Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni |
Wamesema Muswada huo uliotarajiwa kupitishwa jana jioni
baada ya kujadiliwa kwa siku mbili utapitishwa kwa sababu ya wingi wa wabunge
wa CCM, lakini umejaa kasoro na unalenga kuminya vyombo vya habari, watoa
taarifa na kulinda ufisadi unaoweza kufanywa na watendaji wa Serikali.
Wakizungumza katika mjadala huo, wabunge hao waliainisha
baadhi ya vifungu, kikiwamo cha nne, sita, 10 na 19 kupendekeza viondolewe,
huku Mbunge wa Tandahimba (CUF), Katani Ahmed Katani akisema sheria hiyo
inalenga kubana watu katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2020.
Baadhi ya kasoro walizoainisha katika sheria hiyo, ni
pamoja na adhabu kali ya kifungo kwa mtu atakayetoa taarifa za uongo, kuzuia
mtu asiye raia wa Tanzania kupata taarifa, taarifa kutolewa na mamlaka husika
ndani ya siku 30 na sheria kutumika Tanzania Bara pekee.
Kauli za wabunge hao zilipingwa na wabunge wa CCM,
waliosisitiza kuwa Muswada huo ni mzuri na unahitaji marekebisho madogo na
kupingana na kauli ya wenzao wa Upinzani kuwa wadau hawakushirikishwa.
Akizungumzia kifungu cha sita cha sheria hiyo, Mbunge wa
Rombo, Joseph Selasini (Chadema) alisema hakielezi nani anayethibitisha kuwa
taarifa itakayozuiwa kutolewa inalenga kulinda usalama wa Taifa, kwa maelezo
kuwa jambo hilo litakuwa kichaka cha kuficha taarifa muhimu zinazoibua ukweli
kuhusu mikataba ya kifisadi.
“Uko ufisadi wa kutisha ulioibuliwa na taarifa za
uchunguzi, leo hii tunataka kuzuia wanaotusaidia kupata taarifa kwa sababu
Serikali inataka kutengeneza kichaka cha kujibana ili taarifa muhimu zisipatikane,”
alisema.
Huku akisisitiza kuwa Muswada huo utaua uhuru wa vyombo
vya habari na kuvunja haki ya kikatiba ya kutoa na kupata taarifa, alisema
kifungu kinachoeleza kuwa taarifa itatolewa ndani ya siku 30 si sahihi kwa
sababu haiwezi kuwa na maana kama haikutolewa wakati mwafaka.
Alibainisha kuwa sheria hiyo kuelezwa kuwa itatumika
Tanzania Bara pekee wakati Mtanzania anatambulika kama raia wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, ni sahihi, huku akihoji kitendo cha wabunge kutoka Zanzibar
kushiriki mjadala huo wakati hawataitumia sheria husika.
Kauli hiyo ya Selasini iliungwa mkono na Katani
aliyesisitiza kuwa kifungu cha sita kutoa mamlaka ya chombo cha uchunguzi
kuchunguza bila kueleza uchunguzi utafanyika lini, ni jambo linalohitaji
kutazamwa kwa makini.
Mbunge wa Viti Maalumu, Devotha Minja (Chadema) alisema
sheria hiyo inabagua wageni kupata taarifa wakati Tanzania hupata taarifa nyeti
kutoka nchi zinazosaidia kubaini ufisadi, huku akitoa mfano jinsi nchi
zilivyofichua sakata la ununuzi wa rada.
Alisema adhabu ya kifungo cha miaka 15 hadi 20 kwa mtu
atakayetoa taarifa ya uongo ni kubwa na inafanya watu washindwe kutoa taarifa
za awali na kusubiri watoa taarifa wanaotambulika kisheria.
Wakati Minja akisema maoni yaliyotolewa na wadau kuhusu
Muswada huo yameachwa, Mbunge wa Viti Maalumu, Amina Mollel (CCM) alisema wadau
wote walishirikishwa huku akisisitiza kuwa lazima kudhibiti utoaji taarifa,
akitolea mfano habari zilizochapishwa katika gazeti la kila wiki kwamba kifaru
cha Jeshi kimeibwa.
Katika majadala huo, Mbunge wa Ulanga Mashariki Goodluck
Mlinga (CCM) akitumia lugha za vijembe alisema si kila jambo zuri
linalowasilishwa bungeni linalenga kudhibiti wapinzani.
0 comments:
Post a Comment