Mbowe aibwaga NHC kortini


MAHAKAMA Kuu Kitengo cha Ardhi, imetupilia mbali mapingamizi yote ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), dhidi ya kampuni ya Mbowe Hotels, inayomilikiwa na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe. Uamuzi huo ulitolewa jana na Jaji Siyovelwa Mwangasi wa mahakama hiyo, baada ya kusikiliza hoja zilizotolewa na shirika hilo na maombi ya Mbowe.

Mbowe kupitia Wakili wake, Peter Kibatala, alifungua shauri namba 722 la 2016 dhidi NHC, akiomba Mahakama itoe amri ili shirika hilo limrudishe katika jengo la shirika hilo, kwa kuwa alipoondolewa utaratibu wa sheria haukufuatwa.

Katika maombi hayo, Mbowe alidai kuwa hakukuwa na notisi na uondoaji huo ulifanywa bila amri ya Mahakama. Pia Mbowe aliomba arudishiwe mali zake zilizochukuliwa na NHC kiholela siku ya uondoaji.

Baada ya Mbowe kuwasilisha maombi hayo, mawakili wa NHC wakiongozwa na Aloyce Sekule, walipeleka pingamizi dhidi ya maombi hayo, kwamba yana makosa kisheria na kwamba mkataba wa umiliki wa pamoja wa jingo kati ya Mbowe na NHC, ulimalizika mwaka 2015.

NHC katika pingamizi hilo, imedai kuwa Mahakama Kuu haina mamlaka ya kusikiliza shauri la Mbowe na kuiomba ifute shauri hilo.

Hata hivyo Mahakama ilitupilia mbali mapingamizi yote ya NHC na kuamuru kesi ya msingi kusikilizwa Septemba 27 mwaka huu.

Kuhusu madai ya NHC, kuwa mkataba wa umiliki wa pamoja wa jengo kati ya Mbowe na NHC ulimalizika 2015, Mahakama ilisema kuwa hilo ni suala linalobishaniwa, hivyo linahitaji ushahidi na mahakama haiwezi kulichukulia juu juu.

Kuhusu madai kwamba mawakili wa Mbowe hawakutumia vifungu sahihi vya sheria, Jaji huyo alisema vilikuwa sahihi. 

Shirika hilo lilichukua mali mbalimbali za kampuni za Mbowe kupitia mawakala wa kampuni ya Fosters Auctioneers katika jingo lililopo makutano ya mitaa ya Mkwepu na Indira Gandhi (Makunganya) jijini Dar es Salaam.

Hatua hiyo ya NHC ilitokana na mgogoro wa muda mrefu, wakimtuhumu Mbowe kushindwa kulipa deni la zaidi ya Sh bilioni 1.3 za kodi ya kupangishwa kwenye jengo hilo.
Share on Google Plus

About Unknown

    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments:

Post a Comment

Laptop City

Tangazo