Charles James |
NAITAZAMA nembo ya Taifa kabla ya
kuandika Makala haya na kuvutiwa na maneno ya Uhuru ni Umoja yaliyowekwa
kutokana na busara za Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere.
Umoja ambao Mwalimu Nyerere aliuasisi
haukujali itikadi za kiimani, kisiasa ama aina yoyote ya ubaguzi.
Aliliunganisha taifa ambalo licha ya tofauti mbalimbali za kijamii
zilizokuwapo, watu wakawa wamoja katika utanzania wao.
Mwalimu Nyerere aliamini umoja ni njia
pekee ya kuifanya Tanzania kupata maendeleo, na kwamba kama hakuna (umoja)
kutakuwa na machafuko kama vita ambavyo kwa asili vinazibomoa jamii badala ya
kuzijenga. Rwanda iliwahi kuingia kwenye machafuko ya kisiasa yaliyosababisha
mauaji ya kimbari mwaka 1994, yakawahusisha watu wa kabila za Wahutu na
Watutsi.
Vita kama hiyo, ingawa kwa matokeo
yanayotofautiana imewahi kutokea kwa mataifa jirani ya Burundi na sehemu ya
Jamhuri ya Kidemokrasia na Congo (DRC).
Nchini Kenya, ubaguzi uliojikita katika
misingi ya kikabila ukaibuka baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2007. Sehemu kubwa
ubaguzi huo ulizihusisha jamii za Wakalenjin waliokuwa wanaungwa mkono na Waluo
dhidi ya Wakikuyu.
Ni vurugu hizo ziliowafikisha katika
Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC), Rais Uhuru Kenyetta na Makamu
wake, William Ruto.
Wakati Kenyatta alishutumiwa, pamoja na
mambo mengine, kusaidia kundi la Mungiki kuwaua Wakelenjing na Waluo, Ruto
alihusishwa na mauaji yaliyofanywa na Wakelenjing dhidi ya Wakikuyu na Waluo.
Hiyo ni mifano michache inayothibitisha
hatari inayozikabili jamii zinapoingia katika machafuko hasa yanayotokana na
siasa.
Wakati hali ikiwa hivyo kwa mataifa
hayo, Tanzania ikabaki kuwa mfano wa kisiwa cha Amani katika Mashariki mwa
Afrika na ukanda wa maziwa makuu. Umoja na ukarimu wa raia wake ukatumika kuwa
mfano kwa nchi nyingine za Afrika hasa zilizokabiliwa na machafuko ya kisiasa.
Lakini hivi sasa hali ilivyo Tanzania
ni kama ipo tenge. Tenzi za amani zimegeuzwa kupitia ndimi za viongozi na raia
wa kawaida wanaotaja vurugu na machafuko kila wakati.
Machafuko na hatari za kuvurugika kwa
amani zimekuwa kauli zilizo karibu, hivyo kutoka vinywani mwa wanasiasa kwa
haraka na urahisi. Kengele ya hatari inagonga kichwani mwangu, inakuwa vigumu
kukiamini kinachotokea hapa nchini.
Wapo wanaotaja Mwalimu Nyerere
aliyefariki Oktoba 14, 1999, kwamba kama angekuwa hai basi angesaidia ‘kupozesha’
tishio la kuvunjika kwa amani.
Hakuna maelewano ndani ya vyama vya
siasa, hakuna maelewano kati ya watawala na wapinzani, ushirikiano wa polisi na
raia wa kawaida unadorora, vyombo vya habari vinaendeshwa kwa hofu ya kuhusishwa
na uchochezi.
Siasa zinaonekana kugeuka kutoka uwanja
wa kushindana kwa hoja kuwa uadui. Mwenye ushawishi mkubwa kwa jamii anataka
kuidhihirisha ‘nguvu ya umma’ wakati watawala wanawadhibiti kupitia vyombo vya dola.
Kidogo kidogo, Taifa linashuhudia
matukio ambayo hayakuzoeleka, yakiwa na athari kubwa kwa fikra na ukuaji wa
kizazi cha sasa. Swali la kujiuliza ni kwamba umoja ulioasisiwa tangu kabla na
baada ya uhuru wa Desemba 9, 1961, umekwenda wapi?
Amani inatoweka hadi ndani ya Bunge,
chombo chenye uwakilishi mpana wa raia. Malumbano yanawaibua majemedari
washindi na wanyonge wanaokimbilia kwa wananchi, wakilalamika kuonewa.
Wanaolia kuminywa uhuru wa kuzungumza
ndani ya Bunge na kuamua kwenda kwa wananchi, ‘wanapigwa stop’ kwa tamko la
kutokuwapo mikutano ya kisiasa hadi 2020!
Hatua hiyo inawafanya wafikie ukomo wa
uvumilivu na kuamua kutangaza kwamba utawala uliopo sasa ni wa kidikteta,
wanaunganisha nguvu zao kupitia Umoja wa Kupinga Udikteta Tanzania (Ukuta).
Matukio yote hayo hayatoi dalili njema
kwa nchi kwa maana yanaondoa dhana na uwapo wa amani ya kweli. Angalau kunakuwa
na faraja wanapojitokeza viongozi wa dini na kuushawishi upinzani hususani Chama
cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kutoendelea na maandamano na mikutano ya kisiasa
nchi nzima, ili kuepusha shari.
Amani ambayo Mwalimu Nyerere aliiasisi
na kuihubiri inatafuta njia ya kuelekea wapi ili itoweke katika ardhi ya ardhi
ya Tanzania? Tutumize wajibu. Si muda wa kuonyeshana ubabe hasa kwa wanasiasa.
Taifa liwe tayari kuilinda na kuitetea amani iliyopo.
jambonewspaper@yahoo.com
0 comments:
Post a Comment