WAKATI agizo la siku saba la Rais John Magufuli likimalizika jana, Shirika la Taifa la Nyumba (NHC) limesema bado linaendelea na makusanyo ya madeni ya wadaiwa sugu huku likieleza mwishoni mwa mwezi huu taarifa zitatolewa.
Akizungumza jana na JAMBO LEO,
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa NHC, Suzan Omari alisema baada ya tamko la Rais
Magufuli, kitengo cha ukusanyaji bado kinaendelea na ukusanyaji madeni ya kila
mwezi na mchakato utakapokamilika, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo, Nehemia
Mchechu ataweka hadharani kiasi cha fedha kilicholipwa.
“Bado ukusanyaji madeni nchi
nzima unaendelea, baadhi ya wadaiwa wamepunguza madeni yao taarifa halisi zitatolewa
mwishoni wa mwezi huu katika utaratibu uliozoeleka,” alisema.
Alisema baada ya tamko, kuna
wadaiwa waliomba wapewe muda wa kulipa fedha wanazodaiwa.
Alisisitiza kuwa kabla ya agizo
hilo kutolewa, NHC ilikuwa ikidai wapangaji wake takribani Sh bilioni 15 zikiwamo
taasisi za Serikali, wizara, taasisi na watu binafsi.
Hivi karibuni, Rais Magufuli
akiwa Magomeni Kota alitoa siku saba kwa taasisi za Serikali zinazodaiwa malimbikizo
ya madeni na shirika hilo zilipe madeni yao, la sivyo mali zao zitolewe nje.
Pia alimtaka Mkurugenzi wa NHC
kutomwogopa mtu yeyote awe Rais, Waziri, Chadema au kiongozi wa Serikali na
endapo atashindwa kulipa, mali zake zitolewe nje.
Miongoni mwa taasisi zinazoongoza
kudaiwa na NHC madeni ambayo yamefikia zaidi ya Sh bilioni tisa ni Ofisi ya
Rais inayodaiwa zaidi ya Sh milioni 10 na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano inayodaiwa zaidi ya Sh bilioni mbili.
Taasisi zingine ni Wizara ya
Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo inayodaiwa zaidi ya Sh bilioni moja;
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto I zaidi ya Sh
bilioni moja; Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na
Kikanda Sh milioni 613 na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Sh milioni
360.
Mchechu alisema pamoja na deni
hilo, zimo taasisi na watu binafsi ikiwamo ya Mwenyekiti wa Chadema, Freeman
Mbowe ambaye hivi karibuni mali zake zilitolewa nje kwa kushindwa kulipa deni
la Sh bilioni 1.1.
Wakati
huo huo, Meneja Operesheni wa Kampuni
ya Udalali ya Majembe, Nicholaus Mwanasenga amesema oparesheni ya kuwatolea
vitu wadaiwa sugu wa NHC litaendelea Dar es Salaam Ijumaa na Jumtatu ijayo.
“Tunafanya kama kushitukiza tukiwaambia
tunaanza leo inakuwa rahisi kujipanga, ukifanya kwa mtindo huu wengi
unawabamba, “alisema Mwanasenga.
Ofisa Habari wa Kampuni ya
Udalali ya Tambaza, Issa Ramadhan alisema kampuni iko katika hatua za mwisho za
kukamilisha kusaini mkataba na NHC kwa ajili ya oparesheni hiyo na kati ya jana
na leo ulitarajiwa kusainiwa.
0 comments:
Post a Comment