wa eneo la Namoyo, Kivu Kusini, walipoteka malori 12 na kutaka walipwe dola za Marekani 4,000 kwa kila dereva, ili waachwe.
Hata hivyo, jana taarifa kutoka vyombo vya habari vya kimataifa, zilieleza kuwa Jeshi la DRC, liliwaokoa Watanzania hao, huku Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano cha Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mindi Kasiga akisema Serikali inaandaa utaratibu wa kuwarudisha.
Akizungumza na JAMBO LEO akiwa safarini DRC, mfanyabiashara Azim Dewji, anayemiliki malori manne yaliyotekwa na waasi hao alisema madereva wote wako salama.
Kwa mujibu wa Dewji, hakuna aliyeumia ila walipewa hifadhi na wanajeshi wa DRC kwenye kambi yao kwa ajili ya matibabu. “Mimi niko DRC ambako tukio hilo lilitokea, ni porini na huku niliko mvua kubwa inanyesha. Siwezi kufika huko (kambi ya Jeshi) hadi kesho (leo).
“Madereva wote wako salama na wamechukuliwa na wanajeshi kuhifadhiwa kwenye kambi ya Kindu na kwa matibabu,” alisema.
Msemaji wa Chama cha Wamiliki wa Malori Tanzania (Tatoa), Elias Lukumai aliishukuru Serikali kwa kushirikiana na ya DRC, kuokoa madereva hao ambao maisha yao yalikuwa hatarini baada ya waasi kudhamiria kuwaua.
Lukumai aliyezungumza na gazeti hili, alisema madereva wanatakiwa kuwa makini wanaposafirisha mizigo kwenda nchi nyingine, ili kuepuka changamoto wanazokutana nazo wakati wowote.
“Sisi tunamshukuru Mungu kwani tuliposikia taarifa hizo tuliwasiliana na Serikali na wao wakawasiliana na ya DRC ambao walifanikisha kuwakomboa Watazania hao.
“Tunaomba madereva wetu kutambua kuwa changamoto zipo nyingi hivyo tunapokwenda nchi za watu, tuwe makini kwani lolote linaweza kutokea,’’ alisema.
Alisema Tatoa inaendelea kuwasiliana na Serikali ili madereva hao wasafirishwe kurudi nchini na kwa upande wa magari yalikuwa na bima, lakini pia wataendelea kuwatengenezea mazingira mazuri madereva.
- Blogger Comment
- Facebook Comment
Subscribe to:
Post Comments
(
Atom
)
0 comments:
Post a Comment