HALMASHAURI ya Jiji la Mwanza imewasimamisha kazi walimu wakuu 62 wa shule za msingi na sekondari wilayani Nyamagana wakituhumiwa kuiba Sh milioni 132.5 za ruzuku ya elimu bure na kusajili wanafunzi hewa 5,559.
Mkurugenzi
wa Halmashauri hiyo, Kiomoni Kibamba (pichani), alibainisha hayo jana wakati akitoa
taarifa kwa waandishi wa habari ofisini kwake kuhusu hatua hiyo.
Alisema katika
uhakiki wa wanafunzi hewa Jiji hilo liliunda timu ya wataalamu wa ndani kufanya
kazi hiyo katika shule 38 za sekondari na 78 za msingi ambapo awamu ya kwanza
katika sekondari hizo walipokea idadi ya wanafunzi 24,209, lakini ikabainika
kuwapo tofauti ya wanafunzi 3,809 hewa.
“Takwimu
tulizofanyia uhakiki kwa shule 38 za sekondari zilituonesha kuwapo kwa
wanafunzi hewa 3,809 kati ya 24,209 na kuisababishia Serikali hasara ya Sh
125,265,590 za ruzuku iliyotolewa kwa shule hizo.
“Pia
tulibaini wanafunzi wengine walikuwa wamehitimu kidato cha nne mwaka jana,
lakini bado waliwekwa kwenye orodha kuwa wako shuleni wanaendelea na masomo,”
alisema Kibamba.
Alisema kwa
shule za msingi 78 za Jiji hilo, walipokea idadi ya wanafunzi 75,208 lakini
uhakiki ulipofanyika ili kujiridhisha na kuhesabu mmoja mmoja walipatikana
wanafunzi 73,498 na hivyo kubaini wanafunzi hewa 1,750 na walimu wakuu
walipohojiwa, hawakuwa na majibu ya kuridhisha.
Kibamba
alisema wanafunzi hewa 1,750 waliisababishia hasara Serikali kwa kupeleka
ruzuku ya Sh 7,320,565, huku tume hiyo ikibaini kuwapo wanafunzi waliohitimu
darasa la saba
mwaka jana,
hali iliyolazimu kuundwa tume nyingine ya wajumbe 10 wakiwamo wa vyombo vya
Dola ili kufanya uhakiki upya.
Mkurugenzi
huyo aliongeza kuwa baada ya tume ya pili kurejea upya kufanya uhakiki Machi,
ilibaini kuwa takwimu ambazo tayari zilikuwa zimetumwa Wizara ya Tawala za
Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Idara ya Elimu, ambazo katika uhakiki,
awali zilionesha wanafunzi wa sekondari 38 walikuwa 21,845 na baada uhakiki
walithibitika wanafunzi halali kuwa ni 20,301.
“Uhakiki
huu wa pili ulionesha wanafunzi wa sekondari hewa wangekuwa 1,650 na fedha za
ruzuku zingeletwa na Serikali katika sekondari zao bila kuwapo shuleni.
“Pia
uhakiki huo kwa shule 78 za msingi kwa takwimu za Machi zilizotumwa TAMISEMI,
zilionesha wanafunzi 95,613 lakini halali ni 87,596 tulibaini wanafunzi hewa
8,017 nao fedha zao zingekuja,” alisema.
Aidha,
Kibamba alisema Jiji limechukua hatua za awali kwa kuwasimamisha kazi ili
kupisha uchunguzi zaidi na baada ya kukamilika watawasilisha taarifa kwa Tume
ya Utumishi ya Walimu, ili kuchukua hatua za kimaadili kwa watumishi hao,
wakati uongozi ukijiandaa kuchukua hatua zaidi za kisheria kwa wakuu wa
sekondari 25 na 78 wa msingi waliohusika kusajili wanafunzi hewa, ili wanufaike
na fedha za ruzuku.
“Tulipoamua
kutekeleza agizo la Rais John Magufuli, walimu walidhani tunatania na hivyo rai
yangu kwa watumishi wote wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, wasifanye kazi kwa
mazoea.
“Watekeleze
majukumu yao na waepuke kutoa taarifa za udanganyifu ambazo zitawasababisha wafukuzwe
kazi na kufikishwa kwenye vyombo vya maadili na sheria,” alionya.
Katika
taarifa ya Mkurugenzi huyo, shule za msingi zilizoongoza kuwa na wanafunzi hewa
ni Mbugani (509), Nyakabungo C (528), Nyakato (397), Nyakabungo B (330),
Nyakabungo (492), Igogo B ( 305) Pamba C (362), Moringe (218) Miembeni (256) na
kufanya idadi ya 1,750.
Kwa upande
wa sekondari alisema jumla yake ni 3,809 na kuongeza kuwa uhakiki wa vyeti vya
shule na vya taaluma kwa watumishi linaendelea na limeingia awamu ya pili.
0 comments:
Post a Comment