Makonda aomba madaktari 90 JWTZ kupima afya bure Dar


MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, ameomba madaktari 90 kutoka Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ili kusaidia upimaji afya kwa hiari jijini Dar es Salaam.

Upimaji huo ulianza juzi kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja ambapo watu wengi walijitokeza kupima afya hata kuelemea madaktari wa Hospitali Kuu ya Taifa ya Muhimbili waliokuwa wakiendesha upimaji huo.

Makonda alisema hayo jana alipokuwa akitoa salamu zake binafsi za rambirambi kutokana na kifo cha mwanahabari Adolph Kivamwo wakati wa hafla ya kumuaga iliyofanyika kwenye viwanja vya klabu ya viongozi.

“Samahanini kwa kuchelewa, nimekuja hapa kama Makonda na si kama Mkuu wa Mkoa, lakini hata hivyo nimechelewa Mnazi Mmoja ambako mnajua tunaendesha upimaji afya wa hiari kwa wakazi wa Dar es Salaam.

“Tulitarajia kupata watu 3,000 lakini hadi natoka huko walishafika 15,000 hivyo tumelazimika kuongeza siku mbili kuanzia kesho na kuomba pia msaada wa madaktari 90 wa ziada kutoka jeshini,” alisema Makonda.

Alisema idadi hiyo imekuwa kubwa kutokana na watu wengine kutoka mikoani ambako walikodi mabasi madogo yaliyowaleta Dar es Salaam ili kunufaika na ‘ofa’ hiyo ya Mkuu wa Mkoa, Makonda.

Awali alisema magonjwa 10 ndiyo yanayopimwa katika viwanja hivyo, ambayo ni kisukari, saratani ya matiti, tezidume, shingo ya kizazi, figo, moyo na mengine ambayo mwananchi mwenyewe atahitaji kupimwa.

Alisema madaktari bingwa kutoka hospitali kubwa nchini ikiwamo Muhimbili ndio wanaotoa huduma hiyo, ambapo mtu atakayebainika kuwa na tatizo kubwa atapelekwa hospitali husika ambako atapata matibabu.

Katika hafla hiyo ya kumuaga Kivamwo, wengine mashuhuri waliojitokeza ni Mwenyekiti wa IPP, Reginald Mengi, Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete, Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki, Shyrose Bhanji na viongozi mbalimbali wa vyombo vya habari nchini na wa wawakilishi wa Klabu ya Simba ambayo alikuwa mwanachama wake.

Mwenyekiti wa tawi la Simba Dume la Mbezi Luis, aliyetambuliwa kwa jina la Ben alisema tawi hilo litapeperusha bendera ya Klabu hiyo nusu mlingoti kwa siku saba, ili kumkumbuka mwanachama wao huyo.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo