Kuwa na
mwili wenye unene wa kupindukia ni tofauti na kuwa na uzito mkubwa kuliko
kawaida ingawa watu wengi huchanganya mambo haya mawili na kufikiri kuwa ni jambo
moja.
Unene wa
kupindukia unatokana na kuwa na mafuta mengi mwilini ambayo yanasababisha mtu
kuwa na nyama nyingi ambazo wengine huziita “minyama uzembe” na kitambi. Lakini
uzito mkubwa wa mwili unaweza kutokea pale mtu anapokuwa na misuli mikubwa,
mifupa mikubwa, maji mengi mwilini pamoja na mafuta. Baadhi ya magonjwa na
matumizi ya dawa pia yanaweza kuchagia mtu kuwa na uzito mkubwa.
Watu wenye
tatizo la tezi shingo linalofanya kazi zake chini ya kiwango wanaweza kukabiliwa
na tatizo hili. Matumizi ya dawa kama vile baadhi ya vidonge vya uzazi wa
mpango na dawa za magonjwa ya akili, pia yanaweza kusababisha tatizo la mwili
kuwa na uzito mkubwa.
Wanasayansi
wa afya wamekuwa wakieleza kuwa kuna uhusiano mkubwa na wa karibu sana kati ya
unene wa kupindukia na magonjwa ya moyo, kiharusi, kupanda kwa shinikizo la
damu, saratani za aina mbalimbali, kisukari, kukoroma wakati wa usingizi,
maumivu ya mgongo na uvimbe wa maungio yaani baridi yabisi.
Kutokana na
kupendelea kuwa na umbo la kuvutia na sababu za kiafya, watu wengi hulazimika
kupunguza unene na uzito wa miili yao. Lakini maswali ya msingi ambayo watu
wengi wamekuwa wakijiuliza kuhusu kupungua kwa unene wa mwili ni pamoja na njia
ipi iliyo bora ya kupunguza uzito au unene.
Kwa mujibu
wa wataalamu mbalimbali wa lishe, njia bora na salama ya kupunguza unene na
uzito ni ulaji unaozingatia kanuni za afya na lishe bora kwa kujiepusha na
vyakula vyenye sukari nyingi na mafuta mengi. Njia nyingine ni kufanya mazoezi
kila siku na kujishughulisha kwa kazi mbalimbali zinazohitaji matumizi ya
nguvu.
“Mazoezi ya
kukimbia yanamsaidia mtu kujenga pumzi, kuondoa maradhi madogo madogo na
kupunguza uzito,” anasema Mwalimu wa mazoezi Chiko Yosia. Tafiti zinaonyesha
kuwa unene hutokea pale kiasi kikubwa cha wanga, sukari na protini zitokanazo navyakula
tunavyokula vinapogeuzwa kuwa mafuta na kuhifadhiwa mwilini.
Katika
utafiti huo pia ilibainika kuwa ili kupunguza kilo 10 za mafuta ni lazima
kuvuta hewa safi ya oksijeni kiasi cha kilogramu 29 na kwamba mchakato huo
huzalisha kiasi cha kilo 28 za hewa chafu ya ukaa na kilo 11 za maji.
“Watu
hawawezi kubaini kiasi cha hewa ya ukaa kwa vile hii haionekani kwa macho
wakati tunapopumua,” anasema Meerman mmoja wa wanasayansi waliofanya utafiti huu.
Hata hivyo
watafiti hao wanaonya kuwa kupumua kwa nguvu bila kufanya kazi ngumu au kufanya
mazoezi hakuwezi kusaidia kupunguza unene kwa vile hakuwezi kuvunja muunganiko
wa vimeng’enywa vinavyohifadhiwa katika seli za mafuta yanayotengeneza minyama uzembe
na kuzalisha hewa ya ukaa.
Kupumua kwa
nguvu pekee kunaweza kusababisha kizunguzungu, kiherehere cha moyo na kupoteza
fahamu kutokana na kukosekana kwa ulinganifu wa kemikali za mwili kwa kuingiza
mwilini oksijeni nyingi kuliko kiasi cha hewa ya ukaa inayozalishwa.
“Kwa
kufanya mazoezi madogomadogo ya kukimbia kwa muda wa saa 1 badala ya kubweteka
kwa saa 1, utendaji wa mwili wa kushughulikia mafuta mwilini huongezeka mara saba
zaidi na kuondosha kiasi cha gramu 40 za kaboni mwilini.
Hiyo pia
husababisha kuongezea kwa uwezo wa mwili wa kuondosha kaboni kwa asilimia 20
hadi kufikia kiasi cha gramu 240 kwa siku moja,” inasema sehemu ya utafiti wa
Ruben Meerman na Profesa Andrew Brown.
Utafiti huo
unatoa angalizo kuwa kiasi kikubwa cha kaboni zinazopotea wakati wa kupunguza
unene zinaweza kurudi mwilini kwa njia ya kula vyakula na kunywa vinywaji vyenye
sukari nyingi.
“Kukabili
unene ni jambo linalohitaji kupunguza kiasi cha kaboni unazoingiza mwilini kwa
njia ya kula kuliko zile unazotoa mwilini kwa njia ya kupumua,” wanasema watafiti
hawa.
Ingawa
utafiti huu unatoa ushahidi mpya juu ya uelewa wa namna mwili unavyopunguza
unene, njia za kuupunguza zinabakia kuwa zile zile zinazofahamika kwa muda
mrefu ambazo kwa ufupi ni kupunguza ulaji na kuongeza mazoezi ya mwili.
Maoni
au maswali tuma kwa simu 0713247889
au kwa baruapepe: afya@jamboleo.net
0 comments:
Post a Comment