Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu |
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es
Salaam imemgomea Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu kupewa maelezo ya
mlalamikaji ambaye ni Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalumu kwa sababu imefungwa
mikono kisheria.
Uamuzi huo ulifikiwa jana na Hakimu
Mkazi Mkuu wa mahakama hiyo, Dk. Yohana Yongolo baada ya kupitia hoja
zilizotolewa na pande mbili katika kesi ya uchochezi inayomkabili Lissu.
“Kifungu cha 9 (3) cha CPA kinanifanya
nifungwe mikono, kwa sababu upande wa Jamhuri hauwajibiki kuwasilisha maelezo
ya mlalamikaji kwa upande wa utetezi.
“Najua mnaitaka taarifa hii kwa sababu
inahusu mashtaka yanayomkabili mshtakiwa ambayo yanaangukia katika Sheria ya
Magazeti, lakini sheria hiyo iko wazi kabisa kwa sababu tayari upande huo
umesema hautamtumia ZCO (mkuu wa upelelezi) kama shahidi,”alisema Hakimu Dk
Yongolo.
Pia alisema katika suala ambalo aliliomba
wakili wa utetezi, Peter Kibatala la kutaka mkuu huyo aje mahakamani aulizwe
maswali lipo chini ya mamlaka yake, kwa hiyo pale atakapoona inafaa atamuita.
“Kwa wakati mwafaka nitakapoona
anahitajika nitamuita, lakini hivi sasa siwezi kwa sababu hata sijui mazingira
ya kesi yakoje, kwa hiyo nikisema nikubaliane na hilo nitakuwa muongo,”alisema.
Baada ya kusema hivyo hakimu huyo aliahirisha
kesi hiyo hadi Oktoba 5, mwaka huu na kuamuru kuwa siku hiyo mashahidi wawepo
ili kesi ianze kusikilizwa.
Awali, Kibatala alidai kuwa ni haki ya
mshtakiwa kuwa na maelezo ya ZCO kwa sababu yanaweza kutumika kama sehemu ya
ushahidi.
Hata hivyo, Wakili wa Serikali Mkuu,
Bernard Kongola aliipinga hoja hiyo akidai kuwa kwa mujibu wa sheria hawapaswi
kumtumia ZCO kama sehemu ya ushahidi. Anadaiwa alitenda kosa hilo kinyume cha
kifungu namba 32 (1)(b) cha Sheria ya Magazeti iliyofanyiwa marekebisho mwaka
2002.
0 comments:
Post a Comment