Rais John Magufuli |
Kwa mujibu wa Serikali, kati ya fedha hizo Sh trilioni
51, deni la Serikali lilikuwa dola bilioni 20.5 (Sh trilioni 42.9) huku la
sekta binafsi likiwa dola bilioni 2.7(Sh trilioni 8.1).
Kwa maelezo ya Mbowe ina maana Watanzania takriban
milioni 50 wakiwamo watumishi wa umma, sekta binafsi, wasio na kazi, wastaafu,
vikongwe, wanafunzi hata vichanga, kila mmoja anabeba mzigo huo wa deni la
Taifa kwa kiasi cha Sh milioni 1.3.
Maelezo hayo yalitolewa jana bungeni na Naibu Waziri wa
Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji wakati akijibu swali la Mbunge wa Ubungo
(Chadema), Saed Kubenea ambaye aliitaka Serikali ieleze deni lake ni kiasi gani
na ina mikakati gani ya kukabiliana nalo.
Baada ya swali la Kubenea, Mbowe aliinuka na kuuliza
swali la nyongeza ambapo alifafanua kiasi anachodaiwa kila Mtanzania, hali
iliyomwinua Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba ambaye alisema
deni hilo haliwezi kupimwa kwa utaratibu huo.
Katika swali la msingi, Kubenea alisema Serikali ya awamu
iliyopita ilikopa fedha kwenye benki za nje na za kibiashara; mwaka 2011
ilikopa Sh trilioni 15 na kufanya deni kufikia Sh trilioni 21 kabla ya mwaka
2015, kwamba ilikopa tena Sh trilioni 9 na kulifanya deni kufikia Sh trilioni
39.
Akijibu swali hilo, Dk Kijaji alisema deni la Serikali
lilitokana na mikopo ya ndani na nje kwa ajili ya kugharimia miradi ya
maendeleo, ukiwamo wa kimkakati wa kuboresha majiji, ujenzi wa njia ya umeme wa
msongo wa kilovoti 400 kutoka Iringa mpaka Shinyanga.
Miradi mingine ni mabasi yaendayo haraka, ujenzi wa bomba
la gesi na mitambo ya kusafirisha gesi, upanuzi wa uwanja wa ndege wa Dar es
Salaam na mradi wa maji Ruvu chini na Ruvu juu.
Akieleza mikakati ya Serikali alisema ni pamoja na
kuongeza ukusanyaji mapato, kupunguza matumizi yasiyo ya lazima, kuendelea
kutafuta misaada na mikopo nafuu na kukopa mikopo michache ya kibiashara kwa
miradi yenye kuchochea haraka ukuaji wa pato la Taifa.
Aidha, kudhibiti ulimbikizaji wa madai ya kimkataba kwa
makandarasi na watoa huduma na kudhibiti madeni yatokanayo na dhamana za
Serikali kwenye mashirika ya umma kwa kufanya ufuatiliaji wa karibu.
Dk Kijaji alisema katika kipindi cha mwaka wa fedha
2010/11 Serikali ilipokea mikopo ya nje yenye masharti nafuu na ya biashara Sh
trilioni 1.3 na mwaka 2014/15 ilipokea mkopo wa Sh trilioni 2.3 na kwamba
mikopo hiyo haikufikia Sh trilioni 15 trilioni mwaka 2011 na Sh trilioni 9
kabla ya mwaka jana.
Katika swali la nyongeza, Mbowe alisema deni hilo ni mara
mbili ya bajeti ya Serikali na kwamba kila wananchi milioni 45 wa Tanzania,
kila mmoja anadaiwa Sh milioni 1.2.
“Ni kweli kukopa ni muhimu, lakini tunapaswa kukopa kwa
kujidhibiti kwa kile ambacho tunaweza kulipa na kwa wakati, kwa nini Serikali
isione uwezekano wa kurudishwa katika mpango wa kusamehewa madeni kama
ilivyokuwa nyakati za Mkapa (Benjamin-Rais wa Awamu ya Tatu)?” alihoji.
Akijibu swali hilo, Dk Kijaji alisema Serikali bado
haijaondolewa kwenye mpango wa kusamehewa madeni isipokuwa nchi zilizokuwa
zinatoa msamaha huo, zilisitisha mpango huo kutokana na kukumbwa na migogoro,
zikiwamo Iraq na Iran.
Alisema bado Serikali inaendelea na mchakato wa
kushawishi wadau wa maendeleo ili kuisamehe Tanzania deni hilo.
Akiongezea majibu katika swali hilo, Mwigulu alikanusha
kauli ya Mbowe kwamba hakuna utaratibu wa kupima deni la Taifa kwa kuangalia
wingi wa watu.
“Kwanza naomba niseme kwamba hakuna siku watagongewa
mlango wakidaiwa deni hilo la Taifa, na wala katika Taifa lolote hakuna
utaratibu wa kupima deni kwa kuangalia ujazo wa watu, deni la Taifa linapimwa
kufuatana na uwezo wa ukusanyaji mapato wa nchi husika,” alisema Mwigulu.
0 comments:
Post a Comment