MWANASHERIA Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu amesema Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ina hali mbaya kifedha kutokana na madeni inayoidai Serikali na ndiyo maana inataka kuondoa fao la kujitoa.
Lissu ametaka wafanyakazi kutetea maslahi ya mafao yao ambayo
yanatumika vibaya na kwamba hawatakuwa na chochote cha kupoteza watakaposimama kidete
kuyatetea.
Akizungumza na JAMBO LEO jana kuhusu tamko lake lililosambaa kwenye
mitandao ya kijamii, Lissu alisema wafanyakazi wakikaa kimya, watapoteza fedha
na kuwataka kuacha kusikiliza wanasiasa uchwara wanaowashauri kukubali kuacha
mafao yao hadi wafikie umri wa miaka 60.
Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki, alisema: “Ukweli,
kama alivyosema CAG (Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali) kwenye
moja ya taarifa zake za mwaka, mifuko ina hali mbaya ya kifedha.
Hii ndio sababu wenye mamlaka wanataka kuondoa fao la kujitoa. Wameigeuza
mifuko ya hifadhi ya jamii kuwa ‘shamba la bibi’ mpaka inakaribia kufilisika.”
Alisema wanasiasa wanaojivika uzalendo uchwara kuhusu fedha za wafanyakazi,
wao wametengenezewa utaratibu maalumu ambapo wanakatwa na NSSF baada ya
kumaliza ubunge wanarudishiwa fedha zao.
“Wanasiasa uchwara hawasubiri wafikishe miaka 60 ndipo wapate mafao
yao ya kujitoa, wanachowahubiria wao hawakifanyi, wana ndimi mbili kama za
nyoka, wafanyakazi amkeni, hamna chochote cha kupoteza isipokuwa minyororo
yenu,” alisema Lissu.
Alieleza kuwa fedha za mifuko hiyo hazitajenga kiwanda chochote, ni
siasa kutokana na kuwa si za Serikali, ni za wafanyakazi zinazotokana na makato
yao ya mishahara.
Alisema Serikali imekuwa inatumia fedha hizo kama zake, wakati si
zake, inafanya makosa kuzichota inapojisikia bila kurudisha. “Tumeshuhudia mara
kadhaa fedha za wafanyakazi zikitumika kujenga Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) kwa
makubaliano, kwamba Serikali ingerudisha kwa mifuko hiyo, lakini haijarudisha
hata senti moja,’’ alisema Lissu.
Alisema fedha hizo zimejenga jengo la Usalama wa Taifa Oysterbay,
nyumba za Polisi na Machinga Complex, hadi sasa haijarudishwa hata shilingi,
ndiyo maana mifuko inayumba. Alisema fedha hizo zilijenga Daraja la Mwalimu
Nyerere la Kigamboni na kwamba ana uhakika haitarudi hata senti moja.
0 comments:
Post a Comment