Lipumba: Bila mimi CUF haipo



ALIYEKUWA Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba (pichani), ambaye uamuzi wake wa kutangaza kurejea baada ya kujiuzulu nafasi hiyo umezua mtafaruku mkubwa, ameeleza sababu za kuendelea kuwa ndani ya chama hicho.

Amesema hawezi kuondoka CUF na kujiunga na chama kingine chochote cha siasa kwa kuwa anataka kukifanya kiwe imara na cha kitaifa, kinachounganisha wanachama wa pande zote mbili za Muungano; Tanzania Bara na Zanzibar.

Profesa Lipumba (pichani) alisema hayo kwenye mahojiano maalumu, Dar es Salaam jana kuhusu mtafaruku mkubwa baina ya wanachama wanaounga mkono na wanaopinga uamuzi wake wa kurejea kwenye nafasi hiyo.

Alisema baada ya uchaguzi mkuu mwaka jana kwisha, viongozi wa wilaya 104 na wanachama wengi wa CUF, walimfuata nyumbani kwake Dar es Salaam kumwomba arejee kuongoza chama baada ya kuona kinadorora.

“Baada ya uchaguzi mkuu, wanachama walikuja nyumbani kwangu kutaka nirejee, wanachama hawa walikwenda hadi kwa Katibu Mkuu naye akawa amesema hana tatizo nami. Wanachama wanasema hali ya chama ni mbaya, hivyo nirejee kukiimarisha,” alisema Profesa Lipumba.

Alisema wakati chama kikiwa na hali hiyo, hakukuwa na kiongozi wa CUF aliyekuwa akikisemea kukiimarisha, hasa upande wa Tanzania Bara.

Profesa Lipumba alisema hiyo ilikuwa tofauti na upande wa Zanzibar, kwani baada ya uchaguzi mkuu kufutwa visiwani humo Oktoba 26, mwaka jana, Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad, alimwomba atumie ofisi kuu ya chama hicho, Bu-guruni, Dar es Salaam, kuzungumzia hali ya uchaguzi visiwani humo.

Alisema sababu nyingine inayomfanya aendelee kuwa ndani ya chama hicho ni kutoridhishwa baada ya kuona kati ya wilaya 158, ni 104 tu za uongozi wa chama hicho, ndizo zilizofanya uchaguzi mwaka jana.

“Kwa hiyo, ili kuimarisha chama, tunahitaji wilaya 54 zilizobaki, nazo zifanye uchaguzi kwa ajili ya kujipanga kwa uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2018 na uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani mwaka 2020,” alisema Profesa Lipumba. Alisema uthibitisho mwingine wa mikakati ovu ya kukidhoofisha chama hicho ni kitendo cha kusimamishwa uanachama wabunge; Magdalena Sakaya (Kaliua), Maftah Nachuma (Mtwara Mjini) ambao kila mmoja alipambana jimboni na kuangusha vyama vyote, ikiwamo CCM vilivyosimamisha wagombea katika uchaguzi mkuu wa mwaka jana.

“Sakaya ambaye ni Naibu Katibu Mkuu hashirikishwi katika uamuzi chama, ili kutimiza azma yao ya kuniondoa,” alisema.

Alisema hata vikao vilivyotumika kumsimamisha uanachama wa wabunge hao, Sakaya ambaye alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa CUF Tanzania Bara hakushirikishwa katika uandaaji wake.

“Pia unapomfukuza Diwani Handeni, Masudi, alikipigania chama kwa muda mrefu bila kusaidiwa na yeyote, unakiua chama na wilaya nyingine zote zilizo Tanga,” alisema Profesa Lipumba.

Alisema alijitenga na CUF baada ya kuona Katibu Mkuu anafanya mikutano na CHADEMA, bila kushirikishwa.

“Ushirika wetu kwenye UKAWA haukuwa na umoja. Katibu Mkuu alitumia utaratibu kama alivyofanya kipindi cha 1984 dhidi ya Jumbe hali iliyosababisha Jumbe (marehemu Aboud) kuvuliwa madaraka,” alisema Profesa Lipumba.

Alisema pia hakutaka kuwa mpiga debe wa aliyekuwa mgombea urais CHADEMA, Edward Lowassa ndani ya UKAWA, kwa kuwa yeye ana sifa nzuri kuliko Lowassa.

“Na mimi na Dk Slaa (Wilbrod) tulishakubaliana kuwa Slaa agombee, kwa kuwa tulikuwa na ajenda hai zaidi. Katibu Mkuu ndio alikuwa na mazungumzo ya karibu na CHADEMA kuliko mimi,” alisema Profesa Lipumba.

Alisema suala la UKAWA ni la Katiba na kusisitiza kuwa iwapo atarejea atataka kuimarisha chama kwenye wilaya zote na kwamba bado anaunga mkono suala la kupata Katiba mpya.

“Kwenye mkutano uliovurugika juzi, kwanza nilipata barua rasmi kutoka kwa Katibu Mkuu, iliyonishauri nisianze kazi Juni 10, mpaka chama kishauriane na wanasheria.

“Mimi nilitengua uamuzi na kilichokuwa kinasubiriwa ni mamlaka ya uteuzi kujadili tatizo. Kikatiba baada ya kutengua uamuzi wangu mimi tayari nilisharudi kwenye nafasi ya uenyekiti,” alisema.

Alisema katika mkutano huo hakualikwa, lakini kwa taratibu huwa wanaalika watu mbalimbali, lakini akasema alimfuata Katibu Mkuu kujadiliana naye juu ya suala hilo bila mafanikio.

“Nilikuwa nyumbani, nikapigiwa simu nije nithibitishe kuwa kama barua inayosomwa na Katibu Mkuu ni yangu, simu nilipigiwa na wajumbe wa mkutano.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo