KUTOKA DAWATI LA ZEZE ‘The Dream Team’
Said Mwinshehe |
KUNA kila sababu ya kupongeza kazi nzuri ambazo zinafanywa na
wasanii mbalimbali nchini. Wamekuwa wakifanya kazi ambazo si tu
zinawatambulisha wao bali na Taifa kwa ujumla. Hongereni wasanii kwa kazi
nzuri.
Baada ya utangulizi huo naomba kutumia nafasi hii kuzungumzia muziki
wa singeli ambao kwa hakika umetokea kupendwa na Watanzania wengi na hasa kundi
la vijana.
Ni aina ya muziki ambao umetokea kukubalika na kupendwa na
walio wengi.Zipo sababu nyingi lakini kwa sehemu kubwa unaonekana ni muziki
ambao umekuja kuleta ushindani dhidi ya Bongo Fleva.
Wakati muziki huo ukiendelea kupendwa kwa kasi ya 4G ni vema
wadau wa muziki huo wakatambua kuwa bado wanakazi ya kufanya ili muziki huo
kukubalika na makundi yote.Bado kuna dhana kuwa muziki huo ni wakihuni.
Dhana hiyo itaondolewa na wasanii wa muziki huo kwa kuonesha
kuwa si muziki wa wahuni na unaweza kupendwa na mtu yoyote.
Profesa Jay kupitia wimbo wa Kazi ambao ameuimba kwa mtindo wa
singeli ameonesha wapi wasanii wa muziki huo wanatakiwa kwenda.Ndio maana kuna
sehemu anawaambia sasa ni wakati wa kusema mapanga No.
Ukweli bado muziki wa singeli unasafari ndefu lakini walioanza
ni vema wakakaza buti ili kuufikisha mahali ambapo kila mmoja wetu ataelewa nini
maana ya singeli.
Najua kuna wengine wanasubiri kuona siku ambayo wasanii wa singeli
wakishirikiana na wasanii wengine huko duniani kuimba muziki huo.Juhudi na
maarifa kwa wasanii wa muziki huo ndio njia sahihi ya kuwafikisha ambako wengi
wanatarajia. Usiwe ni muziki wa vijana tu.
Usiwe muziki kwa ajili ya wahuni peke yao au muziki wa watu
waliokata tamaa ya maisha.Singeli ifike mahali iwe muziki unaopendwa na kila
mtu na hili litawezekana.
Najua wengi wanaoimba muziki huo bado hawajaanza kufikisha ujumbe
wanaokusudia na ndio maana sehemu kubwa umetawaliwa na kelele.Itoshe tu kusema wameanza
vizuri kubwa ni kuendeleza Singeli.
Nafahami ili jambo lifanikiwe ipo haja ya kuwaambia ukweli. Hivyo
Zeze kwa kutumia mamlaka yake katika uwanja wa sanaa na burudani linaona haja
ya kuwakumbusha akina Man Fongo ,Msaga Sumu na wenzao wengine kuwa singeli
inatakiwa kukubalika na kila mtu na si wao kwa wao.
Sawa hata kama haina ushemeji bado iko haja ya kuangalia namna sahihi
ya kuufikisha muziki huo katika kiwango ambacho kitakubalika na walio
wengi.Singeli imekuja na kasi kama vile ile ya mtandao ya 4G lakini wanajua
wanakokwenda?
Kwa maoni -0713833822
0 comments:
Post a Comment