Umaarufu isiwe kigezo cha ajira




UCHAMBUZI
 
KATIKA siku za karibuni kumekuwa na tabia ya baadhi ya vyombo vya habari hususan vya burudani kama redio na televisheni kuajiri watu ambao hawana elimu stahiki ya uandishi wa habari.

Jemah Makamba
Watu hao huajiriwa katika tasnia ya habari kutokana na umaarufu wao, huku waliosomea fani hiyo wakikosa nafasi za kuajiriwa ilhali walikaa na kusoma kila kitu kuhusu uendeshaji na usimamizi wa chombo cha habari.

Nafahamu kwamba kwa sasa, upatikanaji wa ajira umekuwa ni mgumu kiasi cha kusababisha wahitimu kutoka vyuo vikuu, kuhangaika kwa muda mrefu bila mafanikio.

Katika dunia ya sasa ambayo kila chombo cha habari kinahitaji weledi wa hali ya juu, ni jambo la kushangaza na kusikitisha kuona waajiri wakishupalia kuajiri watu wasio na elimu ya uandishi na utangazaji wa habari.

Najiuliza kwamba je jambo hilo linatokana na nini? Ni kukengeuka au kulinda maslahi yao? Si jambo jema kwani watu wasio na elimu ya tasnia hiyo ndiyo wanaosababisha kutoaminika kwa vyombo vya habari.

Wengi wao wanakuwa hawafahamu maana ya maadili ya uandishi wa habari, hivyo kujikuta wakiingia katika matatizo yasiyo na tija na wakati mwingine wakisababisha kufungiwa kwa vyombo hivyo kutokana na uchochezi.

Vijana wengi wamekuwa wakihangaika na bahasha za kaki katika vyombo tofauti vya habari kutafuta kazi bila mafanikio lakini anaweza kwenda kwenye redio ambapo anaomba kufanya kazi lakini kutokana na yeye kutokuwa na umaarufu hawezi kupata kazi.

Nimeshuhudia baadhi ya redio na televisheni hapa jijini, wakiajiri watu kutangaza kwa sababu ya umaarufu wao, kitu ambacho hawajawahi kukaa darasani kusomea fani hiyo ila tu kwa vile wao ni maarufu na ni wasanii basi wanapatiwa kazi kwa urahisi kitu ambacho kinaharibu tasnia ya habari.

Nisingependa kuweka wazi majina ya redio mbalimbali ambazo zimekuwa zikiajiri watu kutokana na umaarufu wao, na majina ya wale walioajiriwa kufanya kazi katika redio hizo kutokana na umaarufu wao kwani naamini wanajifahamu.

Katika hali isiyo ya kawaida, watu hao wasiokuwa na elimu kuhusu mipaka na maadili ya uandishi wa habari, wamekuwa wakipewa vipindi waendeshe. Wanafanya hivyo licha ya kuwa kuna watu wangeweza kufanya kazi hiyo kwa weledi zaidi ni hatari kwa chombo chenyewe.

Nasikitika pale ninapoona hadhi ya vyombo vyetu vya habari ikishuka kila kukicha kutokana na hilo.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo